Wagonjwa 3,000 wanufaika huduma tiba, upasuaji za madaktari bingwa

By Ashton Balaigwa , Nipashe
Published at 08:10 AM May 20 2024
Wagonjwa wanufaika na huduma tiba, upasuaji za madaktari bingwa.
Picha: Maktaba
Wagonjwa wanufaika na huduma tiba, upasuaji za madaktari bingwa.

WAGONJWA zaidi ya 3,000 kutoka katika wilaya za Mkoa wa Morogoro wamenufaika kwa kupatiwa huduma za tiba na upasuaji kutoka kwa madaktari bingwa wa Dk. Samia Suluhu Hassan, walioweka kambi kwenye hospitali ya rufani ya mkoa huo.

Madaktari bingwa hao wamepangiwa kutoa huduma katika kambi ya Kanda ya Kati inayojumuiisha mikoa ya Morogoro, Pwani, Iringa na Singida.

Akizungumza katika hitimisho ya kambi hiyo iliyofanyika katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Morogoro, Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Mifupa kutoka Hospitali ya Tumbi, Kibaha mkoani Pwani, Dk. Amani Malima, amesema mafanikio hayo yametokana na idadi kubwa ya wagonjwa kujitokeza kupata huduma hizo. 

Dk. Malima ambaye ni Mwenyekiti wa Kambi ya Kanda hiyo iliyokuwa na madaktari bingwa na bingwa bobezi zaidi 50, alisema lengo la awali katika programu hiyo ilikuwa ni kuwaona wagonjwa 2,000, lakini hadi kufikia tamati ya siku tano zilizowekwa wagonjwa 3,128 walionwa.

Amesema lengo la awali la wagonjwa watakaofikiwa, walikadiria kufanya upasuaji kwa wagonjwa 100, lakini kutokana na mwitiko mkubwa wagonjwa 109 walifanyiwa upasuaji na wote walitoka salama, wakati wagonjwa 37 walipatiwa rufani kwenda hospitali za kikanda na kitaifa.

Dk. Malima amesema, idara ya magonjwa iliyoongoza ni magonjwa yasiyoambukiza ama magonjwa ya ndani yakiwamo ya shinikizo la juu la damu, magonjwa ya kisukari na ya moyo.

Naye Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Ndani, Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Morogoro, Hadija Mahamoud, amesema idara yake ya magonjwa ya ndani ilikuwa na wagonjwa wengi akitoa mfano wa siku mbili za mwanzo ilipokea wagonjwa 649.

Dk. Hadija amemshukuru Rais kwa kuwasaidia wananchi hao ambao wamefurahi na huduma zilizotolewa na walitamani ziwe endelevu.

Baadhi ya wanufaika na huduma iliyotolewa na madaktari bingwa hao akiwamo Husna Shaibu, mkazi wa Dumila, Wilaya ya Kilosa, ameshukuru huduma hiyo kutolewa mkoani Morogoro na kuwezesha wagonjwa wengi kufanyiwa uchunguzi na kupatiwa matibabu kwa gharama nafuu.

“Madaktari hawa wamewasaidia wananchi wengi ambao hawakuwa na uwezo na ninamwomba mheshimiwa Rais wetu na wabunge waendelee kutuletea huduma hizi ili sisi wananchi tunufaika kwani maradhi ni mengi na wagonjwa nao ni wengi,” amesema Lukinda.

Mkazi wa Mawenzi, Manispaa ya Morogoro, Ally Said amesema huduma zilizotolewa ni nzuri, lakini muda uliopangwa ni mdogo kutokana na mwitikio wa   wananchi na hiyo inaonesha kuwa Watanzania wengi wanaumwa.

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima, amemshukuru Rais Dk. Samia kwa kuwaleta madaktari bingwa mkoani humo na kuleta faraja kwa wananchi.