Binti mwenye kifafa, aliyesomea udaktari adumu kuwa balozi na fani tiba imwajiri

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 07:20 AM May 23 2024
Isrey Ayoub.
Picha: Christina Mwakangale
Isrey Ayoub.

ISREY Ayoub (25) ni shujaa wa kifafa. Amefanya mitihani ya taifa mara mbili, kidato cha nne na cha sita akiwa na hali hiyo.

Mara kadhaa akiwa pekee yake shule ya bweni, alikuwa na hali ya kuogopa inayoitwa ‘hallucination’, hisia zilizomfanya akipita eneo tulivu ahisi kuna hatari imemzingira.

Isrey, alianza matibabu ya afya ya akili Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe (sasa Taasisi ya Taifa ya Afya ya Akili) mwaka 2016, akiwa kidato cha nne, huku dalili hizo zikianza akiwa kidato cha kwanza.

Binti huyo mtoto wa mwisho kati ya watano, katika familia yao, ameielezea Nipashe katika mazungumzo maalum hivi karibuni, katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dar es Salaam, katika kufahamu changamoto anazopitia pamoja na matarajio yake, takribani miaka minane tangu agundulike anaugua kifafa.

Yafuatayo ni mazungumzo yake, ya maswali na majibu na mwandishi wa makala hii:

SWALI: Jina lako ni nani na una umri wa miaka mingapi? Pia, unaweza kuelezeaje hali yako?

JIBU: Naitwa Isrey Ayoub. Mimi ni miongoni mwa wanaopata changamoto ya kifafa. Nina miaka 25.

Kwa takribani miaka sita sasa, hali imekuwa ikinipata rasmi nikiwa kidato cha nne. Nilikuwa nakutwa na degedege mara kwa mara, nilipokuwa kidato cha nne.

Baada ya hapo, sikufahamu nilikuwa naumwa nini. Nilikuwa nasoma shule ya bweni, hivyo mara nyingi nilikuwa narudi nyumbani, napatiwa dawa kama vile za kupaka.

Nilikuwa nikisali sana, nikitumia dawa za kujifukiza kutoka kwa waganga wa kienyeji. Lakini kulikuwa hakuna matokeo yoyote, nikamaliza kidato cha nne.

Shule ya sekondari nimesoma Kazima, ipo mkoani Tabora. Wazazi wangu walikuwa wanakaa Dodoma. Niliporudi, wazazi wakaniona kwa mara ya kwanza nikiumwa, kumbuka nilikuwa niko shule ya bweni, kwa hiyo kilichokuwa kinanisibu wazazi wangu walikuwa hawajui.

SWALI: Kwa mara ya kwanza wazazi wako walipogundua una tatizo hilo, nini kilitokea?

JIBU: Wazazi wangu mara ya kwanza, mama akaniona na baba, sijui walibaini nini. Nikaumwa mara tatu au mara nne nikawa naenda kwa kiongozi wa dini ‘ustadhi’ ananiombea, kwa kuamini kwamba ilikuwa ni mapepo, pepo wabaya.

Baada ya hapo, baba akasema ngoja twende Mirembe Hospitali (Taasisi ya Taifa ya Afya ya Akili) ... tumefika Mirembe, nikakutana na daktari. Ingawa kabla ya hapo nilielezea historia yangu.

Nikiwa kidato cha kwanza, nilikuwa nakumbwa na ‘hallucination’ (woga na fikra zisizio sahihi kama harufu, kadhia au kuguswa, ikijenga woga).’

Nilikuwa nasoma kijijini (bweni), kulikuwa na miti, mibuyu. Nilipopita, nahisi kama nakumbwa na watu wa hatari, naogopa, hii hali wanaita ‘hallucination’.

Unajihisi kama uko eneo tofauti na eneo halisi ulipo. Nahisi nimegubikwa na nguo nyingi. Nikaelezea hivyo kwa daktari. Yaani hata kulala peke yangu nilikuwa naogopa. 

Nilikuwa nalala na mama, baba. Kwa hiyo nilivyokuwa Tabora nikizipata hisia hizo, naogopa ‘nahisi anxiety (wasiwasi) napita pembeni kama nipo njiani. 

Nakumbuka daktari akaandika ‘epilepsy’ (kifafa), nikajisemea ahaaa! Nikapewa dawa za vidonge za mwezi, ilikuwa mwaka 2016. Kwa mwezi mmoja nikazitumia.

Nikarudi mwezi mwingine tena kuchukua dawa. Matokeo ya kidato cha nne yalitoka. Kliniki yangu ya kwanza ilianzia Mirembe. Dawa natumia mara moja kwa siku, kila siku usiku, vidonge vinakuwa vinne, hadi sasa.

Kila siku natumia dawa, mimi ni msichana, ni binadamu! Kumbuka kuna muda mwingine ninasahau, nachoka kumeza. Nikaenda sekondari ya juu, Bwiru Girls, sio kama nilikuwa sipati hizo ‘episode’ (vipindi), za degedege nilikuwa napata.

Nilikuwa napata pengine kwa sababu ya uzembe, simezi dawa. Lakini, kumbuka mzazi yeyote huwa anatarajia na kufanya kila awezalo, ili mtoto wake apone.

Kwa hiyo, nikawa naendelea kujifukiza, nikawa napelekwa kwa waganga tofauti, ili hii hali iishe. Nibaki kuwa Isrey yule wa kwanza. Changamoto nyingi nilizipata shuleni, nikamaliza elimu sekondari ya juu.

SWALI: Ulipohitumu kidato cha sita ndoto zako au ulitarajia kujiunga na elimu ya juu?

JIBU: Nilipomaliza kidato cha sita, nikajiunga na St. David College Health & Allied Sciences, mwaka 2019, hapa Dar es Salaam.

SWALI: Kwanini uliamua kusoma eneo la afya?

JIBU: Nilikuwa na rafiki yangu, Prisca, wote tulipata ‘division‘ ya tatu na yeye alikuwa amesomea PCB na mimi nilisoma CBG. Tukikaa dada yangu na yeye, akasema anakwenda kusomesha ‘Clinical Officer’, ikanishawishi.

Ingawa nilipenda kusomea ‘Nutrition’, ila yeye akaenda kusoma chuo kipo Iringa, mimi nikasalia hapa (Dar es Salaam) katika chuo nilichosoma. Nimesoma miaka mitatu, udaktari ngazi ya diploma.

SWALI: Unatarajia kuendelea na masomo hayo?

JIBU: Inshaalah! Natarajia kusoma zaidi miaka kama mitano hivi, ili niwe daktari kamili.

SWALI: Changamoto gani ambazo unapitia, hasa ukizingatia unameza dawa kila siku, jamii, watu wa karibu wanakuchukuliaje?

JIBU: Mara ya kwanza, kwa sababu nilijua naumwa…degedege, inapoanza kuja unahisi. Ukishakata mawasiliano ndio inakuwa hujui kinachoendelea. Ila mwanzo inapoanza, unajitahidi kuomba msaada…nisaidieeee nisaidieee…ila sauti haitoki.

Mpaka mwisho, unapoteza fahamu. Kwa hiyo kutumia dawa, nikawa sijali mtu, kwa sababu nilikuwa na bidii darasani, ila nilipoanza kuumwa nikawa nakaa nyumbani hata wiki tatu, hata mtihani wa ‘mock’ kidato cha sita sikufanya.

Nakumbuka nilienda hospitali, wakasema unameza vidonge vingapi? Nikasema vinne, wakaniongezea. Hivyo nikawa naumwa mwili unalegea. Nikaondoka Mwanza…dawa zilinifanya nilale sana hata darasani, nilikuwa naumwa sana kichwa. 

Kwa sababu ukitokewa na hali hiyo, ukishapata fahamu, kichwa kinauma sana. 

SWALI: Uliwahi kuambiwa sababu au chanzo ni nini?

JIBU: Dawa nameza, vipimo bado sijafanya…vipimo ni gharama, hadi uende ustawi ufanye utaratibu, upate kibali. Kwa kuwa nilikuwa nasoma sikupata muda wa kutosha kushughulikia kibali.

Dawa nanunua kwa fedha taslimu na kwa mwezi Sh. 10,000 inanitosha na hata mimi mwenyewe kwa fedha yangu nahakikisha sikosi ‘phenobarbital’ (dawa inayotumika kutibu au kuzuia kifafa) kwenye kabati.

SWALI: Ulitarajia kuwa nani tangu ukiwa mdogo?

JIBU: Mimi naitwa Daktari Isrey (kicheko)...ingawa nilipenda kuwa mwanamitindo, napenda sana na mtu akitokea akiwekeza kwangu, tutafanya kazi.

Kwa sasa natamani nipate kazi nzuri, ingawa pia napenda kujikita katika kutoa elimu, ushauri kuhusu kifafa. Kupaza sauti kwa kujiamini, natamani niwe daktari na nimiliki taasisi binafsi.

Kwenye akili yangu nawaza…nitengeneze kitu tofauti kwenye jamii, labda msichana mrembo mwenye ‘epilepsy’. Napenda kupambania kizazi changu, ili aliyeko kuanzia 2020 ajue nini cha kufanya, watoe zile dhana hasi kwenye akili zao.

SWALI: Kuna tahadhari zozote huwa unachukua kwenye maisha yako?

JIBU: Mimi ni mtu ambaye kwanza natembea na dawa zangu, pia mimi kifafa huwa kinanikuta usiku, usingizini. Nikiwa nimelala nashtuka, zinaanza ‘hallucination’. 

Zamani, lakini hata sasa, mkono wa kulia unaanza, hapo nitakimbilia kufuata vidonge ili nimeze. Nainuka, najua kabisa hapa naumwa, lazima nitafutie dawa. Nikimeza na ninakuwa kama natulia, ila bado nakutwa kama ‘mawenge’.

Tahadhari nyingine, ni kwamba mama yangu ananiambia nisiende kuogelea. Lakini, kama nipo na rafiki zangu wanataka tukaogelee, sikatai, naenda. Pia, kupika napika. Kwa ufupi, mimi mchana niko vizuri, ila kifafa kinanikuta usiku nikiwa nimelala.

Mimi nimesoma na wanafunzi ambao mwingine unakuta kaanguka. Mwanafunzi unajua ni mbishi utakuta ana dawa, hamezi!

SWALI: Je, huwa unatoa elimu kwa jamii, kuhusu hali yako?

JIBU: Ndio. Nimekuwa balozi. Ila changamoto utakuta mtu anakufuata anasema …’dada Isrey lini tutapona kabisa, tufanyaje ili tupone?’... Mimi nawaambia tu, tutumie dawa vizuri. Ukiona dawa haikusaidii vizuri, rudi hospitali. 

Napenda kusema, jamii iache unyanyapaa. Watu wanaachika kwenye ndoa, wanafukuzwa shule, au mtu anashindwa ‘ku-date’na mtu, eti kwa sababu ana kifafa. 

Kuna changamoto wazazi wanapitia, utakuta anaambiwa…’ Sasa wewe una nini mtoto wako mwenyewe ana kifafa…’

Mtaani unyanyapaa! Utakuta mtu anaanguka, watu wanashtuka, wanashangaa, wanaanza kupiga kelele, ukipata fahamu, unakuta watu wamejaa, wanahadithiana awali ilikuwaje unasikia yote.

Imewahi kunitokea mara mbili, mwenzangu akaenda kumuita mwenye nyumba. Nikashtuka watu wamenijalia. Kwenye kazi pia, huwezi kujitangaza una kifafa, huwezi kupata.

BINGWA AFYA YA AKILI

Mtaalamu Bingwa wa Afya na Magonjwa ya Akili kutoka MNH, Dk. Saidi Kuganda anasema wanaougua kifafa, rekodi ya muda wa kupoteza fahamu kwa wanaougua ugonjwa huo mara nyingi ni ule ule.

“Huishi kwa masharti fulani fulani, namna ya kulala, yaani ulale upande upi kitandani, hasa usiku, haulali tu ovyo, ulale ubavu, usilale kifudifudi wala chali.

“Ukiona ukilala ubavu ukajikuta umegeuka si kwa fahamu zako, basi weka utaratibu wa kuegesha mto upande mmoja, ili hata iweje ujikute upo upande uleule.” anasema bingwa huyo, ambaye ni Makamu Mwenyekiti cha Chama cha Wataalamu wa Afya ya Akili (MEHATA).

Anasema ugonjwa huo, sababu ya kwamba ni wa kurithi ni ndogo sana, chanzo kikuu ikiwa ajali. Maambukizi kwa watoto wakiwa na umri wa chini ya miaka mitano.

Sio ugonjwa wa kuambukiza, akishauri bingwa huyo na kufafanua kwamba, wagonjwa hao wakikumbwa na hali tofauti, wapewe msaada.