JAMII ilikofika sasa, inapaswa kutambua kuwa mwanamke ana mhimili mkubwa unaowezesha gurudumu la maisha.
Wanawake wanapoamua pamoja, daima wanaweza. Hivyo, kinamama wanapaswa kuongoza watoto wa kike wenzao, waweze kutambua nafasi yao na kujua kilicho sahihi na kinachofaa katika maisha na kipi hakistahili kuwa nacho.
Hivyo, wanaweza kufahamu mambo mbalimbali, ikiwamo anayopitia mwanamke katika umma unaomzunguka, hivyo watu wote kwa ujumla wanapaswa wakumbuke nafasi ya mwanamke ilivyo katika jamii.
Ndani ya jamii za Kiafrika, zimekuwa na mtazamo tofauti kwa kinamama, kwa wanachokiamini kuwa mwanamke ni mfanyakazi za nyumbani na hana kitu kingine cha kufanya.
Hiyo, inawafanya baadhi ya kinababa wengi kutumia fursa hiyo kuwatumikisha wanawake bila ya huruma. Wanawake hawaruhusiwi kuwa na kauli sehemu yoyote.
Mwanamke anashinda nyumbani, akitekeleza majukumu yote na katika baadhi ya maeneo vijijini tunasikia huko, Tarime na Songea na vingine vingi hivyo wanaume walio wengi wana watumikisha wake zao bila kujali kama wamechoka au vinginevyo.
Majukumu yaliyozoeleka, yanajumuisha kukata kuni za mapishi, kuchota maji, hata wanaume ninawasihi peaneni elimu katika kuamini mwanamke, ana haki kwani hata yeye anachoka hivyo anatakiwa kupumzika.
Hata hivyo, bado watu walio wengi nadhani elimu hiyo haijazama kwao kisawasawa, kuna baadhi ya makabila yanayopenda kurithi wanawake, mila mbaya na iliyopitwa na wakati.
Ni jambo baya na si sahihi kumrithi mwanamke, kwani ni unyanyasaji uliopitiliza na ni makosa makubwa kisheria.
Ni dhahiri katika hilo, anayehusika na tendo hilo anabaki kuwa mgandamizaji wa haki na uhuru wa kijinsia kwa mwanamke husika, jambo ambalo sio la kiungwana na linakemewa vikali
Hivyo, mwanaume anayefanya jambo hilo la kumrithi mjane, anapaswa kuchukua hatua, kwani sio vyema. Naye, mwanamke anayo nafasi kubwa katika jamii kwani, kinamama tunao uhuru wa kushiriki kwenye kampeni ikiwa tunaelekea mwaka wa uchaguzi huu 2024 na wa uchaguzi mkuu 2025.
Inatupasa na kukumbuka kwamba, tuna nafasi ya kuwa wazalendo katika kushiriki kwenye uchaguzi kikamilifu, kukiwapo maono ya kuwania cheo. Kwa chochote kile, ni vyema mtu akajitambua anakoelekea.
Wewe mama nakushauri, chukua fomu za kuwania nafasi bila ya kuchelewa, hali itakayosaidia ushindani wa hali ya juu na kuwafanya wanawake kung’ara juu wakishika nyazifa za kuamua katika madaraka ya nchi.
Hivyo, nawasihi wenzangu, msiache kuwa na malengo ya kutimiza ndoto zenu, kwani kuna baadhi ya wazazi hasa vijijini, wamekuwa na mtazamo tofauti katika malezi ya watoto wengi wao, wakiamini kuwa mtoto wa kike hawezi jambo lolote la kufanya. Jambo hilo si la kweli hata kidogo tena!
Kuna falsafa kwamba, mwanaume ndiye mwenye haki ya kurithi na mengine mengi ya aina hiyo, jambo ambalo sio la kweli.
Mimi naamini uhalisia, binti ana nafasi kubwa kuikomboa jamii hiyo inayomhusu. Mama huwa ana uthubutu, pale jamii ikimpa haki na uthubutu wa kujikomboa kuanzia na elimu.
Ni chanzo cha maendeleo na inatupasa kukumbuka kuna vyombo vinavyotetea haki za wanawake.
Wanawake wana fursa mbalimbali za maendeleo, kwani hata Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA), kimeonyesha mfano kwa kutambulisha mradi mpya wanawake mnamo Oktoba, 2020.
Inatambua kuwa ushiriki wa wanawake katika nafasi za maamuzi, hasa ya kisiasa, bado ni mdogo, hivyo ina azma ya kuwakwamua kushiriki kuwania nafasi mbalimbali za uongozi.
Bila shaka, hata watoto wa kike walioko shuleni wasome kwa bidii, kwani wanayo nafasi ya kuongoza inahitaji elimu, hata kuwawezesha kuvuka katika malengo yao.
Niseme, bila ya kusahau napo wapo kinababa wanapaswa kupeana elimu ya utambuzi wa nafasi ya mtoto wa kike na kina mama kwa ujumla, taifa letu lizidi kuwa imara zaidi.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED