Makonda aagiza watumishi waliokula fedha za TASAF kufikishwa kortini kesho

By Beatrice Shayo , Nipashe Jumapili
Published at 12:41 PM Apr 28 2024
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda.

MKUU wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, ameagiza watumishi waliokula fedha za Mpango wa Kunusuru Kaya maskini nchini (TASAF) Sh milioni 428 kufikishwa mahakamani kesho.

Makonda aliyasema hayo leo jijini Arusha wakati akizungumza na waandishu wa habari amesema watumishi waliohusika na upotevu na wizi wa fedha hizo wafikishwe mahakamani kwa kuwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imekamilisha uchunguzi wake.

“Kwa masikitiko makubwa katika mkoa wa Arusha watumishi wameamua kutafuna fedha zilizolenga kwenda kuwasaidia wananchi wa hali ya chini zilizolenga kuboresha mazingira yao na miradi badala yake zimeishia kwenye mifuko ya watu,”amesema Makonda na kuongeza kuwa;

“Vyombo vimeridhika kwa uchunguzi uliofanyika mtu anaingiziwa Sh milioni 428 kwenye akaunti yake sio msambazaji wala sio mkandarasi waliomuingizia hizo fedha wanazunguka upande wa pili na kwenda kuzichukua wanagawana na kumuachia fedha katika akaunti yake kama kishika uchumba kwa kazi ya kuficha fedha za wananchi wa hali ya chini,”.

Amesema watumishi hao wakaamua kula fedha hizo na kujifanya ni miradi yao anaishukuru TAKUKURU kwa kazi waliyoikamilisha.

“Nimeelekeza wote watuhumiwa kupanda mahakamani siku ya Jumatatu na jambo la pili mtandao wote wanaojihusisha na masuala hayo iwe ni Tasaf, Wakala wa Barabara wa Vijijini na Mjini (TARULA), Wakala wa Barabara (Tanroads), maji, umeme, elimu, afya na mradi wowote imefika wakati wa kila mmoja kufunga mkanda hatutamuonea haya mtu kwa kuwa rushwa ni adui wa haki,”amesema Makonda.

Aidha, Makonda amesema watahakikisha miradi saba ya TASAF inachungunguzwa kwa kina ambayo ina thamani ya zaidi ya Sh bilioni 1.8 inawezekana imejengwa chini ya kiwango haionyeshi thamani ya fedha na watu kunufaika na fedha hizo.