Simba tengenezeni upya kikosi chenu, kimechoka, hakina ari

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 03:14 PM Apr 15 2024
Kikosi cha klabu ya Simba.
PICHA: SIMBA SC
Kikosi cha klabu ya Simba.

TANGU msimu uliopita kikosi cha Simba kilionekana kuwa kimechoka, kinahitaji kufanyiwa marekebisho makubwa.

Matokeo yake kilichofanyika ni kusajili wachezaji ambao walionekana ni kama kuja kuongeza upana tu wa kikosi na wala si wa kuingia moja kwa moja.

Viongozi wa Simba wakaendelea kuamini kuwa kina John Bocco, Mzamiru Yassin, Luis Miquissone, Aishi Manula, Shomai Kapombe, Mohamed Hussein 'Tshabalala', na wenzao wataendelea kuibeba Simba.

Kilichotokea wengi wa wachezaji wao wamechoka. Viwango vyao vimeporomoka na hala kingine cha kuongeza kwenye uwezo walionao.

Waliosajiliwa nao asilimia kubwa hawakuingia moja kwa moja kwenye kikosi, badala yake wengi wamekuwa ni wa benchi, na wanaoaza wameshindwa kuibeba timu kama ilivyokuwa kina Bocco zamani.

Kinachotokea Simba ni kwamba viongozi walishindwa kutambua alama za nyakati. Wakashindwa kusikia kengele ya hatari. Wangefanya hivyo wala leo timu hiyo isingekuwa kama ilivyo sasa.

Simba imekosa mvuto, na hata klabu inazocheza nazo haziiogopi kama ilivyokuwa zamani kwa sababu si tishio tena.

Juzi, baada ya sare ya bao 1-1 dhidi ya Ihefu, Kocha Mkuu, Abdelhak Benchikha, alikaa peke yake benchini kwa zaidi ya dakika 10, akiwa na huzuni kubwa baada ya kushuhudia kitu ambacho hakukitegemea kwa wachezaji wake.

Hiki kinachotokea Simba kwa sasa hakijaja kwa bahati mbaya, bali ni ukosefu wa uwajibikaji kwa viongozi. Ni kitu ilibidi wakifanye?

Baada ya kumalizika kwa ligi ya msimu juzi, wachezaji wengi wa Simba walionekana wamechoka kwa viwango vyao kushuka, kucheza mechi nyingi bila kupumzika, umri na pia tayari wengi walikuwa na mafanikio ya kutwaa ubingwa mara nne, Kombe la FA, pamoja na robo fainali tatu za Ligi ya Mabingwa. Hiyo ilitosha kuanza kutengeneza Simba mpya.

Ilitakiwa kusajili wachezaji wengine ambao wataingia moja kwa moja kwenye kikosi na kuwaweka benchi wale waliopo, na si wa kuja kusubiri.

Badala yake kina Bocco ndiyo wakaendelea kuwa tegemeo hadi ligi ilipomalizika.

Bado viongozi wa Simba hawakushtuka ligi ilipomalizika, haikufanya usajili wa maana hata kwa mabeki wa pembeni kina Tshabalala na Kapombe ambao walitakiwa waletewe wachezaji wa kuingia moja kwa moja, na si kina David Kameta na Israel Mwenda ambao wanasubiri.

Tshababa yupo Simba tangu 2014 akitokea Kagera Sugar, Kapombe aliingia Simba 2013, akitokea Polisi Morogoro, pamoja na kwamba alikwenda nje ya nchi na baadaye kurejea akiwa Azam FC na kurejea tena timu yake ya zamani, haiwezekani hadi leo hii akawa ndiyo tegemeo.

Yanga si tu kwamba haina kina Juma Abdul na kina Kelvin Yondani waliocheza na kina Kapombe na Tshabalala, pia imemuacha hata Djuma Shaaban na kuchukua damu changa, huku Simba ikiendelea na wachezaji wale wale miaka nenda rudi.

Na kwa bahati mbaya sana, karibu misimu mitatu Simba ilikuwa ikisajili wachezaji wakati haina makocha. Viongozi ndiyo walikuwa wanasajili, wakati huo ikiwa ama makocha wameondoka wenyewe, au wametimuliwa na wanaokuja wanakuta usajili umeshafanyika.

Hiki ndicho kilichoimaliza Simba na sasa inatakiwa kufanya usajili mkubwa na wa nguvu. Kama inataka kurudi kwenye ubora wake, hivyo msimu ujao inabidi itoboke, iwe na fungu kubwa la usajili kuliko wakati mwingine wowote, kwa sababu inavyoonekana wachezaji wake wengi kiasi cha asilimia 80 wamechoka. Hawana nguvu za kuipigania Simba na kwa sasa hawana wanachotafuta, kwani kila kitu wameshapata.

Simba isingefika hapa, lakini hiki kinachoonekana sasa ni alama dhahiri ya kuonyesha kikosi kipya kinahitajika.

Ni wakati sasa wa viongozi kuungana na mwekezaji, pamoja na kocha Benchikha kukaa pamoja na kuangalia ni wachezaji gani wa kusajili kwa ajili ya msimu ujao.

Klabu kama ya Simba, inatakiwa isajili wachezaji wenye uwezo na ubora mkubwa ili kuendana na hadhi yake, kwa sasa ambapo ipo tano bora Afrika, si ya kufanyia majaribio, au yeyote tu anaweza kuichezea.