Watetezi watakiwa kushikamana kutoa elimu ya kisheria kwa jamii ya kifugaji

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:04 PM May 28 2024
Mratibu Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) Wakili Onesmo Olengurumwa akitoa elimu kwa watetezi.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mratibu Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) Wakili Onesmo Olengurumwa akitoa elimu kwa watetezi.

Watetezi wa Haki za Binadamu wanaotetea Jamii ya Wafugaji wametakiwa kushikamana kuisaidia jamii hiyo kwa kuwaweka karibu ikiwemo kuwapa elimu za kisheria jamii hiyo ili waweze kuelewa Sheria mbalimbali za nchi.

Mratibu Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) Wakili Onesmo Olengurumwa, amewataka watetezi hao kwa pamoja kuweka umoja na mshikamano katika kazi zao katika kuifikia jamii hiyo.

Amefafanua jamii hiyo inakabiliwa na  changamoto nyingi ambazo zinahitaji ushirikiano katika kuzitatua.

Akizungumza katika hitimisho la mafunzo ya kuwajengea uwezo watetezi wa haki za binadamu wa jamii ya Kifugaji yaliyofanyika  mkoani Arusha leo Olengurumwa amesema kuwa sekta ya ufugaji ni sekta ya pili katika utoaji huduma ya chakula hapa nchini hivyo ni muhimu kwa maendeleo ya Taifa kwa ujumla. 

Amesema jamii hiyo kubwa pia inakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa elimu ya kisheria katika baadhi ya mambo yanayowazunguka katika maisha yao ya kila siku.

"Wekenì nguvu kwa pamoja katika kuifikia jamii hii ya wafugaji nchinii kote" amesema Olengurumwa

Aidha Mwenyekiti​ wa Chama cha Wafugaji Tanzania (CCWT) Mrinda Mshota, amesema kuwa Chama cha Wafugaji kinafanya kazi kubwa ya kuwaunganisha jamii za wafugaji wote hapa nchini ili waweze kufanya kazi kwa pamoja bila kujali wanatoka kabila gani.

Sambamba na hilo Mshota, amesema kuwa suala la wafugaji kuhamia  Ngorongoro, ni suala mtambuka na wametii serikali hivyo linahitaji elimu na majadiliano ya kina  kwa baadhi ya Wafugaji hao ambao bado hawajaridhia kwani maisha ya wafugaji hao yanategemea mifugo kwa maisha yao yote.