Dereva Shabiby mbaroni kusababisha ajali

By Ida Mushi , Nipashe Jumapili
Published at 09:29 AM May 26 2024
Basi la Shabiby likiwa limeanguka eneo la Kihonda kwa Chambo jana Mei 25, 2024 na kusababisha majeruhi 22.
Picha:Mpigapicha Wetu
Basi la Shabiby likiwa limeanguka eneo la Kihonda kwa Chambo jana Mei 25, 2024 na kusababisha majeruhi 22.

JESHI la Polisi Mkoa wa Morogoro linamshikilia dereva wa basi la kampuni ya Shabiby, Sadick Said, kwa tuhuma za kusababisha ajali katika eneo la Kihonda kwa Chambo, barabara kuu ya Morogoro - Dodoma na kusababisha watu 22 kujeruhiwa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Alex Mkama, amethibitisha kukamatwa kwa dereva huyo aliyesababisha ajali wakati akiendesha basi la abiria lenye namba za usajili T. 341 EEU, akitokea Dar es Salaam kwenda Dodoma jana, majira ya saa 12:00  alfajiri. 

Basi hilo lilipinduka kutokana na kilichotajwa kuwa ni uzembe wa dereva kukosa umakini barabarani alipojaribu kuipita bajaji  iliyokuwa mbele yake na kukutana na bajaji nyingine na katika kujaribu kuikwepa, alishindwa kumudu na basi hilo likapinduka. 

Baadhi ya abiria waliokutwa eneo la tukio, Alikwe Masaga na majeruhi Hamis Shaban aliyekutwa Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Morogoro, walisema kwa nyakati tofauti walitoka Dar es Salaam majira ya saa 9:00 usiku kabla ya kufikwa na ajali hiyo. 

"Tulianza safari alfajiri muda wa saa 9:00 usiku kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma, tukapita salama stendi ya Msamvu Morogoro majira ya sa 12 kasoro asubuhi ambako tulipata mapumziko mafupi na kujisaidia) na kuendelea na safari.

 “Tulipofuika Kihonda jirani na daraja la reli ya mwendo kasi, ndipo dereva alitaka liipita  bajaji iliyokuwa mbele yake  lakini ghafla ilikuja bajaji nyingine ndipo dereva akajaribu kukwepa na  kusababisha gari kupinduka, " alisema Masaga. 

Ofisa Habari na Uhusiano wa Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Morogoro, Beatrice Kapori, alithibitisha kupokea majeruhi 22 wa ajali hiyo ambao wanaendelea na matibabu na  mpaka jana mchana walikuwa wanaendelea vizuri. 

Naye Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Dharura katika hospitali hiyo, Nafsa Maromba, aliasema kati ya  majeruhi hao, 15 ni wanawake na saba ni wanaume na walioumia sana ni watano, wakiwamo watatu waliopata mivunjiko katika maeneo mbalimbali  huku wawili wakiumia zaidi maeneo ya mgongo. 

Alisema majeruhi wengine wamepata majeraha madogo madogo na michubuko na baadhi yao wamepewa matibabu na kuruhusiwa. 

Majeruhi Hamisi Shabani aliyekutwa hospitalini hapo,  alibainisha kuumia zaidi maeneo ya mguu na mgongo lakini maumivu yamepungua kidogo na anaendelea na uangalizi wa madaktari.