Samia akerwa ubabe ma-RC, ma-DC

By Paul Mabeja , Nipashe Jumapili
Published at 08:05 AM Jun 16 2024
Rais Samia Suluhu Hassan.

RAIS Samia Suluhu Hassan, amesema bado kuna wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya wanaendeleza ubabe akionya kwamba, kuna usugu wa aina fulani ambao unahitaji kushughulikiwa.

Rais Samia aliyasema hayo jana Ikulu jijini Dodoma katika hafla ya kupokea Ripoti ya Kamati ya Kuandaa Mkakati wa Utekelezaji wa Mapendekezo ya Tume ya Kuangalia Jinai Nchini.

“Matumizi mabaya ya madaraka linatakiwa kuwa jambo la kihistoria. Waraka namba moja uliotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi unaowataka wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya kuzingatia ipasavyo matumizi ya sheria inayowapa mamlaka ya ukamataji uende ukatekelezwe vyema.

“Pamoja na waraka ule ambao umetolewa mwaka jana (2023) bado kuna wakuu wa mikoa wakuu wa wilaya wanaendeleza ubabe kule maeneo waliko.

“Nikimnukuu makamu mwenyekiti wakati ananipa utangulizi anasema, wakati wa kikao chao na wakuu wa wilaya. Mmoja  alithubutu kusimama na kusema ‘mimi ni mwakilishi wa Rais hapa kwa hiyo lolote lililopo hapa ni la kwangu, hata kama ni mahakama ikiamua sivyo mimi nitatengua’,”alisema.

Kutokana na hayo kuendelea, Rais Samia alisema anadhani bado hawajakaa vizuri ama elimu zaidi inahitajika au kuna usugu wa aina fulani unahitaji kushughulikiwa na kuagiza waraka ule uzingatiwe na kufanyiwa kazi vizuri.

“Nilikuwa ninazungumza na Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Haki Jinai, Balozi Ombeni Sefue, ameniambia kuwa wakati wa kukutana na wakuu wa mikoa na wilaya wengi hawakushiriki vikao hivyo, lakini pia hata mawaziri baadhi yao hawakushiriki.

“Sasa ninaomba kamati hii kuhahakikisha makundi haya yote yanafikiwa kwani bila kuwa na uelewa kuhusu jambo hili, hatuwezi kulifanikisha ni lazima kila mtu apate uelewa,” aliagiza Rais Samia.

Alisema kutokana na idadi ya washiriki wa vikao vya ufafanuzi wa mkakati kuwa ndogo ipo haja kwa Tume hiyo kurudia tena ili makundi yote kupata uelewa zaidi wa mkakati huo ulioundwa.

Rais Samia alisema bado baadhi ya wakuu wa mikoa na wilaya wanatumia nafasi zao vibaya ikiwamo kukamata na kuwaweka mahabusu wananchi bila kufuata sheria ya utumishi wa umma.

“Ninaishukuru kamati kwa mapendekezo yake ikiwamo hili la mtumishi ambaye atafanya kosa kuweka wananchi ndani na mwananchi akilalamika na kubainika kuwa alikamatwa kinyume hilo, litakuwa kosa lake na serikali haitahusika na kitu chochote,” alisema.

Awali, akiwasilisha taarifa hiyo, Balozi Sefue, alisema moja kati ya mambo ambayo wameyabaini ni bajeti pungufu kulinganisha na hali halisi kwenye taasisi nyingi za haki jinai nchini katika miaka mitatu ya fedha.

Alisema taasisi hizo ni mahakama, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Jeshi la Polisi, magereza, TAKUKURU na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya.

“Katika kipindi hicho cha miaka mitatu taasisi hizi zilipokea Sh. trilioni 1.99 sawa na wastani wa Sh. bilioni 662.6 tu kwa mwaka. Shilingi trilioni 1.86 kutoka bajeti ya serikali na Sh. bilioni 127.78 kutoka washirika wa maendeleo,” alisema.

Alisema kamati imefanya uchambuzi wa mahitaji ya rasilimali fedha ambayo yatahitajika na sehemu kubwa ikiwa na marekebisho ya miundombinu ya majengo na vitendea kazi.

“Hii ni kutoka na hali iliyobainika kuwa kwa miaka mingi sana bajeti iliyokuwa inatolewa kwa taasisi hizi ilikuwa chini sana ya mahitaji halisi.

“Kamati inapendeza uwapo mpango mahsusi wa kuongeza bajeti katika miaka mitano mfululizo ya kutekeleza mkakati huu ili kupunguza kwa kiasi kikubwa upungufu ulipo ikiwamo ujenzi wa majengo na miundombinu mingine,” alisema Balozi Sefue.