Wanafunzi vyuo vikuu kujengewa uwezo kujiajiri

By Faustine Feliciane , Nipashe
Published at 06:44 PM Jun 12 2024
Mkurugenzi mwenza wa taasisi ya empower, Miranda Naiman (wa pili kushoto) akibadilishana nyaraka na Afisa Mkuu wa Tigo Business, John Sicilima.
Picha: Faustine Feliciane
Mkurugenzi mwenza wa taasisi ya empower, Miranda Naiman (wa pili kushoto) akibadilishana nyaraka na Afisa Mkuu wa Tigo Business, John Sicilima.

WANAFUNZI katika vyuo vikuu vitatu nchini watapata fursa ya kujengewa uwezo na maarifa katika kutafuta ajira au kujiajiri baada ya kumaliza masomo yao.

Wanafunzi hao watafaidika kupitia mradi wa 'Generation Empower' ambapo watapewa elimu kupitia semina mbalimbali pamoja na kujifunza kupitia mtandao wa intaneti.

Akizungumza leo kwenye hafla ya utiaji saini makubaliano ya ushirikiano kati ya taasisi ya Empower na Tigo, Mkurugenzi mwenza wa taasisi hiyo, Miranda Naiman, amesema mradi huo utaendeshwa kwa wanafunzi wa vyuo vikuu vya Dodoma (UDOM). Chuo cha Mtakatifu Agustino (SAUT) na Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM).

Amesema kupitia mradi huo wanafunzi watapata fursa kupata elimu juu ya masuala ya ajira pamoja na kujengewa uwezo wa kuweza kujiajiri baada ya kumaliza masomo.

“Ushirikiano huu unasisitiza ahadi yetu thabiti ya kukuza uwezo wa vijana wa Tanzania. Kwa kuwapa ujuzi wa kisasa, siyo tu tunaboresha mwelekeo wao binafsi bali pia tunachangia katika maendeleo ya jumla ya taifa,” amesema Miranda.

Aidha, amesema kupitia ushirikiano huo, wanafunzi hao watakuwa huru kujifunza mambo mbalimbali kwa njia ya kisasa kupitia intaneti ya bure kutoka kampuni hiyo ya simu.

 Amesema wana mkataba wa miaka mitano na UDSM kuendesha mradi huo na sasa wameamua kupanua wigo kwa kuviongeza vyuo hivyo viwili.

Amesema kwa kipindi cha miaka mitatu, mradi huo umewasaidia zaidi ya wanafunzi 6000 katika UDSM.

Ofisa Mkuu wa Biashara wa Tigo, Isack Nchunda, amesema wamejitolea katika maendeleo ya vijana nchini Tanzania na ndiyo sababu ya kushiriki mradi huo.

Mmoja wa wanafunzi kutoka UDSM, Erica Sospeter nayefaidika na mradi huo, amesema mradi huo umefungua macho ya wanafunzi wengi chuoni hapo.