Wastaafu PSSSF kicheko kikokotoo kikiongezwa

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:06 PM Jun 13 2024
news
Picha: Mtandao
Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF Abdul-razak Badru.

Wastaafu na wanachama wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma, (PSSSF) sasa wana kila sababu ya kutembea kifua mbele baada ya serikali kuongeza kiwango cha mafao yao ya mkupuo.

Neema hiyo kwa wanachama wa PSSSF ilitangazwa  leo mjini Dodoma na Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba, wakati akiwasilisha Bajeti Kuu ya Serikali.

Wastaafu watapokea asilimia 40  badala ya asilimia 33 iliyokuwepo ambayo ilikuwa ikilalamikiwa na wanachama na wastaafu wa mfuko.

Dk. Mwigulu amesema leo bungeni kuwa Rais Samia Suluhu Hassan amesikia kilio cha wastaafu na wanachama wa mfuko huo na sasa wataongezewa hadi kufikia asilimia 40.

“Suala la ongezeko la kikokotoo limekuwa kilio cha muda mrefu kwa wastaafu na wanachama wa PSSSF, Rais Samia ni msikivu sana kwa hiyo ameongeza kikokotoo kutoka asilimia 33 mpaka kufikia asilimia 40,” amesema Dk. Mwigulu.

Mmoja wa wanachama wa PSSSF, Rashid Hoza aliyezungumza baada ya kuongezeka kwa kikokotoo hicho aliishukuru serikali kwamba imesikia kilio cha wanachama wa mfuko huo.

Amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa uamuzi wake wa kuongeza kiwango cha mafao ya wanachama na wastaafu wa mfuko huo kwani zitawasaidia kuanza maisha mapya wakiwa na fedha za kutosha kuanzia maisha.

“Nampongeza Rais Samia kwa kuwa msikivu kwa wanachama wa mfuko huu tulisema sana na kwa kweli mama amesikia kilio chetu tunamshukuru sana sisi wastaafu watarajiwa,” alisema

Mwanachama mwingine wa PSSSF, Anna Mwombeki alisema ongezeko hilo ni faraja kubwa kwa wastaafu na wanachama ambao ni wastaafu watarajiwa na akapongeza serikali kwa kuwa sikivu.

Amesema wastaafu wengi wanakuwa na wakati mgumu wanapostaafu kutokana na kushindwa kuanzisha biashara hivyo kuongezeka kwa  kikokotoo hicho kutawapa unafuu wa maisha wastaafu hao.

“Tunaipongeza serikali na PSSSF ambayo kwa kweli miaka ya hivi karibuni imeboresha huduma zake karibu zote zipo kidijitali na wanachama wake wanaostaafu wamekuwa wakipata mafao yao chap chap,” amesema