Mangariba wabadili mbinu ukeketaji

By Thobias Mwanakatwe , Nipashe Jumapili
Published at 08:29 AM Jun 16 2024
Ukeketaji.
Picha: Mtandao
Ukeketaji.

BAADHI ya mangariba mkoani hapa wameibuka na mbinu mpya ya ukeketaji kwa kuwachukua watoto chini ya umri wa miaka mitano wakidai wanakwenda kuwatibu ugonjwa ujulikanao kama ‘lawalawa’.

Vitendo hivyo vya ukeketaji vimekuwa vikipigiwa kelele na serikali na makundi mbalimbali ndani ya jamii kwa kuwa vimekuwa vikiwakatili watoto, hasa  mabinti.

Mratibu wa kupinga ukatili kutoka Shirika la Empower Society Transform Lives (ESTL), Ruth Ndagu, aliyasema hayo juzi wakati akitoa elimu kwa wanafunzi katika shule nane za msingi na sekondari zilizoko kata ya Ngimu, wilayani Singida.

Shirika hilo linajishughulisha na kuwezesha jamii na kubadili maisha.

Ndagu alisema wakeketaji hao, maarufu kama mangariba, wanachokifanya hivi sasa ili wasibainike na kuchukuliwa hatua, ni kuwachukua watoto wakidai wanawatibu maradhi kumbe wanakwenda kuwakeketa.

“Ukatili mkubwa umeongezeka kwa watoto chini ya miaka mitano ambapo ukeketaji unafanyika kwa njia tofauti watoto hawafahamu kama wanakeketwa, wazazi na walezi wanaelezwa wanakwenda kutibiwa ugonjwa wa lawalawa ambao kwa kabila la Kinyaturu unajulikana kama madudu,"alisema.

Hawa Hussein, ambaye ni ngariba mstaafu, alisema ukatili huo umekuwa ukifanyika nyakati za usiku baada ya mangariba kukubaliana na wazazi na walezi  wa watoto. Alisema kutokana na mbinu wanayotumia ya matibabu imekuwa vigumu kujulikana.

Mwalimu wa Shule ya Msingi Ngaramtoni, Dotto Kasese, alisema watoto wengi wanaofanyiwa ukeketaji huo ni wa kuanzia umri wa miaka sifuri hadi mitatu.

Kutokana na kuwapo kwa hali hiyo, Kasese aliiomba serikali kufanya uchunguzi na kuchukua hatua kwa wahusika kwa kuwa vitendo hivyo vimekithiri vijijini na kuchangia kuharibu watoto.

Ofisa Elimu Kata ya Ngimu, Tabu Omari, aliishukuru Shirika la ESTL kwa kutoa elimu ya ukeketaji kwa wanafunzi wa shule hizo, ambayo itasaidia watoto kujua madhara yake na kuwa mabalozi wa kuwaelimisha wazazi na walezi.

Utafiti uliofanywa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), miaka mitatu iliyopita, ulibainisha kuwa mikoa inayoongoza kwa ukeketaji nchini kuwa ni Mara, Dodoma na Singida.

Katika mikoa hiyo, wananchi wanaamini ili mtoto wa kike avuke kutoka katika hatua ya kuwa msichana kwenda hatua ya utu uzima ni lazima akeketwe.