Nchimbi ataka wanaoanguka waache nongwa

By Halfani Chusi , Nipashe Jumapili
Published at 01:13 PM Apr 14 2024
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi.
PICHA: CCM BLOG
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi.

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, ametaka viongozi wa chama hicho wanapoanguka katika nafasi za uongozi kutotafuta mchawi na kuacha kuwanunia walioshindwa bila sababu.

Pia amekemea kitendo cha baadhi ya viongozi wa chama hicho cha kuwadhalilisha watumishi wa umma pale wanapofuatilia utekelezaji wa ilani ya chama na kutengeneza mazingira ya kutaka fedha kinguvu.

Balozi Nchimbi ametoa kauli hiyo mjini hapa katika ziara ya viongozi wakuuu wa chama hicho inayohusisha mikoa sita, huku akisisitiza kuwa uongozi bora huanzia ngazi ya familia.

Katika ziara hiyo, kiongozi huyo ameambatana na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makala, na Katibu wa NEC, Oganaizesheni, Issa Ussi Haji ‘Gavu’, ambao watafanya ziara katika  mikoa ya Rukwa, Songwe, Mbeya na Ruvuma.

“Uongozi bora unaanzia ngazi ya familia, lakini wewe unatoka nyumbani kwako hakuna anayekuunga mkono, hujaongea na watoto wako halafu unataka uchaguliwe wewe. Mwisho wa siku utasikia familia yako wanasema huyu akishinda kazi tunayo. Lakini  pia tabia ya kukataa matokeo tuiepuke kwa maslahi ya chama na serikali yetu.

“Hakuna mwenye akili asiyejua CCM ikipasuka nchi imepasuka. Ndiyo maana wapinzani baadhi wanatuambia, “jitahidi chama chenu kisipasuke” chama cha siasa madhubuti kinaongozwa na misingi ya kidemokrasia,” amesema.

Balozi Nchimbi amesema kiongozi wa kweli ni yule anayekubali matokeo bila kusita na kujitolea mfano kuwa aligombea mara 28 na kuanguka mara nne.

“Nilipigwa kisawasawa lakini nilikubali matokeo. Wale mtakaoshinda mtumie nafasi hiyo kuwaunganisha wananchama na kufanya kazi pamoja na walioshindwa ili kushirikiana kuijenga nchi pamoja,” amesema.

Nchimbi amesema mtu hawezi kuwa kiongozi kama ataanguka katika uchaguzi na kuamua kutuma wapelelezi kujua kama wanamwongelea vibaya.

“Huo si uongozi. Kuna wanachama ambao ni viongozi ndani ya CCM, wanalazimisha kupewa fedha na watumishi wa serikali, hao ni wezi kama wezi wengine tu, tunataka viongozi watende haki mtu akiulizwa haki inapatakana wapi, aseme inapatikana CCM. Ninaomba tuutimize wajibu huo bila kigugumizi,” amesema.

Katika mkutano huo, Balozi Nchimbi amewaahidi wananchi mkoani humo kushughulikia tatizo la umeme lililoibuliwa na Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Katavi, Idd Kimanta, ambalo limedumu kwa muda sasa.

Naye Makalla  amesema katika ufanyaji wake wa kazi katika nafasi hiyo, hatoshughulikia migogoro ambayo kesi zake zipo mahakamani kwa kuwa,  hicho ndicho chombo pekee cha kutoa haki.

“Hatuwezi kuiamrisha mahakama. Sisi  tutawasaidia wananchi kwenye matatizo ambayo bado hayajafika mahakamani, lazima tuwe wa kweli, tuwaeleze wanachi, siyo kumwaaminisha kitu ambacho huwezi kumsaidia.

“Kuna mtu aliwahi kuja ofisini kwangu ameshindwa kesi katika mahakama zote halafu anataka mimi Mkuu wa Mkoa (wakati huo) ndio nitatue shida yake. Hilo haliwezekani nitakachoshauri labda akakate rufani.

“Mimi nitashughulikia migogoro ambayo bado haujafika mahakamani, kwenye kikao cha ndani tumepokea taarifa ya chama na serikali yapo mazuri  yaliyofanywa na tumeridhishwa na utekelezaji wake," amesema Makalla.

Amesema wakati anaondoka Katavi, baadhi ya maeneo yalikuwa hayana lami, lakini ndani ya miaka mitatu ya Rais Samia Suluhu Hassan yamewekwa.

"Ushuhudua mwingine Katavi ilikuwa inachukuliwa kama mkoa uliofungwa kwa sababu kulikuwa hamna barabara wala uwanja wa ndege lakini leo nimetua hapa kwa ndege.

"Kila mwanachama anapaswa kutembea akisimulia mambo mazuri yaliyofanywa, na wapo watu tukikaa bila kusema watasema serikali haijafanya chochote, mwambie ukitoka hapa mpaka Sikonge unateleza, Tabora unateleza mwambie kwa kujiamini kabisa,” amesema Makalla 

Gavu amewataka wanachama kutafuta viongozi wenye sifa wataokinadi chama hicho bila gharama na kuweza kushinda nafasi zote za uchaguzi.

 “Tunahitaji kuwatumikia na kutumwa na mtu mwenye uthubutu na utayari, kama ni mwenyekiti ajue kilichompa thamani ni CCM. Wakati wa kukumbatia watu umepita. Tunahitaji mtu ambaye akisimama atakuwa nyenzo ya kutufikisha kwenye ushindi,” amesema.