Wakuu mtumie yatokanayo kambi mafuriko, staili ya MBWA kuwajibika

By Peter Orwa , Nipashe
Published at 06:13 AM Apr 19 2024
Katuni, ikionesha mfano wa watu wakimuokoa mwenzao kutoka kwenye maji ya mafuriko.
Mchoraji: Msamba
Katuni, ikionesha mfano wa watu wakimuokoa mwenzao kutoka kwenye maji ya mafuriko.

MARA zote katika taaluma na majukumu ya kikazi, inapotokea dharura ya ama mazuri au mabaya, mhusika mkuu huwa anakumbuka wajibu wake wa msingi.

Mwanafunzi, hali kadhalika mwalimu wake anaposikia msamiati ‘mtihani’ daima wanabadilika ghafla kujiweka tayari kukabili kijacho.

Kanuni zote za kitaaluma hurejeshwa haraka kumbukumbu mahsusi kwa somo tajwa na kujinoa kusikoisha huchukua nafasi yake. Maana hata Mjerumani Dikteta Addolf Hitler, aliyeaminika haogopi chochote duniani ikiwamo kifo, inadaiwa alipohojiwa akasema anachokiogopa maishani mwake ni mtihani pekee.

Dharura hiyo na mandalizi ya staili hiyo  ndio anayo hata mkulima, mfanyabiashara kwa soko  jipya au askari ambaye anarejea kuwa ‘soja’ akiweka silaha yake ‘haipoti’, inaanzia katika dharura ya usalama.

Baada ya hayo kupita, kitaaluma hufanyika majumuisho au tathmini za staili mbalimbali, lengo ni kujifunza kulikopatiwa na kulikosewa kwa ajili ya waendako.

Kwa wanahabari na wenzao wengi wanaangukia majukumu ya kitaaluma, huingia katika tahmmini ya kina pamoja baadaye kuumiza vichwa, inayoitwa ‘postmortem’, kama ilivyo kwa madaktari kutafakari kazi zao. 

Sasa ikiangaliwa kitaifa kuna dharura ya mfuriko tarkiban mikoa sita; kuanzia na Rufiji mkoani Pwani, Kilombero (Morogoro),  Geita, Arusha, Mbeya ma Mwanza mvua imezalisha mafuriko makubwa, hali kama hiyo ikitokea hata nje ya mipaka kama kwa majirani Beira Msumbiji na huko Uarabuni.

Mara moja, uongozi wa juu wa nchi umeagiza wakuu wa kiserikali, wakiongozwa na mawaziri kupiga kambi kuwajibikia kusaidia waathirika.

Ni sentesi kubwa na nzito sana, kutoka kwa mkuu wa nchi. Mosi, ni ishara ya walioko juu wanawawajibikiaje walio chini.

Lakini, kuna la pili hapo kupitia ‘postmortem’ zao wakubwa hao, hawatakiwi kuwasahau waathirika baada ya kuwawajibikia misaada hiyo katika kipindi cha dharura kilichoko.

Bado tunakumbuka marais Dk. Samia Suluhu Hassan, mtangulizi wake hayati Dk. John Magufuli na watangulizi wao, wamekuwa wakisisitiza wajibu viongozi kwenda waliko wananchi kutambua shida zao na kuzifanyia kazi wakiziona.

Ni hivi karibuni, Rais Dk. Samia akawakumbusha mawaziri, huku akitoa mfano wa anayetumia staili hiyo na kumpa kongole, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jerry Slaa, anavyowezesha kumaliza kero za ardhi papo kwa hapo, kupitia ziara hizo.

Sasa mtambue mawaziri, hilo la kuweka kambi linapswa kuwa staili ya kudumu katika kufanikisha kilichomo kwenye hadidu za rejea za majukumu yenu.

Ile timu inayoweka kambi naamini mtakuwa na safari za kutosha kuifuatilia huko kote penye majanga, maana hata msimamizi mkuu wa serikali, Waziri Mkuu wiki hii tukamshuhudia analitenda hilo akiwa angani anakagua  kwa helikopta kinachojiri katika mafuriko ya Morogoro.

Utendaji huo ni tiba, unaopotekelezwa kwa usafaha na wasimamizi wakuu wa ngazi mbalimbali, kama vile wakuu wa mikoa na wilaya una maana kubwa.

Ni uwajibikaji wa majukumu, pia kwa umma ambao ndio mabosi wenu wakuu, ikiwa sehemu ya staili ya menejimenti na utawala, ambao watafiti tangu zama hizo walikuna vichwa na kuja na nadharia inayohubiri hilo.

Wenyewe wanaiita nadharia ya MBWA, kwa maana yake kizungu ‘Management By Walking Around’ akimaanisha staili ya menjimenti, mkuu akifanya usimamizi kujua kinachoendelea katika picha halisi huko huko kunakohusika.

Ni wiki iliyopita katika kumbukumbu ya kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Moringe Sokoine, mengi yalisimuliwa kifo chake kilitokea akiwa safarini kutoka Dodoma Kwenda Dar es Salaam, akitumia fursa hiyo kukagua hali halisi ya mandeleo ya kilimo, badala ya kutumia ndege. Kimsingi, akiwa kiongozi alikuwa anatekeleza nadharia ya MBWA katika majukumu yake.

·             Mwandishi wa safu hii wiki hii amekosekana kwa sababu zisizozuilika. Mhariri.