Kinanama wajasiriamali wa Fungu Refu walivyoshikilia soko, wateja wakuu DRC

By Rahma Suleiman , Nipashe
Published at 06:06 AM Apr 19 2024
Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi, Shaabani Ali Othman, akikagua Kiwanda cha Kusarifu Dagaa, kilichoko Unguja.
Picha: Maktaba
Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi, Shaabani Ali Othman, akikagua Kiwanda cha Kusarifu Dagaa, kilichoko Unguja.

LICHA ya Zanzibar kuwa na utajiri mkubwa wa uvuvi, inatajwa bahari yake inapotumiwa vizuri, kuna maendeleo makubwa yatapatikana, kwa kupitia fursa zilizomo baharini na Ukanda wa Pwani.

Uvuvi unatajwa kuwa muhimu kwa maendeleo ya jamii katika maeneo yanayopakana na maji. Pia, ili sekta hizo kuleta tija, inapaswa kutumia teknolojia za kisasa na ushirikishwaji sekta binafsi.

Ni sababu ambazo visiwa hivo sasa, vinasifika kwa biashara ya usafirishaji dagaa kavu, penye soko kubwa katika Jamhuri ya Kidemokrasia  ya Congo (DRC).

Kuna eneo tajwa la Fungu Refu, kisiwani Unguja maarufu kwa shughuli za uvuvi, ukaushaji na uanikaji dagaa, kabla ya kuingia sokoni kuuzwa.

Hapo kuna wafanyabiashara wengi watokao nchi jirani ya DRC, wakifuatilia soko la dagaa hao, Kaskazini mwa Unguja.

Eneo hilo limekusanya wajasiriamali zaidi ya 2000 wanaofanya biashara hiyo ya dagaa kutoka maeneo mbalimbali ya visiwa vya Unguja, Pemba na baadhi ya mikoa ya Tanzania Bara, ikiwamo Tanga, asilimia 80 ya wanaoshughulika ni kinamama.

MWENYEKITI GRACE

Grace Ngoti (39), ni miongoni mwa wajasiriamali hao anayesema eneo hilo ndilo tegemeo kwake na kinamama wenzake katika kukuza kipato chake na kuendeleza familia kupata mahitaji muhimu, ikiwamo chakula na kusomesha watoto wake.

Anasema, ni zaidi ya miaka 10 sasa anafanya biashara hiyo ya kuanika dagaa, akinunua kutoka kwa wavuvi, anapika na kulikausha kwa jua kabla ya kuwauza.

Grace, mama wa watoto watatu, yuko na kinamama wenzake wengi akiwaongoza katika nafasi yake ya Mwenyekiti wa Wajasiriamali Wanawake, katika eneo hilo.

Anasema, ili kukuza biashara yao hiyo ambayo ni tegemeo anashauri imefika wakati serikali ikawajengea uwezo, kwa kuwapatia mtaji na kuacha kutegemea matajiri wateja wa kigeni, ambao ‘huwalazia’' katika kununua dagaa.

Anasema mjasiriamali anapopata mtaji mzuri, anafanya biashara vizuri, ikiwamo kununua dagaa na kuwasafirisha nje ya nchi, kwa sababu soko la uhakika lipo.

WANAVYOLALIWA SOKONI

Mwenyekiti huyo anasimulia, wanachokifanya matajiri wao kutoka DRC huwapa fedha na kutafuta dagaa ambazo baadaye hutaka wauziwe kwa bei wanayoitaka wao, bila ya kujali gharama na muda alioupoteza mjasiriamali.

''Kwa sasa hatuna mtaji wa kutosha wa kufanya biashara hii na matokeo yake tunategemea matajiri kutoka Congo (DRC) ambao ndiyo wanaotupangia bei ya kununua dagaa,''anasema.

Mjasiriamali Fatma Haji Juma (41), anasema kilio chao kikubwa ni serikali kuwezesha ujenzi wa kiwanda cha kusarifu dagaa katika eneo hilo, ambacho kitaongeza thamani ya bidhaa hiyo kuwa na matumizi mengi zaidi.

Anasema ujenzi wa kiwanda, ndiyo mkombozi kwao na kitaleta mageuzi makubwa katika biashara yao na serikali ikipata kodi.

''Tunaamini biashara hii itakuwa mkombozi kwetu na kufika wakati wa kuacha kutegemea soko moja la Congo,''anasema.

Katibu wa Umoja wa Waanika Dagaa katika eneo hilo la Fungu Refu, Mkubwa Fundi Kombo, anasema serikali inawafahamu wafanyabiashara wa eneo hilo, kwa sababu kupitia mamlaka husika, hukusanya kodi kutoka kwao.

''Biashara ya kuanika dagaa katika eneo la Fungu Refu ni maarufu. Hivi sasa asilimia 80 inafanywa na wanawake ambao wameonyesha utayari katika kujikomboa, pamoja na kushiriki kikamilifu katika Uchumi wa Buluu,'' anasema.

Rai yake serikali anaitaka iwajengee kituo kidogo cha polisi, kwa sababu kuna mkusanyiko mkubwa wa watu, hivyo hata pakitokea uhalifu, inakuwa rahisi kuwafikia, badala ya kutegemea huduma ya mbali Mkokotoni.

WADAU WA KINAMAMA

Ofisa Mradi wa Wanawake na Uongozi katika Siasa na Uchumi, kutoka katika Chama cha Waandishi wa habari Wanawake Tanzania (TAMWA) – Zanzibar, Mariyam Ame Chum, anasema shughuli za kiuchumi zinazofanywa na wanawake wa Fungu Refu, zinahitaji kuungwa mkono, ili wanawake wafikie malengo ya kujitegemea kiuchumi.

Anaitaka Hamlashauri ya Mkoa husika, kupaimarisha Fungu Refu, ikiwamo ulinzi na usalama kwa wajasiriamali wanawake, hatua inayowaongezea ufanisi wa kufanyika kazi bila ya hofu.

''Mradi wa Wanawake na Uongozi katika Siasa na Uchumi (SWILL), ambao unafadhiliwa na serikali ya Norway, umefurahishwa na juhudi zinazochukuliwa na wajasiriamali waliopo Fungu Refu ambao kwa asilimia 80 ni wanawake,  wanavyojituma katika kujiimarisha kiuchumi na kujitegemea” anatamka Maryam.

KIWANDA CHAJA

Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi, inatarajia kuingiza mamilioni ya fedha, baada ya kukamilika ujenzi wa Kiwanda cha Kusarifu Dagaa kinachoendelea kujengwa katika wilaya ya Magharib A, Unguja.

Matarajio yaliyopo yanatajwa kuwa kiwanda hicho kuwa na uwezo wa kuzalisha tani 20 za dagaa kavu kwa siku, zenye thamani ya zaidi ya Sh. milioni 200.

Hadi sasa dagaa ni sehemu ya mazao makuu ya kimkakati visiwani humo, katika sekta ya uvuvi na mazao ya baharini, sasa mipango iliyoko ni kuliinua zao hilo kupitia ushindani wa kisiasa kwa ubora masokoni, ndani na nje ya nchi.

HALI YA UZALISHAJI

Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi (sasa yuko Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale), Aboud Suleiman Jumbe, anasema Zanzibar chini ya uongozi wa Rais Dk. Hussein Mwinyi, uzalishaji dagaa umeongezeka.

Jumbe anafafanua kuwa takwimu inabadilika, kwa nyongeza kutoka tani 2,405 zenye thamani ya shilingi bilioni 10.33 hadi tani 21,827 zenye thamani ya shilingi bilioni 89.31.

Anasema, pia usafirishaji wa dagaa umeongezeka kutoka tani 3,579 zenye thamani ya shilingi bilioni 12.31 mwaka 2020, hadi kufikia wastani wa tani 9000 zenye thamani ya milioni 35 kwa mwaka 2023.

Anataja mafanikio ya uzalishaji dagaa, yamewezesha kutanuka sekta ya uvuvi wa samaki kutoka tani 38,107 mwaka 2020 hadi tani 80,085 zenye thamani ya shilingi bilioni 569.08 kwa mwaka huu. Ni ongzeko la asilimia 210.

“Ongezeko hilo ni ushihidi mkubwa wa kihistoria na imewezesha wavuvi kupata ajira na kuinua hali zao za maisha. 

“Takwimu za hivi karibuni zinaonyesha kuendelea kukua kwa kasi kubwa kwa sekta ya uvuvi nchini kwa kiwango cha asilimia tisa kwa mwaka,” anasema Jumbe.

Pia, anafafanua mchango wa sekta ya uvuvi katika Uchumi wa Buluu umeongezeka kufika wastani asilima 17.40, matarajio ya kuwapo kiwanda cha kukausha dagaa, kitachochea ongezeko la mapato yao, kutoka shilingi  435,300 za sasa, hadi shilingi  742,500 kwa mwezi.

Sensa ya mwisho ya uvuvi mwaka 2020, inataja Zanzibar kuwa na wavuvi 88,000, huku asilimia sasa ikifafanuliwa kimaisha asilimia 21 ya Wazanzibari wanatumikia Uchumi wa Buluu. 

Mkurugenzi wa Kampuni ya Uvuvi Zanzibar (ZAFICO) Amiri Haidar Mshenga, anasema mradi huo wa kujenga miundombinu ya dagaa, ni miongoni mwa utekelezaji wa ahadi zake Rais Dk. Mwinyi, kwa wajasiriamali wanaosarifu dagaa.

Mshenga anasema, Zanzibar ina wastani wa wajasiriamali 16,000 wa dagaa, Unguja wakiwapo 14,000 na 12,000 Pemba.

Vilevile, kuna jumla maeneo matatu yametengwa kwa ajili ya mradi wa usarifu wa dagaa, ikiwamo Fungu Refu na Ndagoni.

Anasema, mradi huo unatarajiwa kujumuisha ujenzi wa viwanda viwili vya kusarifu dagaa, ujenzi wa majengo ya kuoshea dagaa, majengo ya kuchemshia dagaa, jengo la mtambo baridi kwa ajili ya kuhifadhia dagaa na mtambo wa kuzalisha barafu na jengo la biashara.

“Hadi kukamilika kwa kiwanda hiki, sisi ZAFICO tutaweka chanja 5000 za kuanikia dagaa na mradi huo kwa awamu ya kwanza utakamilika mwaka huu na unatarajiwa kuajiri wajasiriamali zaidi ya 10,000 wakiwamo wavuvi na wafanyakazi wa sekta ya dagaa,” anaeleza.

 HIFADHI MAZAO BAHARI 

Mkurugenzi wa Idara ya Uhifadhi wa Mazao ya Baharini, Dk.Makame Omar Makame, anasema mikopo tayari imeshatolewa kwa awamu mbili tofauti,  kwa sasa wanasubiri kadri fedha zitakazorejeshwa, ili kuwapatia wengine.

Anasema, Idara ya  Uvuvi na Mazao ya Baharini, miongoni mwa majukumu yake ni kuratibu wajasiriamali wanaofanya kazi za uzalishaji dagaa, wakiwamo wa Fungu Refu Mkoa wa Kaskazini Unguja, kuona namna wanavyofanya shughuli zao kwa mafanikio makubwa.

Anasema, Kiwanda cha Kusarifu Dagaa, kwa kiasi kikubwa kitawafanya wajasiriamali hao, kufanya shughuli zao kitaalamu zaidi kwa kutumia teknolojia ya kisasa, ikianzia wanavyowaanika dagaa.