Wajukuu watoa ushahidi kortini bibi yao kuwaunguza makalio

By Joctan Ngelly , Nipashe
Published at 08:44 AM May 28 2024
Mahakama ya Wilaya Geita.
Picha: Mtandaoni
Mahakama ya Wilaya Geita.

MAHAKAMA ya Wilaya ya Geita imeanza kusikiliza kesi inayomkabili mkazi wa Mtaa wa Kagera mjini hapa, Anasitazia Maziku (62), anayeshtakiwa kuwachoma moto wajukuu zake wawili.

Mshtakiwa huyo anadaiwa kuwachoma moto kwenye makalio na kuwasababishia majeraha na maumivu, kitendo ambacho ni kinyume cha sheria.

Alipandishwa kizimbani jana mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Nyakato Bigirwa na aliposomewa mashtaka yake alikana kuhusika na makosa hayo na yuko nje kwa dhamana ya wadhamini wawili na mali isiyohamishika yenye thamani ya Sh. milioni tatu kwa kila mdhamini.

Upande wa mashtaka unaongozwa na Mawakili wa Serikali, Mussa Mlawa na Deodatha Dotto, ambao walidai mahakamani wana mashahidi wawili ambao ni waathirika wa tukio hilo na wako tayari kuwasikiliza.

Hakimu Bigirwa alimwuliza mshtakiwa kama yuko tayari kuwasilikiza mashahidi wawili wa upande wa Jamhuri, naye akajibu yuko tayari. 

Baada ya mshtakiwa huyo kudai yuko tayari, Hakimu Bigirwa alimwambia Wakili wa Serikali Deodatha Dotto aendelee.

Shahidi wa kwanza na wa pili; wa kwanza ni mvulana (10) na wa pili ni msichana (7), walidai mahakamani kuwa siku ya tukio hilo, Septemba 22, 2023, mshtakiwa ambaye ni bibi yao aliwatuma wanafunzi hao wa Shule ya Msingi Nyanza kwenda dukani kuchukua betri ya simu.

Shahidi wa kwanza alidai kuwa kutokana na kuchelewa kurejea nyumbani, bibi yao aliwafuata, njiani walipomwona walikimbia hadi nyumbani.

Alidai kuwa bibi yao alipofika nyumbani aliwakamata na kuwafunga kamba mikononi na miguuni kisha kuwacharaza fimbo na baadaye alichukua kiwashio cha randa za mbao na kuwachoma moto kwenye makalio kisha kuwafungua kamba na kuwapa kazi za kufanya.

Alidai kuwa yeye alipewa kazi ya kulima shambani na mdogo wake alipewa kazi ya kuosha vyombo. Baadaye walitoa taarifa kwa baba yao, Shukrani Jumapili ambaye alikwenda Kituo cha Polisi Geita na kufungua shauri kisha kuwapeleka watoto wake wote wawili katika Hospitali ya Mkoa wa Geita kwa ajili ya matibabu.

Baada ya shahidi wa kwanza wa upande wa Jamhuri kumaliza kutoa ushahidi wake, Hakimu Bigirwa alimwuliza mshtakiwa kama ana maswali ya kumuuza shahidi wa upande wa Jamhuri. Naye alidai anayo na kumwuliza shahidi kama kweli alimfunga kamba, kumchoma moto, shahidi huyo akidai kutendwa mambo hayo na mshtakiwa.

Baada ya mshtakiwa huyo kumaliza kumwuliza maswali shahidi wa upande wa Jamhuri, Wakili wa Serikali Dotto aliomba tarehe nyingine kwa ajili ya kuendelea kusikiliza mashahidi wengine waliobakia.

Hakimu Bigirwa alikubaliana na ombi hilo na kuahirisha kesi hiyo hadi Juni 10 mwaka huu kwa ajili ya kuendelea kusikiliza mashahidi waliobakia.