MKUU wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego, amewaagiza wakurugenzi wa halmashauri za wilaya mkoani hapa kufanya ukaguzi wa haraka kwenye shule za msingi na sekondari ili kubaini uhaba wa madawati na kuondoa tatizo la wanafunzi kujisomea wakiwa wamekaa sakafuni.
Dendego alitoa maagizo hayo jana baada ya kufanya ziara ya kushtukiza katika shule ya Msingi Bomani, iliyoko Manispaa ya Singida, baada ya kusambaa picha mitandaoni zikionesha wanafunzi shuleni hapo wakifanya mitihani yao wakiwa wamekaa chini.
Akizungumza na viongozi pamoja na walimu wa shule hiyo, Dendego alisema picha hizo zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii zimeleta taharuki kubwa kwa jamii tofauti na hali ilivyo shuleni hapo ambayo ina upungufu wa madawati manane.
Kutokana na tukio hilo, Mkuu wa Wilaya huyo, alionya tabia ya baadhi ya watu kuchukua picha na kusambaza mitandaoni bila kutafuta ukweli, jambo ambalo linapaswa kukomeshwa.
Dendego ametoa siku saba kwa Mkurugenzi wa Manispaa hiyo kuhakikisha anapeleka madawati yanayohitajika shuleni hapo ili wanafunzi waweze kujifunza na kujisomea katika hali bora na nzuri zaidi.
“Serikali imewekeza fedha nyingi katika uboreshaji wa elimu nchini, vitu kama hivi vinapotokea vinaleta mshtuko mkubwa siyo kwa wazazi tu hata kwa jamii nzima kwa ujumla, jambo ambalo halileti picha nzuri na lazima likomeshwe,” aliagiza.
Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Joachim Msechu, alikanusha kuwa shule hiyo haina upungufu mkubwa wa madawati, ni kwamba hawana madawati manane tu na walikuwa kwenye mchakato wa kukarabati madawati mengine yaliyoharibika ili wanafunzi waweze kuyatumia.
Mkuu wa Wilaya ya Singida, Godwin Gondwe, amemhakikishia Mkuu wa Mkoa huo kuwa, maelekezo aliyoyatoa watayafanyia kazi kuanzia sasa ili kuondoa mapungufu madogo madogo yanayotokea katika sekta ya elimu, lengo ni kuimarisha shughuli za ufundishaji wa wanafunzi shuleni yenye watoto 894 na walimu 16
Wiki iliyopita gazeti hili liliripoti wanafunzi 485 wa Shule ya Msingi Kimpungua iliyoko Manispaa ya Singida, wakikakaa chini kutokana na ukosefu wa madawati.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED