Mwamuzi Arajiga chezesha vyema kama 'dabi' iliyopita

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 10:33 AM Apr 20 2024
Mwamuzi Ahmed Arajiga.
Picha: Maktaba
Mwamuzi Ahmed Arajiga.

MWAMUZI Ahmed Arajiga amechaguliwa tena kuchezesha mechi ya watani wa jadi, maarufu kama 'dabi' itakayochezwa leo, kwenye Uwanja wa Banjamin Mkapa, Dar es Salaam kuanzia saa 11:00 jioni.

Arajiga ndiye aliyechezesha mechi iliyopita ya Novemba 5, mwaka jana, iliyochezwa kwenye uwanja huo huo, wenyeji Simba wakipokea kipigo kitakatifu cha mabao 5-1.

Ameingia katika rekodi ya kuchezesha mechi mbili za Ligi Kuu za Simba na Yanga kwa msimu mmoja, mzunguko wa kwanza na wa pili, kitu ambacho ni aghalabu sana kutokea.

Shirikisho la Soka Nchini (TFF) na Bodi yake ya Ligi (TPLB), imemwamini kwa mara nyingine tena Arajiga si kwa bahati mbaya.

Ni kwa sababu mechi iliyopita alichezesha kwa makini na uwezo wa hali ya juu kiasi pamoja na Simba kufungwa idadi kubwa ya mabao, hakuna mwanachama au shabiki yoyote wa timu hiyo aliyemlaumu mwamuzi.

Kila mmoja aliyekuwa uwanja na aliyekuwa akiangalia kwenye televisheni alilaumu kile ambacho aliamini kilisababisha bila kumtaja mwamuzi.

Ndiyo maana hadi leo, si wengi wanaojua katika mechi ile, ni Arajiga aliyechezesha.

Kama angechezesha vibaya, si asingepewa tu mechi hii, lakini hata jina lake lingekuwa midomoni mwa mashabiki mpaka dabi hii ya leo itakapochezwa.

Baada ya mechi ile, mashabiki na wanachama na Simba, wengine waliwalaumu viongozi, kuna waliolaumu wachezaji, na wapo waliomlaumu aliyekuwa Kocha Mkuu, Roberto Oliveira 'Robertinho', na ndiyo mechi ilisababisha atimuliwe.

Arajiga, alifanya mashabiki kuongea soka badala ya kumzungumzia mwamuzi. Wanachama na mashabiki wa Yanga waliondoka wakimsifia Kocha, Miguel Gamondi na wachezaji wao kwa soka safi waliloonyesha kiasi cha kuibuka na ushindi huo mnono.

Alichofanya mwamuzi siku ile aliacha soka lichezwe na matokeo yaamuliwe kwa uwezo na viwango vya wachezaji na si yeye kutumia nguvu kutaka kuibeba timu moja au 'kubalansi.'

Baadhi ya waamuzi wanaochezesha mechi hiyo wanaonekana kuingia na presha zaidi kuliko hata wachezaji wenyewe.

Inawezekana kwa sababu ya woga wa dabi, au tayari ana maelekezo ya nani anatakiwa kushinda kutokana na sababu mbalimbali, ikiwamo rushwa.

Matokeo yake kunakuwa na maamuzi ya ovyo kiasi mechi ikimalizika, mashabiki badala ya kuzungumzia mpira, kusifu mbinu za makocha na uwezo ulioonyeshwa na wachezaji, anazungumziwa mwamuzi na maamuzi yake yote uwanjani.

Hali hii ilikuwa ikisababisha baadhi ya dabi kutokuwa na mvuto, badala yake lawama na kelele kutoka kwa mashabiki, ingawa ni kweli wapo baadhi yao ambao wao timu ikifungwa hata kama ikipoteza kimpira, mwamuzi anahusika.

Ninachomshauri Arajiga kuchezesha kama alivyofanya mechi iliyopita, akiacha soka lichezwe na matokeo yajiamue yenyewe kwa timu itakayoizidi nyingine kwa kiwango, mfumo na uwezo wa wachezaji wake uwanjani.

'Akopi na kupesti' kile alichokifanya siku hiyo ili aendelee kujizoea sifa kwa sababu inawezekana kabisa hata msimu ujao akapewa tena dabi nyingine kwa mara ya tatu au ya nne kabisa.

Ajiondolee lawama na kuwa nyota wa mchezo badala ya wachezaji. Asiogope kufanya maamuzi magumu kama alivyofanya mechi iliyopita dakika ya 85 alipotoa penalti kwa Yanga, wakati tayari Simba ikiwa 'imeshaloa' mabao manne.

Inapohitajika kadi ya njano, nyekundu, itoke, asisubiri kusawazisha makosa, yaani mmoja anafanya anamezea, halafu mwingine anafanya baadaye anaacha na sababu aliacha ile ya kwanza, mechi itamshinda.

Nafikiri Arajiga ataendelea kuchezesha vyema ili kujijengea heshima, kupewa mechi mbili za dabi ndani ya msimu mmoja si kubahatisha, ni dhahiri 'wakubwa' wamemwamini, lakini pia ni kama mtego kwake.