Watiwa mbaroni kwa tuhuma kukutwa na meno ya tembo

By Allan Isack , Nipashe
Published at 09:18 AM May 28 2024
Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) George Katabazi.
Picha: Maktaba
Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) George Katabazi.

JESHI la Polisi Mkoa wa Manyara limekamata watu wanne kwa tuhuma za kukutwa na kilogramu 29 za dawa za kulevya aina ya mirungi na meno manane ya tembo.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Babati jana, Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) George Katabazi, alisema watuhumiwa hao walikamatwa katika matukio tofauti. 

Kamanda Katabazi alitaja watuhumiwa hao ni Monica Kamili (48) na mwenzake ambaye hakutaja jina lake, wote wanadaiwa kukamatwa wakiwa na kilogramu 29 za mirungi.

"Watuhumiwa wawili walikamatwa kwa pamoja Mei 21, 2024 majira ya saa 11:30 asubuhi katika Kijiji cha Vilima Vitatu, Kata ya Nkaiti, wilayani Babati," alisema.

Kamanda huyo alisema watuhumiwa hao walikamatwa wakiwa wanasafirisha dawa za kulevya kinyume cha sheria, wakitumia gari aina ya Toyota Succed lenye namba za usajili T 520 DRU.

Katika tukio lingine, kamanda huyo alisema watuhumiwa Richard Lutema (49), mkazi wa Shinyanga, na mwenzake ambaye hakutaja jina, walikamatwa wakiwa na vipande vinane vya meno ya tembo.

"Watuhumiwa wawili wamekamatwa eneo la Mtaa wa Mji Mpya, mjini Babati saa 16:25 jioni Mei 21 wakiwa na vipande hivyo vinane vya meno ya tembo bila kuwa na kibali," alisema Kamanda Katabazi.

Kwa mujibu wa kamanda huyo, wakati wowote kuanzia sasa wanatarajia kuwafikisha mahakamani watuhumiwa hao wanne, upelelezi wa tukio hilo ukikamilika.

"Ninatoa wito kwa wananchi kuacha kujihusisha na biashara haramu za dawa za kulevya na nyara za serikali kwani polisi hatutafumbia macho matukio ya uhalifu," alisema Kamanda Katabazi.

Pia alitoa rai kwa jamii kuendelea kuelimisha wananchi na kuendelea kuliamini Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za matukio ya uhalifu ili hatua za kisheria zichukuliwe.

GARI LA MIRUNGI

Mkoani Shinyanga, mwandishi wetu Marco Maduhu anaripoti kuwa Jeshi Polisi limekamata gari aina ya Nissan lenye usajili namba T.575 CAF lililosheheni dawa za kulevya aina ya mirungi viroba 25 huku dereva akitokomea kusikojulikana.

Kamanda wa Polisi mkoani Shinyanga, Janeth Magomi, akizungumza na waandishi wa habari jana, alisema jeshi hilo linaendelea kumsaka dereva wa gari hilo pamoja na mmiliki wake ili kujibu tuhuma za usafirishaji wa dawa hizo.