Magonjwa sugu yanayotesa afya ya wazee katika maisha ya uzeeni

By Flora Wingia , Nipashe
Published at 11:44 AM Jun 13 2024
Mzee akipata tiba kliniki.
PICHA: MTANDAO
Mzee akipata tiba kliniki.

AFYA ya wazee na uzee, ni moja ya maeneo yanayotiliwa mkazo sehemu mbalimbali duniani, kutokana na kuwa na magonjwa sugu yanayosumbua kundi hilo maishani.

Mtaalamu na Mshauri wa Masuala ya Afya ya Jamii, Dk. Ali Mzige, anafafanua kwamba inakadiriwa watu milioni moja, wanavuka kuingia umri miaka 60, kila mwezi duniani. 

Anataja karne ya 20 inaingia na ongezeko la wazee katika nchi zinazoendelea na zilizoendelea. Inakadiriwa katika robo ya karne ya 21, idadi ya wazee duniani itakuwa na mitazamo kadhaa.

Inatajwa, miaka mitano baada ya 2020, Wajapani watakuwa na idadi kubwa ya wazee duniani, kwa asilimia 31 watakuwa na umri zaidi ya miaka 60, wakifuatiwa na Italia, Ugiriki na Uswisi.

 Kadhalika, inakadiriwa kuvuka miaka hiyo, nchi tano kati ya 10 zenye idadi kubwa ya wazee zitakuwa: China, India, Indonesia, Brazil na Pakistan.

Ikaelezwa kuwa ifikapo mwaka 2020, inakadiriwa idadi ya wazee katika nchi zinazoendelea, itaongezeka kwa kiwango asilimia 240, kutoka iliyokuwapo miaka ya 1980; sababu ni kupungua watoto wanaozaliwa na ongezeko la umri wa kuishi. 

Kitaalamu inafafanuliwa kusababisha na kuwapo teknolojia iliyoendelea, zikiwamo dawa za kutibu magonjwa mbalimbali. 

Wanawake kwa wastani wanatajwa wanaishi muda mrefu, kuliko wanaume takriban katika kila nchi. Idadi ni kubwa iko katika kundi la wazee na wajane, huku wazee hao ndio watoa huduma kwa wazee wenzao duniani.

HALI YA TANZANIA 

Tanzania inakadiriwa kuwa na wazee milioni 3.5 au zaidi, wenye umri kati ya miaka 60 na 65 na idadi yao inaongezeka kila mwaka.

Magonjwa sugu yanayowasibu wazee duniani kote ikiwamo Tanzania: Magonjwa ya moyo, ikiwamo shinikizo la juu la damu- presha pia saratani (kansa) za aina mbalimbali, kama mapafu, kibofu cha mkojo, tezi dume (prostate), pia shingo la mfuko wa kizazi kwa wanawake. 

Dk. Mzige anasisitiza kuwa ugonjwa wa kisukari kwa anayeugua ni wa maisha, pia presha, akifafanua nasaha yake vijana wasidanganywe na wale wanaojinadi kuyatibu. 

“Nimeujua ugonjwa wa kisukari na presha miaka 50 iliyopita nikiwa shule ya sekondari. Hadi leo, presha na kisukari kinadhibitiwa, ili mgonjwa asipate matatizo ya muda mrefu,” anafafanua Dk. Mzige.

Anasimulia karaha watu walizopata kwa kunywa kilichoitwa ‘Kikombe cha Babu’ kukabili magonwa yao.  

Pia, anataja magonjwa mengine yanayowatesa wazee ni ya viungo na nyonga (osteoarthrosis and hip joints), hasa wanapokuwa na uzito mkubwa zaidi ya kilo 70 kwa mwanaume na 60 kwa mwanamke. 

“Endapo katika ujana na usichana wako hukushiriki michezo, wala kupiga kwata, pia hukubahatika kwenda Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), ulikaa ukaponda raha, shida itakupata,” anasema. 

Dk. Mzige anasema, mtu anapofanya mazoezi ya viungo mwilini, asiache endelee na kama Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili (marehemu), Mzee Ali Hassan Mwinyi. 

“Huyu alikuwa kigezo changu cha ‘mzee na uzee’, lakini sio ugonjwa, bali maumbile. Magonjwa ya mapafu ikiwamo kifua kikuu na mengine yanasababishwa na uvutaji wa sigara. 

“Magonjwa ya akili hususan kupoteza kumbukumbu, upweke na wasiwasi wa ziada (anxiety), msongo wa mawazo (stress) na sonona, kiharusi (stroke), husababishwa na shinikizo la damu,” anasema.

Anasema, pia maradhi ya Ukimwi yanasababisha kiharusi, hasa kwa wasio na presha au kisukari, akiorodhesha pia, uvutaji sigara na unywaji pombe kupindukia, nazo ni wakala wanaowezesha kiharusi.

Dk. Mzige anatahadharisha kuwa mtu asipokunywa maji ya kutosha, akipoteza maji mengi ama kwa njia za jasho na mkojo, anaweza kupata maradhi kiharusi, akitoa elimu ya uwiano anapokufa Mwingereza mmoja kwa kiharusi London au kokote nchini kwao, Tanzania kunakuwapo vifo kama hivyo 10.

Mtaalamu huyo anafafanua, hiyo inatokana na imani anayoinukuu akimtaka: “Mwenye kiharusi karogwa au amechezewa mpelekeni kwa... (fundi-mganga wa jadi) ...” 

MAGONJWA MACHO

Eneo lingine analitaja ni magonjwa ya macho na hasa ‘mtoto wa jicho’ au trakoma, ambao unapokosa usahihi wake, unaweza kumpatia upofu wa macho. 

Vilevile, Dk. Mzige anataja shida ya presha ya macho (glaucoma) ambayo ikipanda sana, inahatarisha uono wa mtu, akinena ni tatizo la wazee wa jinsia zote kutokana na umri, wengine upungufu wa lishe zao.

“Kama hilo miwani ipo inasaidia kurekebisha, kushindwa kusikia vizuri, hatua inapofikia hapo ni kumuona Daktari wa Pua, Koo na Masikio, ili upime na ikibidi upatiwe kifaa kitakachokusaidia kusikia,” anasema Dk Mzige.

Anaitaja kadhia nyingine ya wazee na uzee wao, ni kupoteza meno kuwa kibogoyo, akitoa tahadhari hiyo ngumu iakuwapo kwa mgonjwa asiye na huduma za Bima ya Afya, kumhudumia.

Hapo mtaalamu huyo anatumia uzoefu wake, akishauri kuwa, ni vema wazee wasiokuwa na Bima ya Afya, wapewe mfumo wa tiba kwa kadi, au Mfuko wa Afya wa Jamii, utakuwa ukombozi wao wa kudumu.

Binafsi, anasema utumishi wa umma miaka 11 iliyopita na amekuwa akipewa somo la kufundisha afya za wazee wanapokaribia kustaafu, au kwa waliokwishastaafu. 

Mafunzo hayo, anasema anayatoa kwa watumishi wanaoanza ajira, ili wajiandae kuwa na afya nzuri, wakiwa kazini kabla hawajastaafu.

MAGONJWA AKILI

Magonjwa ya akili yamo katika kundi la magonjwa yasiyo ya kuambukiza. Hofu na wasiwasi, ni kitu cha kawaida katika maisha, lakini inatajwa inapozidi, huathiri maisha ya mhusika ya kila siku.

Kazi nyingi, zinatakwa kuleta matatizo ya malezi ya watoto na wajukuu au vilembwe, ndoa inayoyumba, kufukuzwa kazi, gari kuharibika, kukosa fedha za kulitengeneza.

Wahusika ni wengi, na wanaonekana kabla ya kustaafu au baada ya hapo, walikuwa wanahitaji huduma za tiba uzeeni (geriatric medicine) na kwa bahati mbaya wanazikosa. 

Hapo kunatajwa haja ya kuanzisha huduma aina hizo;  ushauri nasaha na maelekezo ya  cha kufanya, anapopata tatizo la magonjwa ya akili.

Ana ufafanuzi mwingine, baadhi ya wazee wanakosa mlo kamili, hali inayosababisha kuwa na lishe duni, huku kukiwapo asilimia 20 ya wagonjwa wa akili wanaolazwa wodini katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dar es Salaam,   wameathirika na ulevi wa pombe na dawa za kulevya kwa vijana wetu. 

Kwa ushauri zaidi wasiliana kupitia 

[email protected] au simu: 0713 410 531.