Misiba ya sasa, ukilinganisha na zama zile, imebadilika kupitiliza!

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 06:38 AM Apr 20 2024
Msiba.
Picha: Maktaba
Msiba.

MIENENDO ya watu siku hizi misibani imebadilika kabisa, siyo kama ilivyokuwa zamani.

Kuna tofauti kubwa utaikuta siku hizi katika misiba, kuanzia kwa wafiwa, majirani, ndugu, mpaka waombolezaji.

Sababu zipo, lakini inavyoonekana moja wapo ni athari za maendeleo ya teknolojia.

Kwanza, miaka ya nyuma eneo lenye msiba lilitisha watu wengi kiasi kwamba hata baadhi ya watoto waliogopa kupita. Wasichana ambao hawakuhusika kabisa, ambao huwa wanapita tu, walibadilisha kabisa njia.

Siku hizi kwenye msiba, watu wamekaa, lakini wanapita bila matatizo yoyote, tena kwa madaha.

Ilikuwa mama zetu wakisikia msiba, atatoka amefunga khanga, anafunga kilemba na kuvaa kandambili zake, kihuzunihuzuni!

Majirani wanapofika msibani kitu cha kwanza ni kumfariji mfiwa, kuchukua watoto wake wote wenye umri mdogo na kuwaondoa eneo la tukio, wakipelekwa nyumba jirani ambako watafanyiwa kila kitu, wataoga, watakula na kuambiwa wakae ndani na wenzao.

Majirani wa kike watakutana na kupanga nini cha kufanya, ambapo kila mmoja ataingilia huku na kuleta unga, mchele, sukari, kuku, bata, pamoja na kutafuta kuni za kupikia, ili kumpunguzia gharama mfiwa, ambaye wakati huo, akili yake haijakaa sawa kutokana na pigo la kufiwa.

Kikubwa zaidi ni kwamba muda wote watakuwa na mfiwa, wakihakikisha halii moja kwa moja, badala yake kumbembeleza kula chakula, na mahitaji mengine muhimu ili aendelee kuwa na nguvu.

Wanaume majirani nao wataitana kuhakikisha mwenzao anatatiwa kila aina ya msaada ya awali kabla ndugu na jamaa hawajafika, ikiwemo kupitisha michango, na mengine yanayofanana na hayo.

Kifupi ni kwamba zamani utawasikia waombolezaji muda wote waakimlilia marehemu, wakitoa michango mbalimbali. Wapo waliokuwa wakisaidia kazi muhimu msibani, wengine wanawatia moyo wafiwa.

Wapo wataohakikisha mali za mrehemu na vitu mbalimbali pale nyumbani haviibiwi kwa sababu wafiwa wanakuwa hawapo kwenye hali ya kawaida, nyuso za zao zilionekana kuwa na simanzi kiasi kwamba mtu unapopita huwezi hata kuuliza kama kuna msiba au la, pia watu wanaswali, wanasali na kuimba kwa hisia kali.

Kinyume chake, mienendo ya watu misibani siku hizi inahuzunisha kuliko hata msiba wenyewe.

Msiba ukitokea, utawasikia waombolezaji wakidodosa kinachoendelea au ratiba imekaaje, ili wahudhurie tendo la mwisho ambalo ni kuzika, watawanyike. Ni adimu siku hizi kusikia siku tatu za msiba baada ya kuzika.

Hapo msibani watu wanaendelea na maisha ya kawaida, wanaongea mpira, wanataniana, wanabishana, wengine wanachati na simu mwanzo, mwisho, hakuna tofauti na mtu anavyoshinda sebuleni kwake, kama vile hakuna chochote kilichotokea. Simu ziko bize kupiga picha na kuziposti kwenye akaunti zao.

Walio machachari, tayari wameshakuwa wenyeji kwenye 'pub', za jirani na hata kuzama kwenye maasi, baada ya kumalizika msiba unasikia mengi yatokanayo, kupitia umbea wa mtaani.

Wanaolala msibani hivi sasa ni wale wanandugu hasa, damu damu na marehemu, au ambao hawana pesa, lakini ndugu wengine visingizio vingi, ili mradi tu asishinde hapo.

Kipengele cha kulala msibani, ndiyo kimebadilika balaa. Huwezi amini, kwa sababu hizio hizo, kundi kubwa linajaa gesti za jirani, huku wengine usiku kucha kama hawako 'pub', basi kwenye mechi za Arsenal, na haishangazi simulizi za ndoa nyingi huanzia kwenye matukio hayo.

Huko uani, kinamama wanashindana nani kaja na dela la gharama, na simu ya bei mbaya, ndugu yangu kama umekuja na kitochi, utakoma.

Kuna wafanyaji tathmini, mara yupo jikoni, kisha kaenda sebuleni walipo wafiwa, akirudi huko, mjadala ulioshiba. Vile vile waliomo na wasiomo kwenye umbea, kila mtu kaweka antena, 'marehemu kafa kwa nini?' Atasemwa marehemu, mwenza wake, wanandugu wote, mpaka unajiuliza, wamekuja kulia, au wana jambo lao? Hapo nimemsahau mmoja, mtaalam kakusanya kundi hilo, yeye ndiyo anamjua marehemu ndani , nje, akimfafanua kama vile mwanahabari aliyekabidhiwa jukumu hilo, akaliambie umma.

Yaani, kila nililitafakari hili naishia kujiliwaza, makubwa haya, mbona madogo yana nafuu!

 Tuma meseji 0716 350534