Wanaotoa maoni Simba wanafungiwa, wanaoshusha 'brandi' wao wanaachwa

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 11:16 AM Jun 17 2024
Wanachama maarufu wa Simba, Agness Daniel ‘Aggy Simba’ na Mohamed Hamisi ‘Dk Moo’.
Picha: Mtandao
Wanachama maarufu wa Simba, Agness Daniel ‘Aggy Simba’ na Mohamed Hamisi ‘Dk Moo’.

NILIANDIKA wiki iliyopita kuwa kosa walilofanya viongozi wa Simba ni kutowajibika kuita wanachama wao ili kuwaambia kinachoendelea wakati timu inafanya vibaya katika mechi za Ligi Kuu na Kombe la FA.

Lakini walipoguswa kwenye maslahi yao ya kutaka kujiuzulu, wakaitisha vikao ambavyo si rasmi kwa ajili ya kile kilichoonekana kujihami.

Nikaandika kwa nini hawakufanya hivyo awali wakati timu inafanya vibaya, kwa sababu angalau wangeshusha presha ya wanachama na mashabiki wao.

Kilichoonekana ni kwamba baadhi ya viongozi wa Simba ni kama hawaangalii sana heshima, mafanikio na 'brandi' ya klabu, badala yake wanajiangalia wao tu.

Moja ya sifa ya kuongozi ni kuipandisha thamani klabu, kuitetea na kuilinda nembo, nguvu na gharama zote, baadaye ndiyo unaweza sasa kujiangalia mwenyewe.

Naona hilo limejirudia tena na sitolinyamazia, niliongelee tena ili kuwakumbusha uongozi wajibu wao ni upi ndani ya klabu.

Juzi Sekretarieti na klabu ya Simba imetangaza kuwafungia kujihusisha na masuala ya klabu wanachama wawili, Mohamed Khamisi Mohamed, maarufu kama Dk. Mohamed, na Agnes Daniel, maarufu kama Aggy Simba mpaka pale Kamati ya Maadili ikapoamua vinginevyo.

Sekretarieti ikadai imepokea malalamiko mengi ya kimaadili dhidi ya wanafamilia hao wa klabu, ikiwamo kuitisha mikutano kinyume na taratibu na kuchochea migogoro klabuni.

Mwisho ikasema itawafikisha wanachama hao mbele ya Kamati ya Maadili hivi karibuni.

Wala sipepesi macho nikisema haya yote yanatokea kutokana na sakata la kushinikizwa kujiuzulu kwa wajumbe upande wa wanachama.

Binafsi sikubaliani na adhabu hii kwani imekuwa kubwa mno, tofauti na kile ambacho walikuwa wanahitaji kukifanya wanachama hao.

Hawa walikuwa katika harakati za kutaka kuijenga Simba kutokana na kile kilichotokea cha kufanya vibaya kwa timu, iliyokuwa inaongozwa na viongozi hao ambao hadi leo hawajaitisha mkutano kuwaambia sababu ya kufanya vibaya msimu uliomalizika.

Mimi sidhani kama walikuwa wanachochea mgogoro, bali walikuwa katika harakati za kutoa maoni yao kama wanachama na mashabiki ili yafanyiwe kazi na uongozi, pamoja na malalamiko ni kwa nini timu ilifanya vibaya, kipi kilisababisha usajili uwe mbovu, na watajikwamuaje kutoka hapo. 

Nadhani baadhi ya viongozi walichofanya ni kujilinda wao wenyewe, sidhani kama walikuwa na haja ya kufanya hivyo zaidi ya kuwaita na kuongea nao kwa sababu wote ni Wanasimba wanaojenga nyumba moja tu.

Hawa hawa akina Aggy Simba ndiyo wanaosafiri na timu kila inapokwenda ndani na nje ya nchi kuishangilia na kuwapa hamasa wachezaji, leo hii wanaonekana wanachochea migogoro, ambayo haipo.

Ndiyo wanaokusanya pesa na kuwasaidia matibabu baadhi ya wanachama na Simba waliopata ajali mbili, Machi 28, walipokuwa wanatoka mikoani kwenda Dar es Salaam, kutazama mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika wakati ya timu yao ikicheza dhidi ya Al Ahly ya Misri. 

Hawa wanaojitolea yote haya ndiyo wanaopewa adhabu hii ya kufungiwa.

Kama kuchukua hatua, nadhani sektetarieti ingefanya hivyo kwa baadhi ya wanaojiita wanachama na mashabiki wa Simba ambao wanashinda mitandaoni kuitukana, kuidhalilisha, kuiponda, kushusha hadhi na 'brandi' ya klabu.

Hawa mbona hatujawahi kuona angalau wakipata onyo, au kuchukuliwa hatua kwa sababu moja kwa moja wanaiharibu nembo ya Simba.

Wanavaa jezi za Simba, lakini hawana chochote kizuri ambacho timu yao inafanya. Aggy na Dokta Mohamed wanaonekana wanaongea kwa uchungu. Lakini hawa wengine wanaonekana wanaongea kwa kejeli, dharau na udhalilishaji uliovuka mipaka.

Sijaona viongozi wakidili nao kisheria ili wathibitishe kwanza kama wao ni wanachama au mashabiki wa Simba kama wanavyojinasibu, halafu mengine yafuate.

Na kwa nini wavae jezi za klabu na kuidhalilisha? Kama ni mashabiki wa timu nyingine waliojificha kwenye kivuli hicho, basi wavae jezi zao. Badala yake wamekaa kimya tu.

Hii ina maana hawatumii nguvu kuitetea nembo ya klabu, au kuilinda, ukiharibu 'brandi' ya Simba kwao sawa tu, wanaonekana hawana mpango na hilo, ila ukigusa maslahi yao ndipo wanapotumia nguvu na mamlaka walizopewa na klabu ili kujilinda wao binafsi. Kwa nini wasifanye hivyo pia kuilinda klabu yenyewe ya Simba dhidi ya wanaochafua nembo?