TUME ya Huru ya Taifa ya Uchaguzi inatarajia kufanya uzinduzi wa zoezi la uboreshaji wa daftari la wapiga kura ambapo uzinduzi huo utafanyika Julai mosi, Mkoani Kigoma na unatarajiwa kuzinduliwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Akizungumza na waandishi wa habari, visiwani Zanzibar, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Jacobs Mwambegele, amesema siku hiyo ya uzinduzi pia uboreshaji utaanza katika mkoa huo na kuendelea katika mikoa mingine ya Katavi, Rukwa na Tabora.
Amesema kwa lengo la kutekeleza jukumu hilo kwa ufanisi, uboreshaji utafanyika kwenye mizunguko 13 itakayobainishwa na litaendeshwa kwa siku saba kwenye kila kituo cha kuandikisha wapiga kura.
Amesema watakaohusika kwenye uboreshaji huo wa daftari la kudumu la wapiga kura ni wapiga kura wapya raia wa Tanzania wenye umri wa miaka 18 na zaidi, wapiga kura walioandikishwa awali na ambao wamehama kutoka mkoa au wilaya moja kwenda nyingine ili kuhamisha taarifa zao kutoka kata au jimbo walioandikishwa awali.
Amesema zoezi hilo litatoa fursa kwa wapiga kura walioandikishwa kurekebisha taarifa zao, kutoa kadi mpya kwa wapiga kura waliopoteza kazoo zao au kuharibika na kuondoa wapiga kura waliopoteza sifa kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo ya kuukana uraia wa Tanzania na kifo.
Amesema daftari linatarajiwa kuwa na wapigakura 34,746,638 kutoka 29,754,699 ya mwaka 2020 ambapo ni ongezeko la wapiga kura wapya 5,586,433 sawa na asilimia 18.7.
Mwenyekiti huyo amesema wapiga kura 4,369,531 wanatarajiwa kuboresha taarifa zao na wapiga kura 594,494 wataondolewa katika daftari kwa kupoteza sifa za kuwa wapiga kura.
Amesema kwa mara ya kwanza wafungwa gerezani na watuhumiwa waliopo mahabusu watapata fursa ya kuandikishwa katika daftari la wapiga kura ili kupata haki yao ya kupiga kura katika uchaguzi wa mwaka 2025, lakini ni kwa wale wanaotumikia kifungo chini ya miezi sita.
Mkurugenzi wa uchaguzi wa Tume hiyo, Kailima Ramadhani, amesema uandikishaji wa daftari la wapiga kura utagharimu Sh. bilioni 418.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED