Hawa ndiyo waliosababisha vijana wa zamani kujiita'mabitozi', sasa'matozi,'

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 07:22 AM May 25 2024
Kundi machachari la muziki,  'The Beatles,' lililoanzishwa mwaka 1960 na kuvunjika mwaka 1970, ambalo lilitikisa dunia.
Picha: Mtandaoni
Kundi machachari la muziki, 'The Beatles,' lililoanzishwa mwaka 1960 na kuvunjika mwaka 1970, ambalo lilitikisa dunia.

SIKU hizi kijana akiwa anapenda kuvaa vizuri na mtanashati anaitwa au kujiita 'tozi.'

Vijana wa kisasa wanapenda kuitwa au kujiita 'matozi', ikiwa na maana kwanza ni kijana anayejipenda, mtanashati, anajua kuvaa na mara zote ni nadhifu na msafi, ambapo kwa jina lingine wanaitwa 'mabishoo.' Hata hivyo wenyewe huwa hawapendi kuitwa jina la 'bishoo', badala yake wanalipenda sana lile la 'tozi.'

Nini maana ya jina hilo na limetoka wapi? Nani aliyewapa jina hilo vijana watanashati?

Jina hilo ni mwendelezo wa jina la 'mabitozi', lenye maana ile ile ya mwanzo.

Vijana wa zamani, kuanzia miaka ya katikati ya 1960, hadi mwishoni mwa miaka ya 1990, wao walijiita au kuitwa, 'mabitozi.'

Sababu ya kuitwa au kujiita hivyo ni ile ile, kujipenda, kuvaa vizuri, utanashati, umaridadi, usafi na unadhifu.

Zamani miaka hiyo, ukionekana uko nadhifu, umevaa vizuri, watakuita 'bitozi.'

Hapa unapata picha kuwa kumbe maneno 'mabitozi' na 'matozi' yana maana moja, tofauti ni enzi tu, na staili ya mavazi tu. Vijana wa zamani wao walijiita 'mabitozi' na wa sasa, 'matozi.'

Hawa wa kisasa 'wameliediti', tu neno 'bitozi', wakaweka 'tozi.'

Sasa twende pamoja, hilo jina la 'bitozi', mpaka kuwa 'tozi' limetokana na nini, hapo vijana watanashati, wenye kujipenda wanalitumia?

Vizazi vyote hivi, vya zamani na sasa wanatumia neno hilo ambalo ni jina la bendi ya muziki ya vijana machachari wa zamani, waliounda kundi lao nchini Uingereza katika jiji la Liverpool, wakaliita, 'The Beatles.' Sasa nadhani umeanza kupata picha jina hilo limetoholewa kutoka wapi.

Waswahili wao wakaacha kulitaja kama 'bitozi', wakaita kama wanavyoita, na baadaye likabadilika na kuwa 'tozi' hadi hii leo.

The Beatles lilikuwa kundi la wanamuziki wanne, ambao ni John Lennon, Paul McCartney, George Harrison na Richard Starkey, maarufu kama Ringo Starr.

wakati huo walikuwa vijana wadogo, Waingereza waliojaliwa vipaji vya kuimba miaka hiyo, wakiwa na umri mdogo tu kuanzia miaka 18 mpaka 22, lakini walikuwa balaa.

Jamaa pamoja na kujaaliwa kuimba, walikuwa wasafi, wanajua kuvaa, kujipenda na kutokana na utanashati wao, ndiyo Wabongo walipoanza kujiita au kuitwa 'mabitozi' kwa wale vijana walionekana wanatashati, na hadi leo hii hawanaitwa 'matozi.'

Nadhani sasa vijana wa kizazi kipya ambao walikuwa hawaelewi neno 'tozi' limetoka wapi, sasa wameelewa.

Wao ndiyo waliolipaisha sana jiji la Liverpool na Uingereza kwa ujumla, muziki wao ulipata soko duniani na wao wenyewe kupendwa sana na kuwa ndiyo kioo cha vijana wengi duniani kutokana na utanashati wao.

Wanamuziki hawa walitikisa dunia, walipata pesa nyingi sana katika umri mdogo, walifanya chochote walichokitaka. Katika kila nyimbo 100 bora katika chati ya Billboard miaka hiyo, nyimbo kuanzia nyimbo tano au zaidi zilikuwa zao.

Chenye mwanzo hakikosi mwisho, kundi lilivunjika mwaka 1970, baada ya baadhi ya wanamuziki kujiengua na kuanza kupiga muziki kivyao, maarufu kama 'solo artist.'

Mpaka leo hii, ni wanamuziki wawili tu ambao wapo hao, nao ni McCartney mwenye umri wa miaka 81 sasa na Ringo Starr, ambaye ana miaka 83.

Lennon aliuawa New York nchini Marekani akiwa na miaka 40, Desemba 8 mwaka 1980, na Harrison, alifariki 2001, akiwa na umri wa miaka 58.

 

Tuma meseji 0716 350534