HESLB yaanika utaratibu upangaji mikopo

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 08:24 AM Jun 09 2024
Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB,  Dk. Bill Kiwia.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dk. Bill Kiwia.

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetoa ufafanuzi kuhusu utaratibu unaotumika katika uchambuzi na upangaji wa mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu na kusema upangaji huo huzingatia uhitaji wa mwombaji na kuwa si waombaji wote hupata asilimia 100.

Ufafanuzi wa HESLB unatokana na taarifa iliyochapishwa na gazeti hili juzi kuwa kuna uwezekano baadhi ya wanafunzi hawatapata mikopo kwa asilimia 100 kutokana na bajeti iliyotengwa ya Sh. Bilioni 787 kwa wanafunzi 250,000 katika mwaka wa masomo 2024/25.

“Upangaji mikopo ya elimu inayotolewa na HESLB huzingatia uhitaji wa mwombaji mkopo ambao hupimwa kwa taarifa anazojaza wakati wa maombi, hivyo si kila mwombaji ana uhitaji wa asilimia 100,” alisema Meneja Mawasiliano wa HESLB, Venerranda Malima. 

“Kwa mfano, miongozo yetu inaeleza kipaumbele hutolewa kwa waombaji wenye ulemavu, yatima na wale ambao wanatoka katika kaya zinazohudumiwa na TASAF, waombaji kutoka katika makundi haya huwezi kuwalinganisha na waombaji wa kawaida,  waombaji hutofautiana uwezo na uhitaji,” aliongeza Malima.

Juzi, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB,  Dk. Bill Kiwia, alitangaza kufunguliwa kwa dirisha la kuomba mikopo kwa njia ya mtandao kwa siku 90 kuanzia Juni Mosi hadi Agosti 31, mwaka huu.

Dk. Kiwia alisema mwombaji mkopo anapaswa kuingia katika tovuti rasmi ya HESLB (www.heslb.go.tz) na kubofya sehemu ya kuomba mkopo, atajisajili huko kwa kutumia namba yake ya Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne na kufuata maelekezo.

Nipashe katika toleo lake la juzi ilisema katika wa masomo wa 2024/25, dirisha kwa ajili ya mikopo kwa wanafunzi wanaotarajiwa kujiunga na masomo ya vyuo vikuu limefunguliwa kwa wanafunzi 250,000 wanaotarajia kunufaika na fursda hiyo.

Hilo ni ongezeko la wanafunzi 25,944 kulinganishwa na wanufaika 224,056 wa mikopo hiyo kwa mwaka wa masomo 2023/24.

Pamoja na kuonyesha kiasi cha fedha na idadi ya wanafunzi, Nipashe ilifanya uchambuzi na kubainisha kuwa ata hivyo, kiasi kilichotengwa kwa ajili ya utoaji mikopo hiyo kinazua utata na kutoa ishara kwamba wanufaika wengi hawatopewa mkopo kwa asilimia 100.

Kwa mujibu wa uchambuzi huo, katika lugha ya hisabati, Sh. bilioni 787 zilizotengwa na serikali kwa ajili ya mikopo kwa wanufaika 250,000 zina maana kutatolewa mkopo wa wastani wa Sh. milioni 3.148 kwa kila mnufaika. 

Uchambuizi huo ulionyesha kuwa ni ishara kwamba wanafunzi wengi hawatapewa mkopo kwa asilimia 100 kwa kuwa fedha kwa ajili ya kujikimu ni Sh. milioni 2.4 kwa mwaka (Sh. 10,000 kwa siku).

Ukitoa Sh. milioni 2.4 katika fungu la wastani wa Sh. milioni 3.148 kwa kila mnufaika, kitabaki kiasi cha Sh. 748,000 ambacho ndicho mwanachuo atalazimika kukitumia kama kianzio kulipa ada ya chuo, mafunzo kwa vitendo (PT), utafiti, vitabu na vifaa vingine vya darasani.