Mchawi hajasinzia usiku na mchana kwa miaka 30!

By Flora Wingia , Nipashe Jumapili
Published at 04:54 PM Apr 14 2024
Imani za kishirikina.
PICHA: MAKTABA
Imani za kishirikina.

KARIBU tena msomaji wangu tuendelee na ushuhuda wa mchawi mmoja aliyeamua kujilipua hadharani na kutoa siri zote. Baadaye akaokoka kwenye kongamano la injili lililoongozwa na Mchungaji Ezekiel kutoka Kenya kwenye uwanja wa Biafra, Kinondoni DSM, Machi 22, mwaka huu.

Ushuhuda huu nilianza kuutoa wiki iliyopita kwa wale waliosoma safu hii ya Maisha Ndivyo Yalivyo, kwenye NIPASHE hii kila Jumapili. Hakika ni Mwanga wa Jamii.

Alielezea jinsi alivyoshirikishwa katika uchawi ambao alisema pia ukoo wao ulikuwa ni wachawi wakubwa. Akataja baadhi ya silaha wanazotumia kufanya ushetani huo kuwa ni pamoja na Simba, chatu, nyuki, vyura na fisi.

Akaelezea mambo ya kichawi aliyofanya katika maisha yake hadi kupelekea kukatwa mguu baada ya kukiuka masharti kwa wakuu wake wa kichawi. Baada ya ulemavu huo akakimbilia kuokoka. Hebu msikie anavyoeleza mwenyewe.

Baada ya kuwa mlemavu nikaokoka. Walokole wakaja kuniombea nyumbani kwangu wale wanyama Simba, chatu, fisi wakawa havionekani, walipotea lakini bado vitu viwili vikawa vinanisumbua. Vyura bado vimo ndani na hawa nyuki walihama kwangu wakahamia kwenye kiwanja changu kingine.

Lakini ile nyumba ya milango minne ipo bado sijaivunja. Lakini nikiwa nimelala usiku, huwa napigwa na yule chatu. Ananitoa kitandani ananitupa chini kisha anatoweka. Kwa hiyo bado hiyo roho inanisumbua. Ninafunga sana, ninaomba sana na kutoa sadaka, lakini bado huyo roho mchafu amenizidi nguvu.

Mchungaji Ezekiel akamkatisha na kumwambia, “ni kwa sababu ulikataa kutoa sadaka ya mke, baba, mama au mtoto. Tena wakitaka watakutoa huu mguu mwingine. Wewe ni kiongozi wa wachawi na unaasi na madhabahu ya uchawi haijavunjwa ndio maana chatu anakuja anafanya kazi yake.

Siku ile simba atakuja atakumaliza kabisa. Wakiwa wanataka wakupige, wakuadhibu, wanatuma ugonjwa ili ukatwe mguu. Kwa sababu wewe haustahili kukatwa mguu wala mimi Ezekiel siwezi kukatwa mguu sababu niko katika ufalme wetu. Ndio maana nasimama tangu saa saba ni giza tu limeingia. 

Sababu natumika katika ufalme wetu, badala ya mimi kukatwa mguu nawasaidie wale wanaolemaa, wanapata nguvu wanaendelea. 

Ezekiel anaendelea kusema: “Ukiona nyoka ndani ya samaki, fahamu ameasi madhabahu yake. Sasa wakati unapigwa mguu ulikataa kutoa sadaka, wanaweka ugonjwa kwako ili utoe.”

Sasa ile kwamba nyoka anakuchapa kofi unaanguka chini, siku wakiamua kuja simba wanaweza kukufanya jambo lolote.  Mtoa shuhuda akakiri ni kweli na kusema; Nyoka anapokuja hujiviringisha mguuni na kumtupa chini.

Halafu kuna kipindi mbuzi beberu wanakuja wawili, mwekundu na mweupe wanagombana. Wameshikana vichwa, lakini huyo mwekundu anakuja kwangu, huku mweupe anamsukuma mwenzie ili waje wanigonge. Wakishanikaribia tu usingizi unaisha.

Nina miaka 30 sijasinzia usiku wala mchana. Sijapata usingizi hata dakika tano! Nimewahi kuoa wanawake 15 na ninao watoto 21. Mke wangu wa mwisho huyu hapa ni wa 16, wengine wote 15 walishaondoka kwangu.

Mke huyu wa 16 alipohojiwa na Mchungaji Ezekiel alisema ana watoto sita na mumewe huyo. Hao wanawake walioondoka walikuwa wakiishi na bwana huyu miaka mitatu wanaondoka. Baba huyu anasema alizaliwa mwaka 1961 na huyu mke wa mwisho umri wake miaka 43.

Akasema ana watoto wa kike wanne warembo sana. Lakini hakuna mwanaume aliyekosea hata namba aje awaoe. Niliua sana sana mimi.

Msomaji wangu, kipengele hiki cha kuua sana fuatilia wiki ijayo mambo mazito sana. Aliua watu wa aina gani na kwa njia zipi, usikose uhondo huo japo wa kusikitisha katika safu hii.

Bila shaka msomaji wangu umeanza kupata picha mambo yanayofanyika katika ulimwengu wa giza unaotawaliwa na shetani. Wapo watu wanaojikuta wakifanya mambo mabaya pasipo wao kutaka kama baba huyu. Hakupenda mambo ya kichawi lakini akalazimishwa. Na hata alipojaribu kukataa alikumbana na adhabu kali kama alivyopigwa na nyoka na pia kukatwa mguu.

Wapo watu waliowatoa kafara wanafamilia, baba, mama, watoto kwa udanganyifu wa shetani ili kupata na mali nyingi. Hata hivyo, watu wa aina hii wameishia pabaya sana. Kazi ya ibilisi ni kuua, kuharibu na kuchinja.

Tafuta nguvu ya Mungu mpendwa kudhibiti wachawi. Je, una maoni, kisa? Ujumbe 0715268581.