Waja na kampeni kila kona kudhibiti ukatili

By Sabato Kasika , Nipashe Jumapili
Published at 04:43 PM Jun 02 2024
Kampeni nikiendelea katika maneno mbalimbali ya Kipunguni hadi sehemu ya kucheza bao.
Picha: Sabato Kasika
Kampeni nikiendelea katika maneno mbalimbali ya Kipunguni hadi sehemu ya kucheza bao.

KITUO cha Sauti Kipunguni jijini Dar es kimeanza kampeni ya kupambana na ukatili ya kijinsia kwa kutoa elimu katika masoko, vijiwe na maneno mbalimbali ya Kata ya Kipunguni.

Mkurugenzi wa kituo hicho, Seleman Bishagazi  amesema mwaka huu wa 2024 ni wa ukeketaji kwa kuwa unagawanyika kwa mbili.

Amefafanua kuwa katika jiji la Dar es Salaam, eneo hilo la Kipunguni huwa linakumbwa na vitendo vya ukeketaji.

"Kutokana na matukio hayo, kumeanzisha kampeni maalum ya kutoa elimu dhidi ya ukatili yenye lengo la kuishirikisha jamii kuzuia ukatili," amesema Bishagazi.

Amesema kampeni hiyo ni ya miezi sita, na kwamba wanatarajia kufika maeneo mbalimbali ikiwamo sokoni, gereji, mama lishe, viwanja vya mpira, stendi za bajaj, bodaboda, vikoba, vijiwe vya kahawa, minada na vijiwe vya madalali.

"Elimu tutakayoifikisha ni  nanma ya kugundua viashiria vya ukatili, sehemu za kuripoti ukatili, aina za ukatili, afya ya uzazi, ulinzi wa mtoto madhara ya rushwa ya ngono na umuhimu wa wanaume kushiriki kuzuia ukatili hasa ukeketaji, huku tukikumbuka huu ni mwaka wa ukeketaji na huwa unafanyika Desemba," amesema.

Amesema kampeni hiyo ilizinduliwa na diwani wa kata hiyo Steven Mushi, na kwamba inalenga kuwafikia vijana, akina mama, wanaume ,wazee na watu wenye ulemavu.

Bishagazi amesema, kampeni hiyo inatokana klabu ya kupinga ukatili ndani ya jamii, na kwamba moja ya azimio ni kuhakikisha wanamfikia kila mwanajamii popote alipo.

"Hatuwezi kusimama kutoa elimu kwa sababu hatuna rasilimali fedha bali tunatumia fursa zilizopo kufikisha ujumbe," amesema.