WAZIRI Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba, ametaka Muungano ujikite kuimarisha maisha ya wananchi na viongozi wazungumzie Tanzania zaidi badala ya kuzitenga.
Aidha, zishirikiane katika masuala ya kisera hasa katika uchumi hata kama jambo hilo halipo katika Muungano.
Katika mahojiano maalum yaliyofanyika jana nyumbani kwake jijini Dar es Salaam kuhusu miaka 60 ya Muungano ambayo kila mwaka huadhimishwa Aprili 26, Warioba alisema suala ambalo wananchi wanaweza kulizungumzia ni kuhusu muundo wa serikali na kuwataka ifike mahali waamue.
“Miaka 30 tunazungumzia hili, linatupotezea wakati, badala kuzungumzia maendeleo tunazungumzia siasa za serikali,” alionya.
Alisema, wanakoelekea ni kuimarisha huduma kwa mwananchi jambo litakaloleta umoja zaidi, mshikamano na kulinda amani ya nchi.
Alisema Muungano umesaidia katika umoja na amani, na kwamba jambo la msingi ni kuimarisha maisha ya wananchi.
Alikumbusha kuwa miaka mingi kumeonekana wanazungumzia siasa zaidi na changamoto zinazohusu madaraka.
“Tunapoteza muda mrefu kuzungumzia kuhusu madaraka. Tunapokwenda tunajenga nchi moja hata ukienda katika nchi ambazo zina muungano hawahangaiki kuzungumzia madaraka ya huyu ama yule, nenda India, yale majimbo yana madaraka, lakini wanaangalia maslahi ya India.
“Ni kweli hata viongozi wameendelea kuwa na lugha ya pande mbili. Ninataka tufike mahali tuzungumzie Tanzania, hata siku hizi kuna viongozi unaona mazungumzo yao wanasema serikali ya Bara, sio serikali ya Muungano, anataka serikali ya Bara tena pande zote ni kama wanataka tusiungane,” alisema.
Alionya kuwa kugawanya madaraka kwa kuangalia hilo haliwezi kwenda katika Muungano na kero zote zinazozungumzwa zinahusu madaraka.
“Ninasema hivi tuangalie kero za wananchi, hayo mambo mengine hata hizo kero ukiwauliza wananchi, je, wanazijua watasema, hawazijui,” alisema.
Alitaka watoke katika kuzungumzia madaraka waimarishe zaidi uhusiano na wananchi ili kupata maendeleo na kuachana na matatizo ya kiserikali na kurudi kwao.
“Tunaposema wamefaidika na hiki mara hiki. Sasa ni kuimarisha katika Katiba zote mbili, Katiba ya Muungano na ya Zanzibar kwa mwananchi wa kawaida, yale mambo ya Muungano sio mwongozo wake, yeye (mwananchi) anaangalia haki yake ameipata ya maendeleo,” alisema.
Alisema kipindi kijacho kiwe ni kuimarisha haki zao kwa kuwa, kuna mambo ambayo bado yapo tofauti na ni lazima kuchukuliwe hatua hasa za kimaendeleo.
“Kwa mfano, huduma za afya kwa Mtanzania anataka apate huduma ya aina moja isije akawa anatoka Bara anahuduma ya aina hii, akitoka Zanzibar ana huduma nyingine.
“Kwa maana hiyo, kama kuna mpango wa bima iwe ni ya nchi nzima isije ukawa na bima Bara, ukienda Zanzibar haitumiki au ukiwa na bima Zanzibar, ukija Bara haitumiki ninadhani mambo kama haya tuyaimarishe iwe kwa Watanzania wote,” alishauri.
Katika masuala ya mipango ya kiuchumi, alisema serikali zinatakiwa kushirikiana na yapo mambo mengi ambayo hawawezi kuyaachia kila upande kuandaa sera zake ama mipango yake, lazima kuyatekeleza kwa ushirikiano.
“Mfano uchumi wa buluu unategemea bahari, wanaoshughulika ni Watanzania kutoka pande zote kama unatengeneza sera ni lazima iwe sera moja ili wote waweze kuitumia.
“Mfano mwingine, utalii ni vizuri wakashirikiana wanaotoka nje wanaweza kwenda pande zote kama kuna mtalii anataka kwenda mbugani washirikiane kwa pamoja, badala ya kila upande kuwa na sera yake, inaweza kuleta faida kubwa wanakuja kwa pamoja wanapanga kama wataanzia Serengeti, Ngorongoro na kumalizia Zanzibar, ama wakaanzia Zanzibar na kuja Ngorongoro, Serengeti na Sadaan,” alisema.
“Sera tunazozitengeneza tusije tukaona kwa kuwa suala sio la kimuungano basi unalitengeneza kwa upande mmoja lazima washirikiane,” alishauri.
Alisema unapokuwa hauna sera ya pamoja unaweza kukuta biashara inakuwa tofauti na mtu akitaka kuanzisha kiwanda Zanzibar sera zipo tofauti.
“Mfano ukienda Zanzibar ikifika wakati wa kupiga kura utakuta wanayo sheria ya inasema Mzanzibar Mkazi maana yake ili uwe na haki ya kupiga kura uwe umeishi pale kwa miaka mitatu hii inaweza kuleta matatizo kwa kuwa, unaweza kuishi Unguja ukahamia Pemba mwaka mmoja, unakuja uchaguzi sheria inaonyesha haujaishi miaka mitatu ni kama inawabagua,” alisema.
Alisema serikali ya Zanzibar imefika wakati ione ni mabadiliko gani wanayotakiwa kuyafanya kwa kuwa hayo ndiyo mambo yanayowakera wananchi na yanatakiwa kushughulikiwa.
“Haya mengine kwa kweli bado ninasisitiza mwelekeo wetu uwe ni kuwaungamisha wananchi kwa kila kitu kokote anakoishi, anajua anaishi Tanzania, tuache hii lugha wakati wote kuonesha kuna Tanzania Bara ama Tanganyika na kuna Zanzibar,” alionya.
Hata hivyo, alisema Muungano upo imara changamoto zilizojitokeza ni za kawaida na wananchi wanaupenda.
“Haya tunayosema ni changamoto za serikali zisije kutukatisha tamaa tulipofikia ni mahali pazuri, alisema.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED