"Kataeni kishika uchumba wakati bado ni wanafunzi"

By Rashid Nchimbi , Nipashe Jumapili
Published at 05:00 PM May 26 2024
Mkuu wa Dawati la Jinsia na watoto Wilaya ya Monduli Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Jacqueline Uhwelo.
Picha: Polisi Monduli
Mkuu wa Dawati la Jinsia na watoto Wilaya ya Monduli Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Jacqueline Uhwelo.

Wanafunzi wa Shule ya Wasichana ya Kipok iliyopo wilayani Monduli mkoani Arusha wameaswa kutokubali kishika uchumba wangali wakiwa wanaendelea na masomo.

Ushauri huo umetolewa na Mkuu wa Dawati la Jinsia na watoto Wilaya ya Monduli Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Jacqueline Uhwelo jana mchana wakati wa kikao kilichofanyika shuleni hapo kati ya Dawati hilo na wanafunzi hao wa kidato cha kwanza hadi cha Nne wapatao 1,000.

Alisema kwamba, kumekuwa na tabia ya baadhi ya makabila kupeleka  kishika uchumba kama vile Pete kwa wazazi wa wanafunzi wa kike huku wakitarajia wafunge nao ndoa mara tu baada ya kumaliza shule

Alisema hali hiyo inafifisha ndoto za wasichana hao ambao pengine wanawaza kusonga mbele kimasomo.

"Matukio hayo yanawaathiri sana baadhi ya wanafunzi ambao wengine wanapata ujauzito hata kabla ya kumaliza kidato cha Nne lakini pia kitendo hicho pia kinasababisha mwanafunzi ahamishe mawazo yake toka kwenye masomo na kufikiria kuolewa". Alifafanua mkuu huyo wa Dawati.