Kasi ongezeko ‘single mothers’ yatisha

By Jenifer Gilla , Nipashe Jumapili
Published at 12:11 PM Apr 14 2024
Kasi ya ongezeko la ‘single mothers’ inatisha.
PICHA: MPIGAPICHA WETU
Kasi ya ongezeko la ‘single mothers’ inatisha.

“SITAKI mwanamume wa kunimiliki na sina shida ya ndoa. Kama ni mtoto ninaye sasa ndoa ya nini?

Ilikuwa kauli ya mwanadada mmoja akiwa na wenzake watatu katika mapumziko ya jioni sehemu ya starehe baada ya saa za kazi, pengine wakisubiri muda kupungua kwa msongamano wa magari ili warejee nyumbani. Kauli hiyo ilipokewa kwa vicheko na wenzake ambao walionekana kukubaliana naye. 

Kimtazamo, wanadada hao walionekana kuwa ni watu wenye uwezo kutokana na hali zao. Kundi hilo ni kiwakilishi tu cha kinadada na kinamama wengi ambao hawataki ndoa na wengi wao wameshazaa ama mtoto mmoja au wawili na wana uwezo wa kuwalea na kuwatunza bila msaada wa baba zao. Miongoni mwao ni ni mameneja, wakurugenzi katika taasisi au wafanyabiashara.

Hivyo ndivyo hali ilivyo kwa kinamama hao ambao wanalea Watoto wenyewe, maarufu kama ‘single mothers’ na ongezeko la kundi hilo kwa sasa linakua kwa kasi nchini. Madada na wamama hao wenye ukwasi wanachagiza ongezeko hilo, mbali na wale waliofiwa au kuachwa na waume zao.

Utafiti uliofanywa na ICF Macro mwaka 2011  unaonyesha kuwa  nchini Tanzania, asilimia  19 ya watoto wanalelewa na mama pekee na asilimia tano wanalelewa na baba wakati ripoti iliyofanyika mwaka 2016 inaonyesha kuwa idadi ya kinamama wanaolea watoto ni asilimia 38.

Mfanyabiashara wa nguo Kariakoo, Salma Rashid, anasimulia kuwa baada ya kuachana na mwenza wake akiwa na mtoto wa miezi sita, alimzuia kabisa kuwahudumia kwa chochote kwa sababu anajiweza.

Anasema mwanamume huyo aliwasumbua kwa muda mrefu kutaka kuhudumia mtoto wake na alivyoona usumbufu unazidi, alibadilisha namba ya simu na kuhama eneo walikokuwa wanaishi na sasa anaishi kwa amani na mtoto wake.

“Sihitaji chochote kutoka kwake. Kama  tumeamua kuachana kila mtu afanye mambo yake. Nina  uwezo wa kulea na kusomesha mtoto wangu sina shida na chochote kutoka kwake,” anasema Salma.

Jamila Abdallah anasema haoni haja ya kusumbuana na mwanamume kuhusu malezi ya mtoto wakati Mungu amempa uwezo na kumlea mwenyewe.

Anasema kitendo cha kumpigia mzazi mwenzake kumkumbusha majukumu na ulezi wa mtoto ni kujishushia heshima kwa mtu ambaye hastahili, ikizingatiwa kuwa  alimwacha na maumivu makubwa.

Mama mwingine, Cecilia Bernard, anasema anafurahi kuona mwanamke analea mtoto wake mwenyewe kwa kuwa inamjengea heshima na kuondoa dharau mbele ya mwanamume.

“Unajua ukiwa unalelewa mtoto na mwanaume ambaye mmeshaachana anakudharau. Kwanza, unakuwa unamnyenyekea tu yeye maana ndiye anakusomeshea  mwanao. Mimi  ninayapitia hayo kwa sasa na ikitokea siku nikapata pesa, mwanangu nalea mwenyewe,” anasema.

Wakati wanawake hao wanaona ni vyema kukaa na kuwalea watoto bila msaada wa baba zao, Salum Abdallah anasema kitendo cha kukataa kushirikiana kulea watoto na wenza wao kisa wameachana si kizuri kwa kuwa kinamnyima baba haki ya kulea watoto. Anasema kitendo hicho pia kinawafanya watoto  kukosa malezi ya baba.

Anasema wanawake wa aina hii wengi wao hawataki kabisa baba na mtoto wawasiliane, wakidhani  kuwa wao pekee wanatosha kulea kumbe kila mzazi ana nafasi na umuhimu wake katika makuzi ya mtoto.

TAKWIMU ZA TALAKA 

Talaka na kutengana kwa wanandoa ni moja ya sababu za ongezeko la kinamama hao.  Takwimu za Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) zinaonyesha kuwa mwaka 2019 talaka zilikuwa 442, mwaka 2020 zilifikia 511 na mwaka 2021 ziliongezeka hadi kufikia 550.

Aidha, takwimu za migogoro ya ndoa zilizotolewa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum zinaonyesha kulikuwa na migogoro 39,571 kwa kipindi cha Julai 2021 na mpaka Aprili, 2022  migogoro 19,262 ilipata suluhu, 15,718 bado ilikuwa katika usuluhishi na 4,576 mahakamani.

WASEMAVYO WATAALAM

Mwanasaikolojiatiba, Dk. Saldeen Kimangale, anasema chimbuko la suala hilo ni kuwapo kampeni za kumwinua na kumwonyesha mwanamke  kuwa anaweza, hivyo kusababisha hali ya kujiamini kuwa kubwa kiasi cha kutoona umuhimu wa mwanamume katika maisha yake.

Anasema pamoja na kuwa kuna ushahidi wa kutosha kuwa mtoto kulelewa na mzazi mmoja hakuna madhara, bado kuna ushahidi mwingi pia unaoonyesha kuwa mtoto aliyelelewa na mzazi mmoja, hasa mama, anakabiliwa na changamoto za kihisia na kitabia.

“Watoto  waliolelewa na mzazi mmoja, hasa mama kwa sababu ya kutengana, ugomvi au kukomoana tu kama ilivyozoeleka, leo hii wanakabiliwa na tatizo kubwa la hasira za haraka, ugomvi wa mara kwa mara, kuharibu vitu au kupoteza, kukosa umakini na kujiingiza kwenye tabia hatarishi kama vile kutumia vilevi,” anasema.

Msaikolojiatiba Isack Lema anataja sababu nyingine kuwa ni uwapo wa taarifa nyingi mbaya zinazohusu uhusiano ambazo husambaa mitandaoni kama vile wanawake kuuawa na wenza wao, kupigwa na kusambazwa na kuwatia hofu wanawake kuendelea na uhusiano.

Kutokana na matukio hayo, anasema wanawake wengi wanakuwa hawana mpango wa kuishi na wanaume kwa kuhofia kudhuriwa na unapofika  umri wa kutaka Watoto, huamua kutafuta wanaume wa kuzaa nao tu kisha kutoweka na watoto.

Anasema wakati mwingine husababishwa na migogoro ya ndani na kufanya  wanawake  kupata  sonona na  kupunguza  hamu ya kujamiiana. Hali hiyo husababisha uhusiano kuvunjika na mama kuamua kulea mtoto mwenyewe.

Lema anataja pia uwapo wa hamasa kutoka kwa wanawake wenzao ikiwamo makundi yanayojiita ‘single mothers’ kwa kutiana moyo kuwa wanaweza na wengine hujifunza kutoka kwa mama zao.

KASISI ALONGA

Padre wa Kanisa Anglikana Mtaa wa Mikaeli na Malaika Wote, Tabata jijini Dar es Salaam, Joseph Upio,  anasema suala hilo si sawa kwa sababu vitabu vya dini vinakataza wanandoa kuachana na mama kulea mtoto mwenyewe ingawa kuna wakati  migogoro hutokea na kusababaisha hali hiyo kutokea. 

Anasema ni wajibu wa wazazi wote wawili kuwalea watoto hao ili wakue vizuri kiroho jambo ambalo ni vigumu kutekelezeka kwa mzazi mmoja kwa kuwa mtoto anajifunza kwa wazazi wote wawili.

NINI KIFANYIKE?

Dk. Saldeen anashauri wazazi kabla hawajaamua kuzaa, watafute wenza wenye mienendo inayofaa  ili wawatafutie watoto mama au baba bora.

“Tenga muda wa kutosha kujua historia ya makuzi ya huyo unayekwenda kumposa au anayekuja kukuposa. Kama  kuna maharibiko yoyote katika historia ya utoto wake, tambua kuwa yumo kwenye vihatarishi,” anasema.

Pia anawashauri wanawake wanaolea watoto wenyewe,  waache kukimbia, kujificha au kupambana wenyewe ili kuonyesha jamii kuwa wako imara wakati ukweli ni kwamba  wanatokota na kuyeyuka ndani kwa ndani.

Badala  yake, anasema  watafute  tiba na kisha wafanye juhudi wapate wenza sahihi, hata ikibidi warudiane na wenza wao baada ya kujifunza na kurekebisha makosa na dosari zao ili wawape watoto nafasi ya kufurahia utoto wao wakiwa na wazazi wote wawili.

Lema kwa upande wake, anashauri jamii kufundisha mabinti namna kuanzisha na kuishi  kwenye uhusiano wenye afya, ikiwamo kuwauliza wenza wao maswali ya msingi yatakayowapa majibu ya kule wanapoelekea.

Pia anasema wale waliotoka kweye uhusiano ambao si salama, watafute msaada wa kisaikolojia kabla ya kuingia kwenye uhusiano mpya ili kuondoa  mawazo chanya kwa kuwa si kila aliyeachika hajaolewa.

Padre Upio anasema ni jukumu la vyombo vyote vya dini kutilia mkazo katika maadili ya kidini ili kusiwapo ndoa zinazovunjika na wazazi wote wawasaidie watoto kukua kiroho.