Usimamizi makini unatakiwa utoaji mikopo ya halmashauri

Nipashe
Published at 04:02 PM Apr 17 2024
Mikopo ya halmashauri.
PICHA: NIPASHE
Mikopo ya halmashauri.

SERIKALI jana ilitangaza kuanza utoaji wa mikopo ya asilimia 10 kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kuanzia Julai, mwaka huu, kwa kutumia utaratibu mpya wa kupitia benki. Katika kuanza utaratibu huo mpya wa mikopo, mamlaka 10 za serikali za mitaa zitaanza kama maeneo ya majaribio.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya ofisi hiyo kwa mwaka wa fedha 2024/25 bungeni jana, alisema mfumo huo wa utoaji mikopo umeboreshwa baada ya kubaini upungufu katika mikopo ya awali. 

Mchengerwa alizitaja halmashauri zilizoteuliwa kuanzia utoaji mikopo hiyo kwa majaribio ni majiji ya Dar es Salaam na Dodoma, manispaa za Kigoma Ujiji na Songea, halmashauri za miji za Newala na Mbulu na wilaya za Siha, Nkasi, Itilima na Bumbuli. Kuhusu halmashauri 174 zilizobaki.

Ni dhahiri kwamba uteuzi wa halmashauri hizo umezingatia tofauti za kimifumo katika uendeshaji na jiografia ya mahali zilipo. 

Sambamba na utaratibu wa utoaji mikopo kupitia benki, Waziri Mchengerwa alisema maboresho yanatarajiwa kufanyika ikiwamo uanzishwaji wa kitengo cha usimamizi wa mikopo hiyo katika OR–TAMISEMI na uanzishwaji wa kamati za usimamizi katika  ofisi za wakuu wa mikoa, halmashauri na kata. 

Katika ngazi ya kata, alisema kamati zitakuwa na majukumu ya kutambua waombaji na kuthibitisha vikundi vya mikopo na kuvisajili kwenye mfumo kabla ya kuwasilisha kwenye kamati ya halmashauri.

Kazi zingine zilizofanyika katika uboreshaji wa mfumo mpya ni pamoja na kusanifu na kujenga mfumo mpya unaoitwa ‘Wezesha Portal’ utakaotumika kwa ajili ya taratibu za ukopeshwaji wa makundi husika. Hatua hiyo pia itaondoa changamoto za mfumo zilizokuwapo awali kabla ya mikopo kusimamishwa.

Jambo lingine linaloonyesha kwamba mfumo huo mpya umeandaliwa vyema ili kuondoa kasoro zilizokuwapo awali ni kuwapo kwa mpango wa kuwajengea uwezo wasimamizi wa mikopo kwa kuwapa mafunzo na pia kuongeza idadi ya wasimamizi wa mikopo kwenye ngazi ya kata kwa kuajiri maofisa maendeleo ya jamii 787 na kupangiwa kata zilizokuwa na upungufu.

Katika kuhakikisha kunakuwa na ufanisi, serikali imepanga kurekebisha sheria inayosimamia mikopo hiyo na kanuni zake na baada ya kipindi cha mpito, tathmini itafanyika ili kubaini mfumo bora utakaotumika katika utoaji wa mikopo hiyo.

Hatua ya kurejeshwa kwa mikopo hiyo inatokana na serikali kutambua umuhimu wake katika kuyakwamua makundi maalumu kutoka katika utegemezi na umaskini ili kuwa na uchumi na maisha bora. Kutokana na umuhimu huo, Sh. bilioni 227.96 zikiwamo Sh. bilioni 63.67 ambazo ni za marejesho ya fedha zilizokuwa zikiendelea kukusanywa kutokana na mikopo iliyotolewa kabla ya kusimamishwa.

Ni dhahiri kwamba mikopo hiyo kama itatumika ipasavyo italeta matokeo chanya kwa makundi hayo, kwanza kwa kujiajiri na kushiriki katika shughuli za uzalishaji mali na pili, ni kujikwamua kutoka katika lindi la umaskini. Kwa kutambua hilo, ndiyo maana serikali  imeamua kurejesha kwa mfumo mpya ukiwamo usimamizi thabiti. 

Hata hivyo, kwa kipindi kirefu kumekuwa na taarifa za Mdhibiti na Mkaguzo Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuhusu kutafunwa kwa mabilioni yas fedha katika serikali kuu na  taasisi zake, mamlaka za serikali za mitaa zikiwamo. 

Kutokana na hali hiyo, ni vyema udhibiti na umakini katika usimamizi wa mikopo hiyo vikafanyika ili kuziba matundu ya upotevu wa mamilioni. Hata mikoa iliyositishwa kulikuwa na ubadhirifu na udanganyifu mwingi kutokana na baadhi ya viongozi kujinufaisha kwa kutumia vikundi hewa. 

Kwa  mfumo mpya, ni imani kwamba serikali imejifunza kutokana na makosa yaliyopita ndiyo maana imeandaa mikakati kabambe katika kuziba mianya kwa kuweka mifumo na kamati za utambuzi hadi ngazi ya kata.