Vigogo CHADEMA wachuana uchaguzi kanda

By Vitus Audax , Nipashe Jumapili
Published at 03:35 PM Apr 14 2024
Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA Tanzania Bara, Benson Kigaila.
PICHA: MAKTABA
Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA Tanzania Bara, Benson Kigaila.

BAADHI ya wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wamejitosa kuchangisha fedha za wagombea kuchukua fomu za uchaguzi wa viongozi kanda, huku vigogo ndani ya chama hicho wakichuana kuongoza kanda hizo.

Siku mbili zilizopita CHADEMA kilifungua rasmi dirisha la kuchukua fomu kwa ajili ya uchaguzi wa viongozi wa kanda nne za kiutawala katika chama hicho.

Kwa mujibu wa Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA Tanzania Bara, Benson Kigaila, mchakato wa kuchukua fomu ni endelevu mpaka Aprili 22, mwaka huu.

Wakati hayo yakijiri, uchaguzi huo umeonekana kuwa na ushindani mkubwa tofauti na miaka iliyopita kutokana na vigogo mbalimbali kutajwa kunyukana katika kanda zao, huku wengine wakiweka wazi nia zao mitandaoni.

Miongoni mwa vigogo wanaotajwa kuchuana katika kanda hizo ni pamoja na nafasi ya Mwenyekiti Kanda ya Victoria ni Mwenyekiti wa Baraza la Vijana CHADEMA (BAVICHA) Taifa, John Pambalu, ambaye tayari ametangaza nia kupitia mtandao wake wa X na anatarajia kukabiliana na Hezekiah Wenje.

Wengine ni aliyekuwa Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi  Sugu’ atakayechuana na Mchungaji Peter Msigwa anayetetea nafasi yake kwa Kanda ya Nyasa.

Kanda ya Magharibi mchuano ni baina ya Mawakili Dickson Matata na Peter Madeleka huku Kanda ya Serengeti ikitarajiwa kuwakutanisha Emmanuel Ntobi, John Heche, Lukas Ngoto na Gimbi Masaba.

Wakati mchuano ukiwa mkali kutokana na kuwapo vigogo hao, baadhi ya wana CHADEMA katika makundi sogozi mbalimbali ya chama hicho, wameonyesha kutembea kwenye nyayo za Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kuanzisha ‘mikeka’ kuwachangia wagombea  wanaowapenda ili kuchukua fomu.

Mmoja wa wachangishaji hao ni Machael Masele aliyeanzisha michango kwa ajili ya kumchangia fomu Wenje, ili agombee nafasi ya Mwenyekiti Kanda ya Victoria ambako mkeka huo hadi kufikia jana, ulikuwa na wachangiaji 29 huku Sh. 352,000 zikiwa zimechangwa.

Licha ya mchango huo kuendeshwa katika makundi ya chama, kumeibuka hisia mbalimbali kwamba huenda ukakigawa kabla ya uchaguzi. Mchangiaji  mmoja,  Kapalatu Masanja, alitolea mfano kwa wajumbe wa Tume Huru ya Uchaguzi.

“Kesho wajumbe wa Tume Huru ya Uchaguzi Tanzania nao wanakuja na mahaba kwa Rais Samia Suluhu Hassan, wanamchangia fomu pia ni wapigakura na ni wasimamizi wa kura yaani sipati picha (akimaanisha katika makundi hayo wapo wajumbe, wasimamizi pamoja na wapigakura),” amesema.

Lackson Mjuni, amesema utaratibu huo hauna tofauti na alichokiita ‘uchawa’ (kujipendekeza) na kuhoji kuwa hali hiyo haina tofauti na upande wa watu wa CCM kuwa kiongozi anayehitaji nafasi hawezi kukosa fedha ya kuchukulia fomu.

Hata hivyo, Katibu wa CHADEMA Kanda ya Victoria, Zakaria Obad, ameingilia mjadala huo na kusema suala hilo si kosa na yeyote anaweza kufanya hivyo kutokana na kukutanishwa na siasa.

“Mashabiki wana haki ya kushindanisha mtu wao ili mradi wasiende nje ya katiba, kanuni na miongozo ya chama hususani miongozo wa taratibu za kuendesha kampeni za uchaguzi ndani ya chama toleo la 2012,” amesisitiza.

Aidha, ametoa wito kwa wanachama hao kuchukua fomu kwa kuwa dirisha bado liko wazi na kila mwanachama ana haki ya kuchukua kwa mujibu wa katiba na kanuni za chama hicho.