Chombo kudhibiti huduma za afya ni muhimu

Nipashe
Published at 02:09 PM May 15 2024
Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu.
Picha: Maktaba
Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu.

WAKATI Waziri wa Afya akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya bajeti ya wizara yake bungeni, alisema serikali inakusudia kuja na chombo muhimu kitakachokuwa kinadhibiti ukuaji holela wa gharama za afya kwa wananchi.

Afya ni muhimu sana katika maisha ya binadamu hivyo ni lazima suala la gharama liangaliwe ili lisiwaumize wananchi.

Chombo hicho tumeelezwa kuwa kitakuwa kinafanyakazi ya kusimamia kama ilivyo kwenye gharama za ulipaji maji, umeme na mafuta.

Na kwamba lengo ni kudhibiti ukuaji holela wa gharama za afya kwa wananchi hususan wasio na bima ya afya.

Utaratibu huu utasaidia kudhibiti ule utozaji wa gharama holela unaofanywa na baadhi ya madaktari katika hospitali za binafsi na zile za serikali ili kuwapa unafuu wananchi.

Vyombo kama hivi vimefanikiwa pia katika huduma za mafuta ya petroli ambapo inafahamika kila mtu anapokwenda kwenye kituo cha mafuta kujaza kwenye gari yake anakuta bei elekezi.

Kumekuwa na malalamiko kutoka kwa baadhi ya wagonjwa wanapokwenda kutibiwa kukuta wakitozwa gharama kubwa kumuona daktari kabla ya kupata matibabu, hali inayowafanya wasiokuwa na bima za afya kushindwa kulipia na kuamua kwenda kujaribu tiba zingine mbadala.

Kwa mujibu wa wasilisho la makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti ya Wizara ya Fedha, kwenye vitita vya NHIF, madaktari bingwa katika ngazi ya rufani mkoa, ada imeongezeka kutoka Sh. 15,000 hadi 25,000 ambayo ni sawa na kumuona daktari aliyepo ngazi ya kanda na taifa.

Kiwango hichi cha kumuona daktari kinatoa hamasa kwa madaktari hao kufanyakazi katika mazingira yoyote watakayopangiwa, ikiwamo pembezoni.

Aidha, ada ya usajili na kumuona daktari kwa wanufaika wa NHIF kwa ngazi ya wilaya imeongezeka kutoka Sh. 2,000 hadi Sh. 7,000 kwa ngazi ya zahanati ada imeongezeka kutoka Sh. 1,000 mpaka Sh. 3,000.

Aidha, kitita hicho kitaboresha upatikanaji wa huduma bora za kibingwa na ubingwa bobezi karibu na wanachama.

Aidha, kitita hicho kimezingatia maendeleo ya teknolojia ya tiba, hali halisi ya bei katika soko na uwezo wa mfuko kugharamia huduma hizo huku ukiendelea kuwa endelevu kwa kuzingatia ushauri wa taifa, mapendekezo ya tathmini ya uhai na uendelevu.

Wizara ya Afya pia imetaja vipaumbele na kuimarisha huduma za kinga dhidi ya magonjwa na kuimarisha upatikanaji na ubora wa huduma za afya zinazotolewa na vituo vya kutolea huduma za afya kuanzia ngazi ya zahanati hadi taifa.

Katika bajeti hiyo wizara imetenga Sh. bilioni 117.61 kuimarisha huduma ya kinga dhidi ya magonjwa ikiwamo kuimarisha utekelezaji wa afua za chanjo kwa kuwafikia watoto 3,117,564 wenye umri chini ya miaka miwili, wasichana 871,429 wenye umri wa miaka tisa na wajawazito 3,298.437.

Kwa mujibu wa waziri, Sh. bilioni 17.18 zimetengwa kuimarisha huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto, ikiwamo kujenga, kukarabati na ununuzi wa vifaa tiba vya wodi 100 maalum za watoto wachanga wagonjwa waliozaliwa na uzito upungufu.