WMA yatoa elimu ya vipimo soko la Ilala

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 06:16 PM May 20 2024
Ofisa Tawala wa Wilaya ya Ilala, Charangwe Selemani akigawa mizani kwa vikundi vya wafanyabiashara wa Soko la Ilala Dar es Salaam wakati wa maadhimisho ya siku ya vipimo duniani iliyofanika leo katika soko la Ilala.
Picha: Mpigapicha Wetu
Ofisa Tawala wa Wilaya ya Ilala, Charangwe Selemani akigawa mizani kwa vikundi vya wafanyabiashara wa Soko la Ilala Dar es Salaam wakati wa maadhimisho ya siku ya vipimo duniani iliyofanika leo katika soko la Ilala.

WAKALA wa Vipimo (WMA), imesema utaendelea na operesheni zake za kushtukiza kwenye maeneo mbalimbali ili kuwanaza wafanyabiashara wanaochezea vipimo.

Hayo yalisemwa leo jijini Dar es Salaam na Meneja wa WMA Mkoa wa Ilala, Muhono Nashon, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Vipimo Duniani iliyofanyika kwenye soko la Ilala.

Amesema vipimo vingi vinatumika kwenye maeneo ya masoko na ndiyo sababu WMA imeamua kutoa elimu kwa wafanyabiashara wa soko la Ilala ambapo baadhi ya vikundi vilipewa mizani ya bure kama motisha ya kutumia mizani iliyohakikiwa.

“Wale wanaochezea vipimo tunawasihi waache kwasababu sheria ya sasa ni kali na adhabu imeongezwa, tunawasihi wahakikishe mizani yao imehakikiwa kwa kuweka stika kutoka WMA, kosa moja la kuchezea mzani linaanzia faini ya laki moja hadi milioni 20 kwa hiyo mfanyabiashara akitozwa faini kama hii ni dhahiri atayumba kibiashara,” amesema

Amesema uelewa kuhusu vipimo sahihi umeongezeka kwa kiwango kikubwa na wafanyabiashara wengi wameanza kutumia mizani zilizohakikiwa na wakala.

“Tunapotoa elimu hii tunataka watu wote waache kutumia vipimo vya kienyeji watumie vipimo sahihi na vilivyohakikiwa na tunapofanya msako na kukuta watu wanatumia vipimo batili tumekuwa tukitoa adhabu kali kwa hiyo wafanyabiashara wasisubiri tufanye msako wanapaswa kutii sheria,” amesema

Alisema chimbuko la maadhimisho ya siku ya vipimo ni mataifa 17 yaliyokutana mwaka 1875 yakaamua kusaini mkataba wa haki vipimo ili kuwe na vipimo sahihi kote duniani.

“Lengo la haya mataifa lilikuwa ni kuweka viwango vya vipimo duniani, kwamba ukienda nchi flani unakuta vipimo vinavyotumika ni vile vile vinavyotumika katika nchi mbalimbali,” amesema

Mwenyekiti wa soko la Ilala, Ali Mbiku ameipongeza WMA kwa uamuzi wake wa kuwapa elimu wafanyabiashara wa soko lake ili waweze kutumia vipimo vilivyohakikiwa.

”Mimi binafsi nitaendelea kutoa hamasa kwa wafanyabiashara wa soko hili ili ufike wakati kila mmoja kwenye soko hili awe na mzani uliohakikiwa na wakala ili mnunuzi apate kiwango cha bidhaa kinacholingana na thamani ya fedha alizotoa,” amesema

Naye Katibu Tawala wa Wilaya ya Ilala, Charangwa Selemani amewataka wafanyabiashara kuacha kucheza na vipimo kwani hatua kali zitachukuliwa kwa watakaobainika.

Charangwa amesema kwa muda mrefu serikali imekuwa ikihimiza matumizi ya vipimo sahihi kwa wafanyabiashara kwa kutumia mizani yenye nembo ya WMA na ambayo nisahihi.

“Wafanyabiashara kwenye masoko wamezoea kutumia vipimo vya kienyeji kwa hiyo tumeanza kutoa elimu na kuwapa motisha ya mizani mitano iliyohakikiwa na WMA kwa vikundi vitano vya wafanyabiashara,” amesema

“Tunatoa wito kwa wafanyabiashara wote kuacha kutumia lumbesa na waache kuchezea vipimo kwa hiyo wananchi ombeni kupimiwa bidhaa kupimiwa kwa vipimo rasmi kwasababu hivi vya kienyeji wakati mwingine mnapunjwa,” amesema

Ameipongeza WMA kwa kutoa elimu ya mara kwa mara kwa wafanyabiashara kwani inawajengea uelewa kuhusu umuhimu wa matumizi sahihi ya vipimo ili keupuka faini.