Ziara ya Dk. Nchimbi yaacha kicheko kwa wananchi, asikiliza kero hadi usiku

By Romana Mallya , Nipashe Jumapili
Published at 12:22 PM Jun 02 2024
Mmoja wa wananchi wilayani Babati, mkoani Manyara akimkabidhi Balozi Dk. Emmuel Nchimbi,  nyaraka mbalimbali za kero yake.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mmoja wa wananchi wilayani Babati, mkoani Manyara akimkabidhi Balozi Dk. Emmuel Nchimbi, nyaraka mbalimbali za kero yake.

ZIARA ya Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, imeleta kicheko kwa wananchi kutokana na kiongozi huyo pamoja na wenzake kutenga muda wao hadi usiku kusikiliza kero za mwananchi mmoja mmoja na kuzitatua kila mkoa waliokwenda.

Katika ziara hiyo inayohusisha mikoa mitano baadhi ya wanachi wameridhishwa na namna kiongozi huyo pamoja na wenzake walivyojishusha kwao na kusikiliza matatizo yao hata yanayohusu mambo binafsi.

Viongozi wengine alioambatana nao katika ziara hiyo ni pamoja na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Taifa, CPA Amos Makala, Katibu wa NEC, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa  (SUKI), Rabia Abdallah Hamid, ambao wameshirikiana kuzipokea na kuzitatua kwa haraka zile zinazohitaji majibu ya haraka na nyingine wakiwapa majukumu watendaji husika kuzifanyia kazi.

Yohana Laiza,  mkazi wa Ngaiti, anasema viongozi wanaposhuka kwa wananchi na kutatua matatizo waliyonayo inakuwa rahisi kufahamu kero zao na kuzitafutia ufumbuzi kwa haraka, kuliko kukaa tu ofisini.

"Nimefurahishwa na namna viongozi hawa walivyoamua kuacha ofisi zao na kuja kwetu kutusikiliza, inatia moyo na huku ndio kujenga nchi kwa ushirikishwaji, wao wametueleza yaliyofanyika na sisi tumeeleza changamoto zetu na nyingine tumeona zimetatuliwa hapa hapa," anasema.

Mwasiti Mohamed, mkazi wa Babati Mjini, anasema yeye ni mjasiriamali  mdogo anayejishughulisha na uuzaji wa matunda na kwamba amesikia fursa ya  mikopo maalum ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa wajasiriamali, hivyo anaishubiria kwa hamu ili kukuza biashara yake.

Akihutubia jana katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa stendi ya zamani ya mabasi Babati Mjini, Balozi Nchimbi aliwaahidi wananchi kuwa yupo hapo kwa ajili ya kuwasikiliza na kutatua kero mbalimbali zinazowakabili.

Amewaeleza kuwa serikali imefanya mambo mengi makubwa ikiwamo kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ili kuleta maisha bora kwao, hivyo ni wajibu wa viongozi kwenda kwa wananchi kusikiliza kero zao na kuzitafutia ufumbuzi haraka.

Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa chama hicho, CPA Amos Makala, alisema maandamano ni uzururaji kama mzururaji yeyote  kwa kuwa hayana athari.

Makala anasema, "Wanasema hali mbaya ya maisha, wewe hufanyi kazi unazurura tu barabarani utapata wapi kipato wewe inawezakana wana stress (msongo wa mawazo) wameshauriwa na madaktari kufanya matembezi ya kutembea.

Aidha, amewakumbusha viongozi ngazi mbalimbali kuhakikisha kero za wananchi zinasikilizwa na kutatuliwa na ofisi za CCM kuwa wazi muda wote.