TAKUKURU yabaini 'madudu' idara ya ardhi

By Marco Maduhu , Nipashe
Published at 04:06 PM Apr 23 2024
Mkuu wa Taasisi ya kuzia na kupambana na Rushwa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga Donasian Kessy akitoa taarifa kwa vyombo vya habari.
PICHA: MARCO MADUHU
Mkuu wa Taasisi ya kuzia na kupambana na Rushwa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga Donasian Kessy akitoa taarifa kwa vyombo vya habari.

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Shinyanga, imebaini kuwapo na urasimu wa utoaji hati miliki na vibali vya ujenzi katika idara ya ardhi Manispaa ya Kahama.

Hayo yamebainishwa leo Aprili 23, 2024 na Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga, Donasian Kessy, wakati akitoa taarifa kwa vyombo vya habari kwa kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka, kuanzia Januari hadi Machi mwaka huu.

Amesema kwa kipindi hicho TAKUKURU imeweza kubaini kuwepo kwa urasimu katika utoaji hati miliki na vibali vya ujenzi na hivyo kusababisha migogoro ya ardhi katika halmashauri hiyo.

“Maafisa ardhi Manispaa ya Kahama, wamekuwa wakilalamikiwa kuwa na urasimu mwingi wa utoaji hati miliki na vibali vya ujenzi,” amesema Kessy.

Aidha, amesema pia kupitia program ya TAKUKURU Rafiki wamefanya ufuatiliaji wa urasimishaji maeneo ya makazi kwa wananchi wa Kata ya Ndala, ambapo wananchi 246 walichanga kiasi cha Sh. Milioni 12.3 na kuulipa Manispaa ya Shinyanga kwa ajili ya kupimiwa ardhi tangu mwaka 2018, lakini hawakuwahi kupimiwa maeneo yao.

Amesema vilevile Wananchi wa Mtaa wa Mlepa Manispaa ya Shinyanga wapatao 1,150 nao walishachanga fedha kwa ajili ya kupimiwa na kurasimishiwa maeneo yao tangu mwaka jana, lakini walikuwa bado hawajapatiwa namba za upimaji wa viwanja vyao.

“Urasimu huu kwenye idara ya ardhi ikiwamo wananchi kutopewa hati miliki na kucheleweshewa kupimiwa maeneo yao licha ya kulipa fedha, imekuwa ikisababisha migogoro ya mipaka na viwanja kutoongezeka thamani kwa kukosa utambuzi rasmi, na hata kusabisha kunyimwa fursa ya kupata mikopo katika taasisi za kifedha,” amesema Kessy.

Aidha, amesema  TAKUKURU ilitoa maelekezo kwa idara za ardhi halmashauri hizo mbili za Shinyanga na Kahama, kwamba kushughulikia kero hizo ili kutosababisha kukithiri kwa Migogoro ya ardhi.

Amesema Manispaa ya Shinyanga, katika mitaa ya Mlepa na Ndala, wameshaanza zoezi la upimaji ardhi na urasimishaji makazi, na hadi sasa namba za viwanja 412 zimeshagawiwa kwa wahusika.

Katika hatua nyingine amesema walifanya ufuatiliaji kwenye utekelezaji wa miradi miwili ya maendeleo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu yenye thamani ya Sh.milioni 224.8, na kubaini dosari ndogo, kwamba katika ujenzi wa jengo la utawala Shule ya Sekondari Ukenyenge, walibaini Milango kutengenezwa chini ya kiwango na vigae kutowekewa 'grouts.'

Mradi mwingine ni ujenzi wa jengo la ‘One Stop Center’ katika Hospitali ya Wilaya ya Kishapu, ambako milango miwili haijafungwa, pamoja na jengo hilo kutopakwa  rangi awamu ya pili.

Ametoa pia wito kwa wananchi wa Mkoa wa Shinyanga, akiwataka waendelee kutoa taarifa za rushwa kwenye Ofisi hiyo  au wapige simu bure 113, ili zipate kushughulikiwa zikiwamo taarifa za utekelezaji wa miradi ya maendeleo.