Walimu 39,000 wa sayansi, Hisabati wahitajika

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 01:11 PM Apr 23 2024
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Zainab Katimba
PICHA: MAKTABA
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Zainab Katimba

SHULE zinakabiliwa na upungufu wa walimu wa masomo ya Sayansi na Hisabati 39,610.

Hata hivyo, katika mwaka 2023/24, serikali inategemea kuajiri walimu 12,000 wakiwamo wa masomo ya Hisabati na Sayansi.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Zainab Katimba, amebainisha hayo bungeni jana alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti maalum (Chadema), Esther Matiko.

Mbunge huyo amehoji shule za msingi na sekondari zina upungufu wa walimu wangapi katika masomo ya Sayansi na Hesabu.

Akijibu swali hilo, Katimba amesema mahitaji ya walimu wa masomo hayo nchini ni 71,027 waliopo ni 31,417 na upungufu ni 39,610 sawa na asilimia 55.8.

“Serikali inatambua upungufu wa walimu wa masomo ya hisabati na sayansi katika shule za sekondari nchini. kufuatia upungufu huo, serikali imekuwa ikifanya jitihada kila mwaka kuajiri walimu wa masomo mbalimbali wakiwamo wa masomo ya Sayansi na Hisabati,” amesema.

Amebainisha kuwa kwa mwaka 2020/21 hadi mwaka 2022/23, serikali iliajiri walimu wa masomo ya Sayansi na Hisabati 10,853.

Matiko amesema Halmashauri ya Tarime ina upungufu wa walimu 83 na kuna walimu wa kujitolea 44 sawa na asilimia 53 na kuhoji kwa kuwa serikali inatarajia kuajiri walimu 12,000 kwanini isitenge asilimia 50 ya ajira kwa wanaojitolea ili kutoa motisha kwa walimu wengi kujitolea na kupunguza uhaba uliopo.

Katimba alijibu kuwa wamechukua maoni ya Mbunge na wataona namna ya kuyachakata kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, Utumishi kwa kuzingatia miongozo na taratibu za kiutumishi.

Pia, katika swali la nyongeza, Mbunge wa Viti maalum (Chadema), Tunza Malapo, amehoji mkakati wa serikali wa kutatua tatizo upungufu wa masomo ya Sayansi na Fizikia hilo kutokana na utekelezaji wa mtaala wa mafunzo ya amali.

Naibu waziri Katimba amejibu serikali itazingatia katika ajira za walimu wapatikane wa masomo hayo.

Kadhalika, Spika wa Bunge, Dk.Tulia Ackson ameshauri kuhusu watumishi ikiwamo walimu wanaojitolea, Ofisi ya Rais, Utumishi ilishalieleza Bunge serikali inaandaa mpango maalum kwa ajili yao, TAMISEMI na Utumishi washirikiane ili wapewe kipaumbele kwenye ajira.