Yanga ilivyolinda rekodi CAF, ya Simba ikivunjwa

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 10:57 AM Apr 01 2024
news
Picha: Mpigapicha Wetu.
Straika wa Yanga, Clement Mzize, akiwa ameruka juu kupiga mpira kichwa, akisababisha hatari kwenye lango la Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, akichungwa na beki Mosa Lebusa katika mechi ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

MECHI za kwanza za robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika zilimalizika kwa wawakilishi wa Tanzania, Simba kuchapwa bao 1-0 Ijumaa iliyopita katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, dhidi ya Al Ahly ya Misri, na Jumamosi Yanga kutoka suluhu dhidi ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.

Majaliwa ya timu za Tanzania yapo kwenye mechi za marudiano zitakazochezwa Ijumaa wiki hii, Simba itakapokuwa nchini Misri na Yanga nchini Afrika Kusini ili kujua kama zote mbili au walau moja inaweza kutinga hatua ya nusu fainali.

Kipigo cha bao 1-0 ilichokipata Simba kimehitimisha rekodi nzuri ya timu hiyo kila inapocheza na Al Ahly hapa nchini.

Kwa mara ya kwanza Al Ahly imepata ushindi dhidi ya Simba nchini tangu timu hizo zilipoanza kukutana mara ya kwanza mwaka 1985.

Al Ahly imefanikiwa kuifunga Simba baada ya kucheza mechi nne bila mafanikio kwenye michuano mbalimbali ya kimafataifa hapa nchini.

Simba imeshinda mara tatu na sare moja, kabla ya kupoteza mechi ya Ijumaa, ikiwa ni mchezo wa tano timu hizo kukutana jijini Dar es Salaam.

Kwa upande wa Yanga imefanikiwa kulinda rekodi yake ya mwaka 2001 ya kutoka sare dhidi ya Mamelodi Sundowns. Hii ni mara ya pili timu hizo kukutana nchini na mara zote Yanga imepambana kuhakikisha haipoteza nyumbani.

Katika makala haya tumekusanya rekodi zote za timu hizo zilipochezwa nchini, Simba dhidi ya Al Ahly na Yanga dhidi ya Mamelodi Sundowns na matokeo yake hadi mechi za wiki hii, twende sasa...

 Simba 2-1 Al Ahly (1985)

Mara ya kwanza Simba ilianza kucheza na Al Ahly, Agosti 22, 1985 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, ikiwa ni michuano ya Kombe la Washindi Barani Afrika, sasa Shirikisho, ikishinda mabao 2-1 yaliyofungwa na Zamoyoni Mogella na Mtemi Ramadhani, huku bao la kufutia machozi la Al Ahly likifungwa na Mohamed Ae Khatib 'Bibo' ambaye kwa sasa ndiye rais wa klabu hiyo.

 Simba 1-0 Al Ahly (2019)

Ilikuwa ni Februari 12, 2019 mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi iliposhinda bao 1-0, Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Baada ya kupigwa mabao 5-0, Februari 2 nchini Misri, Simba ilirejea nyumbani na kulipa kisasi hicho kwa bao lililowekwa wavuni na straika, Meddie Kagere. Simba na Al Ahly zote zilisonga mbele kwenye kundi hili.

 Simba 1-0 Al Ahly (2021)

Timu hizo zilipangwa tena kwenye makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, 2021, na mechi ya kwanza ilicheza nchini kama kawaida, Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, Februari 23, Simba ikashinda nyumbani kwa mara ya tatu bao 1-0, likiwekwa wavuni na Luis Miquissone, na ndiyo msimu ambao iliongoza kundi, Al Ahly ikashika nafasi ya pili.

 Simba 2-2 Al Ahly (2023)

Kwa mara ya kwanza, Simba ililazimishwa sare nyumbani dhidi ya Al Ahly katika michuano ya African Football League, mechi hii ilichezwa Oktoba 20, mwaka jana, katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, timu hizo zikimaliza dakika 90 kwa sare ya mabao 2-2. Mabao ya Simba yakifungwa na Kibu Denis na Sadio Kanoute, huku ya Al Ahly yakiwekwa wavuni na Reda Slim na Mahmoud Karhaba.

 Simba 0-1 Al Ahly (2024)

Ijumaa iliyopita, rekodi ya Simba ya kutopoteza mechi yoyote dhidi ya Al Ahly ikicheza nyumbani ilivunjwa, ilipochapwa mabao 1-0 katika mchezo ya robo fainali Ligi ya Mabingwa, Uwanja wa Banjamin Mkapa, kwa bao lililowekwa wavuni na Ahmed Nabil Koka dakika ya nne ya mchezo.

 Yanga 3-3 Mamelodi Sundowns (2001)

Ilikuwa ni raundi ya pili ya hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Yanga na Mamelodi Sundowns.

Baada ya kufungwa mabao 3-2, Mei 13 nchini Afrika Kusini, zilirudiana Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza Mei 27, 2001 na timu hizo kufungana mabao 3-3.

Kwa bahati mbaya sana, Yanga ikawa imetolewa kwenye michuano hiyo, Mamelodi ikisonga mbele mpaka hatua ya fainali ilipofungwa na Al Ahly ya Misri, kwa sare ya nyumbani Sauzi na kwenda kufa mabao 3-0 nchini Misri.

 Yanga 0-0 Mamelodi Sundowns (2024)

Jumamosi iliyopita Yanga ililinda rekodi yake ya kutopoteza mechi nyumbani dhidi ya Mamelodi Sundowns, zilipokutana kwa mara ya pili baada ya miaka 23, na kulazimisha suluhu, katika mechi ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.