WABUNGE wameitaka serikali kuja na mpango mkakati wa kutoa ajira za kutosha katika kada za elimu na afya ili kukabiliana na uhaba wa watumishi nchini hali itakayoendana na utekelezaji wa miundombinu uliofanyika hivi karibuni.
Wakichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kwa mwaka 2024/25, walisema sekta hizo zinahitaji ajira za kutosha.
Aidha, baada ya wabunge wanne kuchangia hoja ya ajira, Waziri wa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene amelijulisha Bunge kuwa usiku wa kuamkia jana Rais Samia Suluhu Hassan, alisikia kilio chao na kutoa kibali cha ajira 46,000 kwa kada mbalimbali.
Mbunge wa Nkasi Kaskazini (CHADEMA), Aida Khenani, amesema uboreshaji na ujenzi wa miundombinu ya shule pamoja na sekta ya afya vinatakiwa kuendana na ongezeko la watumishi kwa serikali kutoa ajira za kutosha ili majengo husika yaweze kutumika ipasavyo kwa maslahi ya wananchi.
Amesema kwa sasa serikali ijikite zaidi kupeleka watumishi pamoja na vifaa tiba katika vituo vinavyojengwa, alitaja katika jimbo lake wana upungufu wa walimu shule 175, sekondari upungufu walimu 202, afya watumishi 175.
“Natambua kwamba kuna ujenzi wa madarasa, vituo vya afya pamoja na zahanati kote nchini, lakini jambo hili litakuwa na maana zaidi kama tunaongeza idadi ya madarasa, lazima iendane na idadi ya walimu kwani shida ya Watanzania sio majengo bali ni elimu na huduma bora za afya,” amesema Khenani.
Aidha, ametaja upungufu wa watumishi wengine wanaotegemewa zaidi katika maeneo husika ni pamoja na watumishi saba, watendaji 15 hali inayorudisha nyuma ukusanyaji mapato, watendaji wa vijiji ni 25.
Mbunge wa Nanyamba (CCM) Abdallah Chikota ametaja uhaba wa watumishi katika jimbo lake kuwa mkubwa hali inayoathiri utoaji huduma kwa wananchi.
Amependekeza katika suala hilo waitazame zaidi mikoa ya pembeni kama Mtwara ambako kuna uhitaji wa watumishi sekta ya afya 6,088 na waliopo ni 2,153 pekee, aliiomba TAMISEMI kuomba kibali kwaajili ya kutoa ajira.
Mbunge wa Urambo (CCM), Margaret Sitta amesema suala uhaba wa wafanyakazi kwa sasa ni kubwa katika maeneo mbalimbali na kutaja wilayani kwake kuwa wilaya nzima ina madaktari wanne pekee wakiwa na uhaba wa madaktari 18.
“Hao ni madaktari tu hatujazungumzia kuhusu wahudumu wengine wakiwamo wauguzi, serikali ije na mpango mkakati wa kuongeza watumishi, ikiwa ni pamoja na kada ya walimu yenye uhitaji mkubwa pia,” amesema Sitta.
Mbunge wa Katavi (CCM), Martha Mariki, amesema fedha zilizotumika katika uboreshaji wa miundombinu ya majengo ya shule na afya mkoani kwake wana uhaba wa watumishi kwa sekta ya afya kwa zaidi ya asilimia 57 hali inayosababisha fedha zilizotumika kutokuonekana kazi yake.
AJIRA 46,000
Waziri Simbachawene amesema nafasi hizo 12,000 ni kwaajili ya sekta ya elimu na zaidi ya 10,000 ni kwa upande wa kada ya afya, fursa hizo zitapunguza kwa kiasi kikubwa changamoto ya watumishi kama zilivyotolewa na wabunge.
Akiwasilisha makadirio ya wizara ya OR-TAMISEMI, Mohammed Mchengerwa amesema wizara hiyo itawezesha upatikanaji wa watumishi 400 wa mkataba watakaofanya kazi katika vituo vya kutolea huduma za afya, kulipa mishahara kwa watumishi 400 watakaoajiriwa.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete, amesema kwa mwaka 2023/24 serikali ilitoa nafasi za ajira kada ya walimu 10,505 huku kwa mwaka 2024/25, inatarajia kutoa ajira mpya kwa walimu 10,590 ili kutatua kwa kiwango kikubwa kero zilizopo katika eneo hilo.
Naibu Spika, Mussa Zungu, ameitaka serikali wakati wa kutoa fursa hizo za ajira kutoa ajira kwa walimu wanaojitolea kwa zaidi ya miaka mitatu hadi minne kwa kuwa wameonesha moyo wa kuisaidia serikali kwa muda mrefu.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED