SUMU na taka za sumu zinazotoka kwenye injini si salama, zina karbon au hewa ukaa inayoweza kukuua, kuchafua hewa na chakula au bidhaa.
Ndiyo maana wataalamu wa afya wanasema kufanya kazi, kula vyakula vilivyochafuliwa au kukaa karibu na moshi ambao una gesi hizo kwa kiasi kikubwa ni hatari kwa yeyote.
Ikumbukwe kemikali na hewa hii hutoka wakati injini zinazotumia petroli au dizeli zinapopumua na moshi huo kusambaa angani na pembeni.
Huwafikia walioko pembeni mwa barabara na kusababisha kupata madhara yanayojificha lakini yanayoweza kuibuka baada ya miaka kadhaa.
Baada ya miaka mingi au muda mrefu magonjwa yanayotokana na hewa chafu huanza kuonekana, kuanzia machoni, kifuani, kwenye ngozi na kooni kote yakisababisha athari.
Kwa kawaida moshi huo huumiza macho, pua na koo na harufu yake inaweza kusababisha kichefuchefu lakini wengi huchukulia kuwa ni kitu cha muda mfupi.
Uchunguzi wa kiafya unaonyesha kwamba baadhi ya watu waliovuta moshi mzito wana matatizo kwenye mapafu yanayosababisha kupumua kwa shida, mafua, kukohoa mara kwa mara na kuwa na mzio au aleji.
Kuzoea kuvuta moshi huu kunaweza kusababisha athari za haraka kama kuwashwa machoni, puani na koo kukereketwa na hata mafua.
Inaelezwa na wataalamu kuwa moshi wa injini za magari, pamoja na bajaji na pikipiki unaweza kuleta madhara makubwa kama kwa afya watu na mimea hasa iliyo kando ya barabara.
Lakini, inavyoelekea wengi hawalielewi tatizo hilo na wala hawachukui tahadhari, mfano wafanyabiashara za vyakula karibu na barabara wana hatarisha maisha yao na wateja wao pia.
Kwa mfano, wale wanaouza vyakula mfano pweza, kachori, mishkaki, chipsi na vitafunwa kwenye stendi za mabasi mijini au kwenye barabara vinachafuliwa na vumbi pamoja na moshi wa vyombo vya moto.
Ni vyema wajue kuwa hula na kuishi kwenye kemikali za simu inayotoka kwenye injini.
Wanaokula na wanaotayarisha huweza kuugua magonjwa kama kuharisha, kutapika, kuhara damu, tumbo kujaa gesi, kupata kichefuchefu na kukosa hamu ya kula.
Ni vyema kukawa na udhibiti wa biashara ikiwamo kuuza vyakula karibu na barabara au vituo vya mabasi ambako magari hupumua. Aidha hata kukataza kupanda mboga barabarani ambazo huchafuliwa na moshi wa injini.
Wafanyabiashara wa vyakula, matunda, wakulima wa mboga na matunda pembeni ya barabara na wauza mboga hizo pembezoni wajiepusha na hatari hizo za kiafya.
Jamii nayo inahitaji elimu na kupewa ufahamu kuhusu madhara ya kula vyakula vilivyochafuka na sumu hasa za kemikali za moshi wa injini ili kujiepusha na magonjwa.
Bila shaka wafanyabiashara, wakulima kila mmoja kwa pomoja wanatakiwa kuwa na tahadhari kwani magonjwa ni sababu ya kuyumba kwa maendeleo kwenye ngazi za familia, jamii na taifa pia.
Visingizio kuwa wanatafuta fedha za kujikimu ndiyo maana wanalima au kuuza bidhaa za vyakula zilizochafuliwa na moshi wa injini kisikubalike kwani vyote vinadhuru afya.
Ni vema kufikiri kuwa hata usipoathirika leo kwa kupata magonjwa yanayoambatana na moshi huo hapo baaadaye kuna hatari ya kusumbuliwa na maradhi kwani mtu anapokua na umri mkubwa matatizo ya kiafya yaliyojificha kwa muda mrefu huibuka.
Ikumbukwe kuwa ni bora kuchukua tahadhari kwani kadiri watu wanavyozeeka, mifumo ya kinga hudhoofika vilevile, uzee una uwezekano mkubwa wa kuwa na changamoto za kiafya kuliko ujana.
Ni muhimu kuwa na tahadhari na umakini kwa kuukwepa moshi wa petroli na dizeli na kuacha kufanya biashara karibu na barabara ili kujikinga na magonjwa ambayo yanaweza kuepukika hasa kutoka kwenye vyombo vya moto.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED