Utafiti: Asilimia 80 wakazi Mbeya wanakula katika migahawa

By Nebart Msokwa , Nipashe
Published at 05:37 PM Apr 22 2024
Wakazi wa Mbeya waongoza kula migahawani.
PICHA: MAKTABA
Wakazi wa Mbeya waongoza kula migahawani.

ASILIMIA 80 ya wakazi wa Jiji la Mbeya wamebainika wanakula vyakula vinavyoandaliwa kwenye migahawa, hali ambayo inaweza ikawasababishia magonjwa endapo watoa huduma wa migahawa hiyo hawatazingatia usalama wakati wa kuandaa.

Kutokana na hali hiyo, serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeanza kuwapatia mafunzo maalumu mama na babalishe kuhusu kuzingatia usalama wa chakula wanachouza, ili kuwaepusha wateja wao na magonjwa hasa ya mlipuko.

Takwimu hizo zilitolewa na Meneja wa Mradi wa Kuboresha Lishe katika Majiji kutoka Shirika la HELVETAS, Agnes Mahembe wakati wa kutoa mafunzo hayo kwa watoa huduma hao.

HELVETAS ni miongoni mwa watekelezaji wa programu ya uboreshaji wa mnyororo wa thamani wa kahawa, chai na mazao ya bustani (Agri- connect) hasa kwenye kipengele cha kuboresha lishe kwa jamii.

Amesema wengi wa wananchi hao wanakula chakula kinachoandaliwa kwenye migahawa kutokana na shughuli wanazofanya kuwa mbali na nyumbani.

“Lengo letu ni kuhakikisha wananchi wa Jiji hili wanapata lishe bora, wengi wanakula hotelini na kwenye migahawa kwahiyo tumeamua kukutana na hawa mamalishe na babalishe ili tuwape elimu ya namna ya kuzingatia usalama wa chakula,” amesema Agnes.

Mkurugenzi wa Shirika la Chakula Tanzania, Ladislaus Nkomba amesema waliamua kutoa elimu hiyo ili kukidhi matakwa ya sheria za nchi na za kimataifa kuhusu usalama wa chakula kwa wananchi.

Amesema chakula kikiandaliwa kwenye mazingira ambayo usalama wake ni mdogo kuna hatari ya kutokea kwa magonjwa ya mlipuko ambayo yanaweza kugharimu maisha ya wananchi na kulisababishia taifa hasara.

Amesema wanawafundisha watoa huduma hao kwa kuwakusanya eneo moja na ili kupunguza gharama za kwenda kuwatembelea kwenye maeneo yao ya kazi.

Baadhi ya mama lishe na baba lishe ambao walihudhuria mafunzo hayo wamesema kwenye maeneo yao ya kazi wamekuwa wakikabiliana na matatizo mbalimbali ikiwemo kuoneana wivu na kutoelewana hasa kuhusu usafi.

Mmoja wa watoa huduma hao, Efania William amesema asilimia kubwa ya maeneo wanayofanyia kazi ni kwenye masoko ambako kuna mikusanyiko mikubwa ya watu na hivyo kila mtoa huduma anakuwa na wateja wake.

Amesema ikitokea mmoja wa watoa huduma akawa anaandaa kwenye mazingira ambayo siyo rafiki wanaambizana lakini siyo wote wanakubali kutokana na kila mmoja kutokuwa na mafunzo.

“Tunawashukuru wataalamu hawa kwa kutupatia mafunzo haya, kule kwenye maeneo yetu ukimwambia mtu kwamba hapa hapafai kuandalia chakula huwa hatuelewani kwa sababu tu ya kuhisi pengine unamuonea wivu lakini kwa elimu hii naamini kila mmoja atakuwa mwalimu,” amesema Efania.

Akifungua mafunzo hayo, Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Beno Malisa amesema hivi karibuni ugonjwa wa kipindupindu ulilipuka katika baadhi ya maeneo nchini lakini hakuna hata kisa kimoja kilichoripotiwa katika Mkoa wa Mbeya.

Amesema elimu inayotolewa na wataalamu hao ikiendelea kuzingatiwa kuna uwezekano jiji hilo likaendelea kuwa salama zaidi hasa kuwafundisha watu kunawa mikono vizuri na kuandaa chakula kwenye maeneo safi.