Safari ya Korea na mauzauza yake -I

By Joseph kulangwa , Nipashe
Published at 04:39 PM Jun 21 2024
news
Mchoraji: Msamba
Mchoro wa katuni.

NI takriban saa 12 jioni ya Mei 31 mwaka huu, tunatua kwenye uwanja wa ndege wa kijeshi wa Korea Kusini jijini Seoul. Hizo ni saa sita mchana za Bongo. Hapo ni baada ya kuruka jana yake kutoka uwanja namba moja wa Julius Nyerere, Dar es Salaam.

Piga mahesabu tumekaa ndani ya lijidrimu hilo la Eitisi kwa muda gani. Mimi na baadhi ya walalahoi wenzangu ikiwa ni mara ya kwanza kupanda ndege tangu tuzaliwe.  

Najikaza huku mwenzangu jirani naona kama anamwomba Muumba wake asijeumaliza mwendo ghafla.Kabla hatujaruka Bongo, rubani anatwambia tutaruka juu kama meta 40,000 na ushei na umbali kutoka Dar mpaka Seoul ni zaidi ya kilometa 12,000.

Wakati tunatafakari na dege limesharuka umbali fulani hivi, mara kulakula inaanza! We acha tu ushamba mzigo! Nikitarajia jisahani la chipsi yai, kumbe…!

Tumeshiba, ghafla kila mmoja anakoroma akiwaza twendako ni wapi!  

Najaribu kufikiria ndege aliyotumia Mfalme Zumaridi kwenda mbinguni kukutana na Mungu na kushuhudia vighorofa virefu vya dhahabu! 

Naamini ilikuwa ni hii hii kwa uzuri wake! Kutoka mwendokasi mpaka ndege si mchezo eti!

Haya tukawa tumetua na kuchukuliwa hadi hotelini usiku. 

Nashangaashangaa tu sijawahi kulala ghorofani. Nayaona maghorofa ya Seoul kama yale yale yaliyosimuliwa na Mfalme Zumaridi, marefuuu.  

Nafikiria pengine nami huko ghorofani nitaonana na Mungu!Tunaambiwa kila mtu atalala chumba chake na anapaswa kukilipia! Wapi na wapi mgeni kulipia chumba cha kulala! Mimi naambiwa utalala chumba 

namba 902 huko juu, mwenzangu mwenye uzoefu na mambo haya ananiambia hapo ni ghorofa ya tisa na tunapanda kwa lifti! 

Mambo ya lifti tena! Ikanikumbusha dogo aliyefyatuka siku moja hapa Bongo akikimbilia kupanda lifti, ilipofunguka akaingia haraka kumbe haikuwapo, akaporomoka na kuvunja mguu. Hofu ikanijaa ghafla, lakini nikajikaza. 

Lakini tunaambiwa tena na wahusika; Wakorea wasiojua Kiswahili wala Kiingereza, wanatumia simu kujirekodi kwa Kikorea na simu inaandika Kiingereza, angalau tunaambulia mawasiliano.  

Anasema leo mtalipa Won 90,000, wengine Won 110,000. Mimi nikaangukia kwenye won 110,000. 

Ujue tu won moja ni sawa na takriban Sh. Mbili za madafu. Pia, tunaambiwa siku za wikiendi malipo yanabadilika kwani yanapanda na hakuna kulipa kwa dola ya Mmarekani, ambayo ndo tulikuwa nayo, lakini kama una kadi ya benki poa.  

Wenye vyumba vya Won 90,000 watalipa Won 130,000, sisi wengine Won 180,000. Kichwa kikanizunguka, nikifikiria nitabaki na nini katika matumizi wakati najua hapa napita tu nitarejea Bongo. 

Hapakuwa na jinsi, kila mtu akapanda lifti mpaka chumbani mwake, lakini udadisi ukatuonesha kuwa kumbe vyumba vya sakafuni hadi ghorofa ya pili havikuwa vinapangishwa wageni bali wenyeji waliokuwa wakifika jozi na kupumzika kwa muda na kuondoka, Bongo mnaitaje sijui!  

Wenzetu hao walikuwa wakipewa vifaa mbalimbali kama miswaki, dawa, mafuta ya kupaka, vichokonoa masikio na ‘zana’, lakini sisi wengine tukiambiwa tujiju kama hujaja na mswaki wako itakula kwako, utatumia vidole.  

Hakika siku ya kwanza yalinikuta hayo.

Asubuhi kuamka tunaambiwa hakuna stafutahi! Umewekewa birika, kahawa iliyochanganywa maziwa na sukari, maji, kahawa baridi ya kopo, chai baridi ya kopo na maji kwenye jokofu. Hivyo ni juu yako mwenyewe kujichemshia hakuna bufee!

Yaani nalipa maelfu na malaki hayo, lakini hakuna chai ya hoteli asubuhi, badala yake nafungua kinywa kwa kahawa na biskuti nne kweli? 

Wanasema ndiyo maisha ya Wakorea hayo, walishajizoelea, ukitaka chai na supu unaingia mtaani. Labda, ndiyo sababu vitambi ni vya kusaka na darubini.

Ufanyeje mlalahoi, wewe unajichemshia maji unachanganya na kilichopo, unafungua kinywa kabla ya kufuatwa na dereva aliyetwambia anaitwa Paul (Mkorea anaitwa Paul sawa na Makonda! Mh kasoma Cuba) asubuhi kuingia mzigoni, mzigo uliotupeleka Korea, kumsaidia Mama katika masuala ya kufungua na kutangaza nchi.

Usiku unawadia tunarudishwa kunako hoteli yetu na kuona kama tutakula nini! Unaambiwa kula ni juhudi zako mtaani. Tulikofikia hapa ni Gasandong, wilaya ya Geumcheon, kila mtaa una mgahawa wa chakula. Chakula kikuu hapa ni nyama ya kuku, kitimoto, samaki na wali au mbatata. 

Unachagua nini? Unafikiri nilichagua nini na walalahoi wenzangu? Wala sikutaka tena kula hotelini baada ya kutoka kwenye mgahawa huu tuliochagua siku ya kwanza kati ya tano tulizokaa Seoul. Bila shaka nitakwambia siku nyingine jinsi nilivyoipenda Korea Kusini na zaidi Seoul na hasa Gasan-Dong. We acha tu! Utanielewa tu wiki ijayo!