Kinana apokea malalamiko mauaji ya kutatanisha Serengeti

By Maulid Mmbaga , Nipashe Jumapili
Published at 06:03 PM Apr 14 2024
Abdulurhaman Kinana akiwa katika kikao maalum cha halmashauri kuu ya CCM Serengeti.
PICHA: MAULID MMBAGA
Abdulurhaman Kinana akiwa katika kikao maalum cha halmashauri kuu ya CCM Serengeti.

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara Abdulurhaman Kinana amepokea malalamiko mbalimbali yakiwemo madai ya mauaji ya kitatanisha dhidi ya wananchi katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti mkoani Mara.

Changamoto ya mauaji katika hifashi hiyo imeibuliwa leo mkoani Mara, wakati wa kikao maalum cha halmashauri kuu ya CCM Serengeti na Diwani wa Kata ya Mochochwe, Joseph Mhegete, aambaye amesema kuwa wananchi wake wamekuwa wakikamatwa, kuuawa na mifugo yao ikikamatwa inataififwa.

"Watu wamekuwa wakipotea mazingira ya kutatanisha na hatujui mazingira haya kwanini yanatokea kwa sisi tunaoishi pembezoni mwa hifadhi hii," amesema Mhegete.

Baada ya kupokea malalamiko hayo Kinana amesema hakuna mwenye haki ya kukatisha uhai wa mtu mwingine. Akieleza kuwa iko haja kwa viongozi kuendelea kuwaelimisha wananchi kuheshimu mipaka iliyopo kati yao na hifadhi hiyo.

“Huwezi kuulaumu upande mmoja peke yake, lakini tunawajibu wa kuwaelimisha wananchi kuhusu kuheshimu mipaka lakini jambo moja la msingi hakuna mwenye haki ya kuondoa uhai wa mtu. Hata katika katiba haki ya kwanza ni kuishi,” amesema.

Kwa mujibu wa Kinana, serikali hairuhusu kuondolewa maisha ya mwananchi yoyote na kwamba vyombo vya ulinzi na usalama wajibu wake ni kufuata sheria.

Hata hivyo, amesema katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto hiyo tayari serikali imeunda kamati ndogo ambayo itafika mkoani Mara kufanya tathimini na hatimaye kutatua changamoto hiyo.