Mzee wa kanisa afuturisha Waislamu

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 05:38 PM Mar 31 2024
Waiamu wakifuturu wakati wa mfungo wa Ramadhani.
PICHA: MGANGA ONE
Waiamu wakifuturu wakati wa mfungo wa Ramadhani.

MZEE wa Kanisa la Waadventista Wasabato la Muheza Central, wilayani hapa mkoani Tanga, John Mdoe, amewafuturisha waumini wa dini ya Kiislamu.

Mdoe kwa kushirikiana na familia yake, wametoa sadaka hiyo kwa zaidi ya Waislamu 100 juzi nyumbani kwake, Mtaa wa Mdote. Mgeni  rasmi alikuwa Shekhe wa Wilaya ya Muheza, Abdallah Seif na ilihudhuriwa pia na Katibu wa BAKWATA Wilaya hiyo, Shabani Nguzo. 

Viongozi hao wa dini walitumia hafla hiyo pia kuiombea nchi amani, utulivu na mshikamano pamoja na kuombea viongozi wa taifa wakiongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Mdoe ametumia fursa hiyo pia kukabidhi zawadi ya nguo aina ya kanga na cheti cha Ramadhani Kareem kwa Shekhe wa Wilaya Seif na Katibu wa BAKWATA wilaya, Nguzo. 

Akizungumza wakati wa futari hiyo, mzee huyo amesema Kanisa la Waadventista Wasabato linaamini kuhusu uhusiano mzuri baina ya Wasabato na dini ya Kiislamu.

Mchungaji wa Kanisa la Sabato, Mtaa wa Michungwani Muheza Mjini, Daud Masindi, amesema katika kipindi hiki cha mfungo wa Ramadhani, hiyo iwe ni sehemu ya kusema hao ni ndugu zao.

“Iwe sehemu ya kuungana nanyi kumwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kutupa amani katika maisha yetu, jamii zetu, taifa letu la Tanzania. Tunamwomba Mungu amjaalie Rais Samia na viongozi serikalini amani,” amesema.

Shekhe wa Wilaya ya Muheza, Abdallah Seif, amempongeza na kumshukuru Mzee wa Kanisa  hilo kwa kuandaa futari hiyo na kusisitiza kuwa, ni jambo la kheri na la kuigwa ambalo linaleta umoja na amani kwa nchi.

Katibu wa BAKWATA wa Wilaya, Nguzo, amesema wataendelea kutoa ushirikiano kwa wakristo katika wilaya hiyo ili kudumisha upendo, umoja na mshikamano.