Miundombinu iliyoathiriwa na mvua sasa kurejeshwa

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 09:03 AM May 26 2024
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Picha: Mpigapicha Wetu
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

WAZIRI mkuu, Kassim Majaliwa amesema serikali imejipanga kuendelea kurejesha miundombinu yote ya barabara zilizoathiriwa na mvua zilizonyesha nchini.

Amesema hayo jana alipokagua daraja lililoko katika kijiji cha Nambilanje ambalo limeharibika kutokana na mafuriko. Daraja hilo linaunganisha wilaya za Liwale na Ruangwa. 

“Kwa wakati huu ambao barabara nyingi zimekatika na kuharibiwa na mvua, Si mkoa wa Lindi pekee, eneo hili TANROADS (Wakala wa Barabara Tanzania ) wameshafika, wameangalia hii hali na Waziri wa Ujenzi (Innocent Bashungwa)  ameshatoa taarifa kwamba wanaendelea na uhakiki,” alisema.  

Majaliwa alisema serikali inasubiri taarifa ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kuhusu kuisha kwa mvua ili itoe fedha na kutangaza zabuni za ujenzi za ukarabati na matengenezo ya maeneo yote yaliyoathiriwa. 

Aidha, Majaliwa alisema Rais Dk. Samia Suluhu Hassan anatoa pole kwa Watanzania wote waliopata athari ya mvua hizo. 

 “Nawasihi muendelee kuwa watulivu na mjenge imani na Serikali yenu Mheshimiwa Rais katika mipango yake nina uhakika daraja litafanya kazi,” alisema. 

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu aligawa pampu 20 na mabomba yatakayotumika kumwagilia kwenye bustani za mboga kwa wakazi wanaojishughulisha na kilimo hicho eneo la Nandagala, Ruangwa mkoani Lindi. 

Majaliwa aliwataka wananchi wachangamkie fursa ya  kilimo hicho kwani kilimo cha mbogamboga kinawezesha mkulima kupata kipato cha haraka. 

 “Tunataka eneo hili liwe kituo kikuu cha upatikanaji wa mazao ya mboga,” alisema Majaliwa. 

Aidha, alisema serikali imeendelea kuweka mikakati endelevu ya kukuza sekta ya kilimo ikiwemo mpango wa kutumia mabonde mbalimbali nchini ikiwemo yaliyo katika wilaya ya Ruangwa kukusanya maji ya mvua na kuyatumia katika kilimo na mifugo.