Simulizi ya mama aliyeuweza uongozi mtaani kwake, ukahalalisha mapinduzi uchumi kwao

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 04:48 PM Jun 21 2024
Leila Chamlumo.
Picha: Mpigapicha Wetu
Leila Chamlumo.

MWENYEKITI wa kijiji ni kuongozi muhimu sana katika nchi kwa sababu kiutawala anaingia kama mjumbe kwenye Kamati ya Maendeleo ya Kata (Ward Development Committee –WDC), ngazi ambayo ndipo vipaumbele vya bajeti ya halmashauri ya wilaya na vya taifa vinaanzia kupangwa.

 Lakini kwa sasa, idadi ya wanawake wenyeviti wa vijiji ni ndogo sana na hivyo kuashiria kwamba nchi yetu inaendelea kuwa maskini hasa vijijini kutokana kukosekana kwa juhudi za kuhakikisha wanawake wenye sifa za kutoa uongozi bora vijijini wanapata fursa hizo sawa na  wanaume.  

Kwa mfano, wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani yenye kata 25 na  vijiji  na  125  ni kijiji kimoja tu cha Mwanambaya kilichoko katika Kata ya Mipeko ndicho ambacho mwenyekiti wake ni mwanamke ambaye anaitwa  Leila Chamlumo. 

Lakini huyu mwanamke mwenyekiti wa kijiji cha Mwanambaya amekuwa  kiongozi wa kupigiwa mfano kwa utumishi uliotukuka kwa wananchi wa kijiji hicho na wilaya kwa ujumla.

 “Chamlumo ametoa uongozi ambao umeleta maendeleo ya wananchi katika nyanja mbali mbali kwenye kijiji chake maana anajituma sana ni mwadilifu”, anasema Prisca Ngwechemi, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Himiza Developemnt Organisation ambalo limefanya kazi za maendeleo ya wananchi wilayani Mkuranga kwa  miaka mitano sasa.

Katika mazungumzo na mwandishi wa makala hii, Chamlumo anataja baadhi ya mambo makubwa ya maendeleo ya wananchi ambayo ameyasimamia yakatekelezwa kwa ukamilifu na ufanisi kuwa ni nafasi yake kama mjumbe wa WDC  ni kusimamia mapato na matumizi ya halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga, kuhakikisha kwamba fedha za kodi ya wananchi zinatumika kikamilifu kuleta maendeleo ya wananchi.

Anatoa mfano, alipoingia kwenye uongozi katika  kijiji chake Mwanambaya zahanati ya kijiji hicho ilikuwa imechakaa kiasi kwamba paa lilikuwa linavuja akinena:‘’Mvua ikinyesha, daktari alilazimika kuondoka kwenye kiti chake na kwenda kujibanza eneo lingine.” 

Chamlumo anasema, aliamua kusimamia kikamilifu na kwa uaminifu mapato ya kijiji chake na kwa muda mfupi, kijiji kikafanikiwa kukusanya fedha shilingi milioni tano kwa ajili ya kukarabati zahanati hiyo. 

Pia, anasimulia kwamba alizungumza kampuni ya madini ya Songas, iliyochangia shilingi milioni 20 na  Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) ikatoa  shilingi milioni tatu kabla ya yeye mwenyewe  kupeleka ajenda hiyo kwenye kikao cha WDC, ambacho Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga nayo ilitoa bajeti ya  shilingi milioni tano, jumla ya  fedha hizo zikatumika  kukarabati zahanati na kujenga wodi ya wajawazito.

“Nilipoanza kazi, zahanati ya kijiji chetu chenye vitongoji saba ilikuwa na kitanda kimoja tu kwa ajili ya wajawazito, lakini leo tuna wodi ya wajawazito na vitanda vya kutosha,” anasema Chamlumo na kuongeza:

“Vilevile tayari tumeshajenga jengo la makazi ya daktari na manesi na wanakaa hapa hapa kijijini kwetu kuwahudumia  wagonjwa mchana na usiku”.

Kuhusu elimu, uongozi wa Chamlumo umeweza kukusanya fedha kutoka mapato ya kijiji na kwa sasa tofauti na miaka ya nyuma, kijiji cha Mwanambaya kilikuwa na shule moja tu ya Msingi Mwanambaya.

Anasema, kwa sasa wamejenga kwa fedha zao wenyewe zinazotokana na mapato ya kijiji  shule mbili zaidi za msingi ambazo zitaanza kuchukua wanafunzi wakati wowote kuanzia sasa na tayari wamekwishanunua madawati 200 kwa ajili ya shule hizo zilizojengwa katika vitongoji vya  Mizugu na Mivule 

“Hizi shule zitawapunguzia wanafunzi kutembea umbali mrefu kwenda shule na kurudi nyumbani kwao,” anasema Chamlumo na kwamba kijiji cha Mwanambaya kina vitongoji saba ambavyo ni  Kiloweko, Madodo, Mizungu, Mamangwa, Kibeneke, Mabatini na Mivule.

Aidha, Chamluno anasema kazi kubwa nyingine ambayo amehakikisha mapato ya fedha za kijiji kutokana na vyanzo mbali mbali zimewezesha ni pamoja na kujenga ofisi kila kitongoji katika vitongozi vyote saba  ili viongozi wa vitongoji hivyo waweze kufuatilia kwa karibu na kutatua matatizo ya wananchi na kuweka kumbukumbu za utendaji wao.

Anarejea alipochaguliwa mwenyekiti kwa mara ya kwanza mwaka 2006 akaunti ya kijiji ilikuwa na shilingi elfu 20 tu, lakini leo akaunti ya kijiji chake ina mamilioni kadhaa ya fedha. 

“Kwa kweli ninamshukuru Mungu maana ninaamini ni kwa sababu utendaji wangu ndiyo sababu wananchi wa kijiji chetu wameendelea kunichagua tangu mwaka kwa miaka 15 sasa.

“Ila ninataka niwaombe kuanzia sasa nisogee mbele kwenye uongozi wa juu zaidi kwenye Kata nishughulikie Kata nzima ipige hatua ya maendeleo kama hiki kijiji chetu,” anasema Chamlumo.

NCHI ILIKO, IENDAKO 

Hadi sasa, Chamlumo ni mmoja wa wanawake ambao wametoa mfano wa uongozi bora katika ngazi ya kijiji,   takwimu  zinaonyesha idadi  ya wanawake wenyeviti wa kijiji ni ndogo mno hapa nchini na kama juhudi  hazitafanywa na wadau mbalimbali.

Mfano unatolewa, serikali, vyama vya siasa, mashirika ya kiraia (NGOs) yanayotetea haki za wanawake, vyombo vya habari na wanahabari na taasisi za dini huenda  uchaguzi ujao  idadi ya wanawake wenyeviti wa serikali za vijiji iko ndogo inapaswa kuongezeka.

Swali kuu la kujiuliza ni: Je uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka huu 2024 utaongeza idadi ya wanawake wenyeviti wa  vijiji hasa kwa kuzingatia kwa viongozi hao ni rasilimali muhimu sana kwa maendeleo ya vijiji?

Takwimu zinaonyesha kwamba, katika ngazi ya kitongozi  ambayo ndiyo ya chini kabisa katika utawala wa nchi yetu idadi ya wanawake katika ngazi hiyo ni mdogo sana. 

Nchini sasa kuna jumla ya  vitongoji 62,612, ambavyo  kwa mujibu wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika mwaka 2019 ni wanawake 4,171 tu walishinda nafasi za uenyekiti wa vitongoji  sawa na asilimia 6.7.  

Kwa upande wa mijini, ingetarajiwa kwamba wananchi wanaweza kuwa na uelewa mkubwa zaidi wa masuala ya demokrasia na hivyo idadi ya wanawake wenyeviti wa  Serikali za mitaa, vijiji na vitongoji  uwe ni mkubwa, lakini hali halisi ya ushiriki wa wanawake kwenye uongozi wa utawala wa Mitaa mijini  bado ni duni sana. 

Takwimu zinaonyesha kwamba wakati uchaguzi wa Serikali za Mitaa, vijiji na vitongoji ulipofanyika mwaka 2019 nchi ilikuwa na mitaa 4,171 ambapo wanawake waliochaguliwa kuwa wenyeviti wa mitaa ni 528 tu nchi nzima sawa na asilimia 12.6%.

Hali ya uongozi wa wanawake bado hairidhishi vijijini. Nchi nzima ina vijiji 11,915 ambapo wenyeviti wa vijiji wanawake ni 246 tu sawa na asilimia mbili nukta moja (2.1%).  

Tafsiri ya idadi hii ndogo sana ya wanawake wenyeviti wa vitongozi, mitaa na vijiji  ni kwamba maendeleo kijamii, kisiasa na kiuchumi katika ngazi za chini wanakoishi wananchi wengi  bado ni changamoto kubwa sana hapa nchini na ndiyo sababu mamilioni ya wananchi wa taifa hili ni mafukara na wanaishi maisha yasiyo na furaha. 

Taarifa ya dunia kuhusu hali ya furaha kwa wananchi, Tanzania mwaka huu 2024  imeshika namba ya 131  wakati mwaka jana 2023 ilikuwa nchi ya  129. Hii inaashiria kwamba hali ya wananchi wa Tanzania kutokuwa na furaha mwaka 2024 imepungua ikilinganishwa na mwaka 2023

CHANZO CHA IDADI NDOGO

Mtaalam wa siasa na uongozi Dk. Victoria Lihiru, anataja tatizo mojawapo ni mfumo wa uchaguzi ambao umewapangia wanawake viti maalum, hivyo wanawake wenyewe na wanaume wa vyama vyote wamekuwa wakidhani nafasi za wanawake ni kwenye viti maalumu ni hali viti maalum lilikuwa ni suala la mpito. 

Jambo lingine linatajwa kutokuwapo kwa Tume Huru ya Uchaguzi, inayomuwezesha kila mtu mwenye sifa za uongozi, bila ya kujali ni mwanaume au ni mwanamke au chama chake kuweza  kugombea nafasi ya uongozi na kushinda au kushindwa kwa haki.

 ‘’Waziri wa TAMISEMI ambaye ni mwanasiasa na mwenye upande wa chama ndiye mwenye kauli ya mwisho kuhusu uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji, huyu hataweza kutenda haki kwa mgombea ambaye si wa chama chake”, anasema William Maduhu, Ofisa Uchechemuzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu.

Vilevile vyombo vya habari, madhehebu ya dini na  mashirika ya kijamii (NGOs), nazo zinatajkwa ni  taasisi zisizofanyajuhudi kubwa  kuelimisha na kuhamasisha jamii na wanawake wenye uwezo wa uongozi wajiunge kwenye vyama vya siasa na wagombee nafasi za uongozi katika Serikali  za mitaa, vijiji na vitongoji ili kuweza kutoa uongozi wa kubadilisha maisha duni ya wananchi.

Katika nini kifanyike, watalamu wanashauri serikali ihakikishe inapeleka bungeni haraka Muswada wa Sheria    itakayiowezesha uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji kusimamiwa na Tume Huru ya Uchaguzi  ili wagombea wa vyama vyote, wanawake na wanaume watendewe haki maana  kifungu cha 10 (1 c) cha Sheria ya Tume Huru ya Uchaguzi iliyopitishwa mwnzoni mwa mwaka huu  ndivyo inavyoelekeza.

Lingine linatajwa ni Wizara ya TAMISEMI itoe mapema iwezekanavyo Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji kwa mwaka uliopo, 2024 na kuhakikisha kanuni hizo vipengene vyake vinatangwazwa kwenye vyombo vingi vya habari  ili wananchi wafahamu kanuni hizo na wagombea waweze kujiandaa kikamilifu.

Vyama  vyote vya siasa viandae idadi  sawia ya wanawake na wanaume wenye sifa na  uwezo wa kuwa viongozi bora wa vijiji, mitaa na vitongoji  na kuhakikisha wanawake hao wanagombea nafasi hizo.

Mashirika yasiyo ya kiserikali, taasisi za dini na vyama vya siasa watumie mikutano na  vyombo vya habari  kuhamasisha wanawake na wanaume wa rika mbali mbali waadilifu na wenye sifa za uongozi  wajitokeze  kugombea nafasi  za uongozi wa vitongoji, mitaa na vijiji na kuwaelimisha kuhusu kanuni za uchaguzi huo kwa mwaka huu ili uchaguzi huo uipatie nchi yetu viongozi bora wanaume na wanawake katika nafasi hizo. Mungu ibariki Tanzania