Sintofahamu mjane ataka mwili wa mumewe ufukuliwe

By Neema Hussein , Nipashe
Published at 03:43 PM May 01 2024
Hapa ndipo alipozikwa marehemu Lutiku Bukuku, ambapo mkewe anataka mwili ufukuliwe na kuzikwa kwa Imani ya kiislamu.

WANANCHI mkoani Katavi wamejikuta katika hali ya mshangao baada ya kuibuka mvutano katika familia ya marehemu Lutiku Bukuku, aliyefariki dunia siku chache zilizopita kwa kugongwa na gari, huku baadhi ya wanafamilia wakitaka kufukuliwa kwa mwili huo ili uzikwe kwa mujibu wa taratibu za imani ya kiislam.

 Inadaiwa kuwa marehemu huyo ambae anadaiwa kuzikwa kwa imani ya dini ya kikristo, kabla umauti haujamkuta, alikuwa ameishabadili dini na kuwa muislamu.

Hatua hiyo imekuja mara baada ya Mahakama ya Wilaya ya Mpanda kutoa hukumu ikitaka kufukuliwa kwa mwili huo ili taratibu za maziko zifanyike upya kwa dini ya kiislamu kutokana na mke wa marehemu kwenda kushitaki baada ya mume wake kuzikwa kwa mujibu wa imani ya kikristo.

Wakati wakijaanda kufufua mwili huo, baba wa marehemu hakuridhishwa na hukumu iliyotolewa mahakamani hapo, hivyo aliamua kukata rufaa ili kesi ianze kusikilizwa upya kupitia Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga

Mke wa marehemu, Rehema Rashid amesema mumewake alibadili dini na wakafunga ndoa ya kiislamu mkoani Kigoma na baada ya kubadili dini alipewa jina la Juma Bukuku.

Rashid Seif ni Imamu wa Msikiti wa Maamuri ulipo Nsemlwa, ambapo amesema marehemu alikua anaswali katika msikiti huo na taratibu za dini zinaruhusu mtu kufukuliwa kisha kuoshwa na kuzikwa upya.

Kwa sasa mwili wa marehemu bado hujafukuliwa kutokana na rufaa iliyokatwa na baba wa marehemu na kesi kuanza kusikilizwa upya katika Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga