DC Mhita: Barabara zilizoharibiwa na mvua kukarabatiwa

By Shaban Njia , Nipashe Jumapili
Published at 10:58 PM Apr 07 2024
Barabara iliyoharibiwa na mvua.
Picha: Mpigapicha Wetu
Barabara iliyoharibiwa na mvua.

MKUU wa Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga Mboni Mhita amekagua miundombinu ya barabara iliyoharibiwa na mvua za masika zinazoendelea kunyesha maeneo mbalimbali hapa nchini, huku akiahidi kufanyiwa matengenezo baada ya mvua kukata na Wakala wa Barabara za Mjini na Vijijini (TARURA).

Mhita aliyabainisha haya leo wakati wa ziara yake ya kusikiliza na kutatua kero mbalimbali zinazowakabili wananchi wa halmashauri za Msalala, Ushetu na Manispaa ya Kahama huku akiambatana na  Kamati yake ya ulinzi na usalama na watalaamu wengine kutoka katika halmashauri hizo.

Amesema, barabara nyingi za nje ya mji zimeharibika kutokana mvua za masika zinazoendelea kunyesha kulinganisha na zile za mjini na kusababisha mawasiliano ya barabara kutokuwa na uhakika ila baada ya mvua kukatika Serikali kupitia TARURA watahakikisha wanarejesha miundombinu hiyo sawa.

Hoja hiyo ilijibiwa baada ya kuibuliwa na wananchi wa kata za Nyahanga na Mhunguliwa katika mkutano wa hadhara huku wakidai barabara nyingi zimeharibika kutokana na mvua za masika na kuomba baada ya mvua zifanyiwe marekebisho ili kurahisisha usafirishaji wa bidhaa hadi somo na mambo mengine.