Mwinyi awashukuru viongozi, wananchi dua kwa baba yake

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 03:18 PM Apr 14 2024
Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi.
PICHA: IKULU ZANZIBAR
Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi.

RAIS wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amewashukuru wananchi na viongozi wa mkoa wa Kaskazini Unguja kwa kuendelea kumwombea dua na hitma baba yake mzazi, Hayati Mzee Ali Hassan Mwinyi, aliefariki dunia hivi karibuni.

Taarifa uiliyotolewa na Idara ya mawasilianio Ikulu, Zanzibar, amesema Dk. Mwinyi ametoa shukrani hizo baada ya ibada ya sala ya Ijumaa iliyofuatiwa na visomo mbalimbali, hitima na dua kweye Msikiti wa Hidaya, Kilimani Tazari, mkoani humo.

Akizungumza kwa niaba ya familia yake, Dk. Mwinyi amewashukuru wananchi hao kwa mapenzi yao kwa Mzee Mwinyi tangu walipomuuguza hadi alipofariki  Februari 29, mwaka huu.

Naye Mkuu wa Mkoa huo, Rashid Hadid Rashid, amesema wanachi wa kijiji cha Kilimani Tazari na vijiji Jirani, kwa makusudi waliamua kukaa pamoja kumwombea dua Marehemu Mzee Ali Hassan Mwinyi, viongozi walio hai na wazee wa vijiji hivyo waliofariki dunia.

Akizungumza kwenye ibada hiyo, Sheikh Khamis Abdul Hamid amewahusia waumini wa Kiislam kuendelea kufanya mema na kumcha Mwenyezi Mungu kwa haki ili roho zao zikawekwe mahala pema baada ya kufa.

Mapema, akikhutubu kabla ya sala ya Ijumaa, Khatib Sheikh, Omar Abdi amewasihi wananchi na waumini wa dini ya Kiislam kuendelea kujenga hofu kwa Mwenyezi Mungu kwa kukithirisha ibada hata baada ya kumalizika kwa Mwezi mtukufu wa Ramadhan.

Amehusia kwamba Mwenyezi Mungu hayuko Mwezi wa Ramadhan pekee bali siku zote, hivyo aliwanasihi waumini hao kuendeleza ibada kwa siku za kawaida kama ilivyokuwa Ramadhan.

Katika ibada hizo za visomo na dua na hitma pia waliombewa viongozi walioko serikalini, wastaafu, masheikh na wazee walio hai na waliotangulia mbele ya haki ndani na nje ya mkoa huo.

Hafla hiyo pia imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa dini na serikali akiwemo Mufti Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Saleh Omar Kaab, na Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Rashid Hadid.