ACT yakomaa wajumbe tume uchaguzi kujiuzulu

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 08:43 AM May 26 2024
Wafuasi wa chama cha ACT- Wazalendo.
Picha: Mpigapicha Wetu
Wafuasi wa chama cha ACT- Wazalendo.

CHAMA cha ACT Wazalendo kimezidi kuwataka wajumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) wajiuzulu na kufanyika mabadiliko madogo ya Katiba kuwaondolea kinga viongozi hao ya kung’ang’ania kupata fursa nyingine katika Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi .

Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho Tanzania Bara, Isihaka Mchinjita, aliyasema hayo jana katika mkutano wa hadhara uliofanyika Tanga mjini.

“Hawa ni wajumbe wa tume ambao mikono na nguo zao zimeloa damu na machozi ya watanzania. Wajumbe hawa kuwavika koti linalowaita kuwa ni watu wema ni dhihaka dhidi ya utu na uhuru wa Tanzania,” alidai.

Mchinjita alimwomba Rais Samia Suluhu Hassan asimamie wajumbe hao wa tume kujiuzulu na ahakikishe yanafanyika mabadiliko madogo ya katiba ili kuwaondolea kinga ya kung’ang’ania kupata fursa nyingine.

“CCM ni wanufaika wa hujuma ya uchaguzi ya 2020 iliyofanywa chini ya usimamizi wa tume hii. Chini ya wajumbe hawa wa tume, zaidi ya madiwani 800 na wabunge 28 wa CCM (Chama Cha Mapinduzi) walitangazwa kupita bila kupingwa,” alisema.

Katika hatua nyingine, kiongozi huyo alisema Tanzania inaendeshwa kwa madeni kwa kile alichokiita kutokana na wizi unaofanywa na viongozi wa serikali ya CCM.

“Ripoti ya CAG (Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali) imeonesha mwaka huu peke yake Sh. trilioni sita zimeibwa, hii ni sawa na asilimia 20 ya kodi tunayokusanya kwa mwaka, alisema.

Alisema wanalipa deni la Sh. trilioni tisa na mishahara Sh. trilioni 14, hivyo miradi ya maendeleo inategemea mikopo.

“Hii maana yake kila Sh. 100 tunayokusanya, Sh. 20 inaibwa, Sh. 31 inalipa deni na Sh. 49 ni mishahara na posho, hivyo kumaliza fedha zote tulizochanga kupitia kodi na shughuli za maendeleo ya wananchi tunategemea mikopo na wahisani ambako huko ndiko ufisadi mkubwa unafanyika,” alisema.

Katika mkutano huo, kiongozi huyo alizungumzia pia suala la viwanda akisema baadhi vimekufa na vilivyobinafsishwa vimegeuzwa magofu na vile vikubwa vimekuwa maghala.

“Tanga ilikuwa ni ukanda wa viwanda kwa Tanzania ilikuwa na kiwanda kikubwa cha mbolea , kiwanda cha plastiki (Amboni Plastic) kiwanda cha chuma, viwanda vya sabuni, kiwanda cha mashati ya Gossage na kiwanda cha nguo na kiwanda cha mbao ambavyo vyote vimekufa yamebaki magofu,” alisema.

Kuhusu uuzwaji wa kiwanda cha saruji cha Tanga, alidai kwa sasa hakizalishi saruji  badala yake kimekuwa sehemu ya kuchukua malighafi kupeleka Dar es Salaam kwa ajili ya uzalishaji.

“Kilimo mkonge ambao ndio zao kuu la biashara mkoa wa Tanga limeonekana kufa taratibu bado hakuna viwanda vya kutosha vya uchakataji wa zao hili.

“Uzalishaji wa mkonge mwaka 2020 ulikuwa ni tani 36,379, mwaka 2021 tani 36,170, mwaka 2022 zilikuwa tani 44,151, mwaka 2023 tani 56,732, taarifa zinaonesha Tanzania mwaka 1970 iliuzwa nje tani 230,000 ikifuatiwa na Brazil na Mexico,” alisema.

Alisema kwa sasa Tanzania ni nchi ya pili ya uzalishaji wa katani duniani lakini hakuna mkazo na jitihada za makusudi za kuendelea zao hilo.

 Kuhusu Bandari ya Tanga, alisema licha ya kuunganishwa na reli na kuwa karibu na mikoa kadhaa, bado haitumiwi kimkakati kuchangamsha uchumi wa mkoa huo.