Utata watanda nyumba ya mstaafu kubomolewa

By Thobias Mwanakatwe , Nipashe Jumapili
Published at 08:16 AM Jun 09 2024
Mwalimu mstaafu mjane, Amina Mghenyi, akiwa nje ya nyumba yake ambayo mahakama imeamuru ibomolewe.
PICHA THOBIAS MWANAKATWE
Mwalimu mstaafu mjane, Amina Mghenyi, akiwa nje ya nyumba yake ambayo mahakama imeamuru ibomolewe.

Hali hiyo ya utata inatokana na mwalimu huyo mstaafu kuwa na hati ya umiliki wa eneo na kulipa kodi ya ardhi kisheria na kuambiwa kuwa aliuziwa eneo ambalo lilikuwa na mgogoro.

Amri hiyo ya mahakama inatokana na hukumu ya kesi iliyotolewa na mahakama ambayo anasema hajawahi kuitwa mahakamani hata siku moja. 

Kutokana na hali hiyo, mstaafu aliyeitumikia serikali kwa miaka 39, amemwomba Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jerry Silaa, kuingilia kati baada ya nyumba yake kutaka kubomolewa kwa agizo la mahakama.  

Akizungumza na waandishi wa habari jana katika nyumba hiyo iliyoko eneo la Mahambe, Manispaa ya Singida, Mghenyi alisema nyumba yake hiyo imewekewa alama ya X ambayo inatakiwa kubomolewa Juni 16, mwaka huu. 

Alisema kiwanja alichojenga nyumba yake alikinunua Juni 16, 2018 kwa Sh. milioni 17 kwa John Gwau ambaye ni marehemu na kupewa hati namba 573 na tangu alipokinunua na kujenga nyumba, amekuwa akikilipia halmashauri kama taratibu na sheria zinavyoelekeza. 

Mghenyi alisema katika hali ya kushangaza, Mei 31, mwaka huu nyumba yake iliwekewa alama ya X na dalali wa mahakama kutoka kampuni ya Taomtra Limited na kutakiwa  kuibomoa mwenyewe Juni 15, 2024 na asipofanya hivyo, ifikapo tarehe hiyo litapelekwa tingatinga na kuibomoa. 

Alisema kinachomshangaza ni kwamba kesi ambayo ilipelekwa mahakamani na mlalamikaji, Suzana Mahami, kuhusu kiwanja cha nyumba hiyo,  hajawahi kuitwa mahakamani na wala hakuwa mshitakiwa katika kesi hiyo. 

Mahami, ambaye ni mlalamikaji katika kesi hiyo, alisema ni kweli mwalimu huyo hakuhusika katika kesi aliyoipeleka baraza la  ardhi bali alimshtaki aliyeuza kiwanja hicho palipojengwa nyumba ya mwalimu huyo kwa kuwa aliuziwa eneo hilo kinyume cha sheria na utaratibu. 

Alisema kimsingi mwalimu huyo, kesi hiyo imemgusa kwa sababu amejenga nyumba yake katika kiwanja ambacho kilikuwa na mgogoro bila yeye kujua. 

"Mimi kimsingi sina tatizo na mwalimu huyo. Ninachotaka  kama atataka nilipwe gharama zangu za kesi na kupewa kiwanja kingine halafu mimi nitamwachia eneo hilo alipojenga nyumba yake," alisema Mahami.  

Naye Sixmund Gwau ambaye ni mtoto wa John Gwau aliyeuza kiwanja hicho kwa mwalimu huyo mstaafu, alisema baba yake alipouza eneo hilo, hakukuwa na mgogoro  wowote na kusisitiza kuwa mwalimu huyo aliuziwa kihalali kwa kufuata taratibu zote. 

Naye Balozi wa Mtaa wa Mahembe, Asia Hamis, alisema serikali iangalie namna ya kumsaidia mwalimu huyo mstaafu na mjane kwa kuwa kama nyumba yake itabomolewa, familia yake ataipeleka wapi, amezeeka na hana nguvu za kufanya kazi kupata pesa za kujenga nyumba nyingine.

 Diwani wa Kindai, Imari Hamis, alisema tangu 2015 alipoingia kwenye udiwani, hajawahi kusikia eneo hilo lina mgogoro na kinachoshangaza hukumu ya kesi hiyo ilitolewa tangu 2012 halafu utekelezaji wake unafanyika mwaka huu kitu ambacho kinatia shaka. 

"Naiomba serikali  na mahakama imsaidie mjane huyu kuokoa maisha yake kwani nyumba yake ikibomolewa na hali aliyokuwa nayo ni wazi kuwa kutasababisha maisha yake kuwa magumu sana," alisema. 

Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi Singida, Bahati Colex, alisema hukumu ya kesi hiyo ilitolewa katika Mahakama ya Kuu Dodoma na wao walipewa amri na kumtafuta dalali wa mahakama kwa ajili ya kutekeleza kuibomoa nyumba hiyo. 

Mkurugenzi Mtendaji wa  Taomtra Limited, Salim Adam, alisema wakiwa madalali wa mahakama walipewa kazi hiyo ya kutaka kubomoa nyumba hiyo na Baraza la Ardhi.